Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitoa rai hiyo wakati akizungumza na wakimbizi kutoka nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) waliopo katika kambi ya Nyalugusu, wilayani Kasulu, Kigoma jana.
Alisema kuna taarifa juu ya baadhi ya wakimbizi wasiowaaminifu kujihusisha na vitendo vya kutumia silaha katika matukio ya uhalifu, uporaji na mauaji.
Aliwataka wakimbizi wanaokimbia nchi zao kuingia nchini bila ya silaha ikiwamo mabomu na risasi, vitu ambavyo vinahatarisha usalama wa watu na mali zao.
“Ninawataka kila mmoja wenu awe mlinzi wa mwenzake na kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama na kwa watumishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) juu ya mtu au kikundi cha watu wanaojihusisha na vitendo ya uhalifu hususani kutumia silaha,” alisema.
Majaliwa pia aliwataka wakimbizi hao kuacha tabia ya kutoka nje ya kambi kwani ni kinyume cha utaratibu na sheria na usalama wao.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, alisema serekali imeandaa utaratibu wa kuwapeleka kwenye Gereza la Mwisa wakimbizi ambao wametoka kwenye majeshi ya nchi zao kwa kipindi cha miezi mitatu ili waweze kutengenezwa kisaikolojia warudi katika hali ya raia wa kawaida na kisha kurudishwa kambini kujiunga na wakimbizi wenzao.
Aliwahakikishia wakimbizi hao ulinzi na usalama wao pamoja na mali zao kwa muda wote watakaoishi kambini hapo. Aidha,waziri huyo alisema katika kukomesha tabia ya wakimbizi ya kuharibu mazingira, serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na UNHCR itagawa majiko yenye matumizi kidogo ya kuni.