Hata hivyo, tayari watu wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa ajili ya kuhojiwa zaidi kutokana na mauaji hayo.
Mahole aliuawa nyumbani kwake juzi majira ya saa 2:30 usiku katika eneo la Katanini, Kata ya Karanga Manispaa ya Moshi baada ya kuvamiwa wakati akishuka katika gari lake akitokea mazoezini.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi (ACP), Moita Koka, aliliambia Nipashe kwa njia ya simu kuwa, saa chache baada ya kifo chake, makachero wa polisi waliwatia mbaroni watu wawili wakihusishwa na mauaji hayo.
Kaimu Kamanda huyo aliwataja waliokamatwa kwa mahojiano kuhusiana na mauaji hayo kuwa ni mfanyakazi wa ndani (house boy) wa mfanyabiashara huyo, Godfrey Thobias Tarimo (22), mkazi wa Usseri, Rombo na Revocatus Martin Massawe (21), mfanyabiashara na mkazi wa Karanga.
“Jirani wa marehemu ambaye ni Kapteni wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ndiye aliyegundua kuuliwa kwa mfanyabiashara huyo, kwa kupigwa risasi mgongoni na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi,”alisema Kamanda Moita
Mwili wa mfanyabiashara huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, ukisubiri uchunguzi wa kitabibu na baadaye kuandaliwa kwa ripoti ya uchunguzi ya kifo chake.
Hata hivyo, taarifa ambazo si rasmi kutoka kwa watu wa karibu na mfanyabiashara huyo, zilidai kuwa mauaji ya ‘Tajiri Mtoto’ yanahusishwa na visa vinavyotokana na masuala ya kibiashara.
Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Karanga, Jonathan Makupa (Chadema), mfanyabiashara huyo maarufu alikuwa akifanya biashara za kununua na kuuza bidhaa za ujenzi kati ya miji ya Dubai (Falme za Kiarabu), Mombasa (Kenya), Dar es Salaam na Moshi alipokuwa akiishi.
“Kwa jinsi nilivyokuwa nikimfahamu Mahole, hakuwahi kubahatika kuoa, lakini aliwahi kunifundisha hata mimi kufanya biashara katika miji ya Dar es Salaam na Moshi. Hakika tumepoteza mtu muhimu na ambaye alikuwa msaada mkubwa katika jamii,” alisema diwani huyo.
Wawili mbaroni mauaji milionea ‘Tajiri Mtoto’ Moshi
31Dec 2015
Nipashe
Wawili mbaroni mauaji milionea ‘Tajiri Mtoto’ Moshi
WATU wanaosadikiwa kuwa majambazi wamemuua kwa kumpiga risasi mgongoni mfanyabiashara wa mji wa Moshi, Joseph Mahole (36), maarufu kama 'Tajiri Mtoto', na kisha kutokomea kusikojulikana pasipo kupora fedha wala mali zake.
GEOFFREY KAMWELA RPC KILIMANJARO