Tuipe ushirikiano TBS kung’oa mizizi ya wasiozingatia viwango

26Jan 2016
Salome Kitomari
Nipashe
Tuipe ushirikiano TBS kung’oa mizizi ya wasiozingatia viwango

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limetangaza kampeni ya kuondoa sokoni matairi ya mitumba, nguo za ndani za mitumba, vilainishi vya magari na mitambo na bidhaa zote ambazo hazijathibitishwa ubora wake.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekaidi agizo hilo.
Nimevutiwa kuandika kuhusu tangazo hili au karipio hili kwa kuwa siyo mara ya kwanza TBS kutangaza na kuchukua hatua za kukamata na kutekekeza nguo hizo ikiwa ni jitihada za kuziondoa sokoni.
Nguo zilizokamatwa na kuchomwa moto, ni kutoka kwa wauzaji wa kawaida kama machinga na kuteketezwa mara kwa mara.
Uwezekano wa kukabiliana na uingizwaji wa bidhaa hizi ni mkubwa iwapo mamlaka za serikali zitashirikiana kwa karibu, ikiwa kuna mkakati thabiti wa kukabiliana na tatizo husika.

Kwa mfano, nguo hizi huingizwa nchini kwa kutumia Bandari na mipaka iliyopo nchini, na mzigo husika unapofika bandarini hujulikana na aina gani na hata wafanyabiashara wajanja wanapoficha kuna uwezekano mkubwa wa kufungua kujua kilichopo ndani yake.
Pia, maduka yanayouza mabelo ya mitumba kwa bei ya jumla na rejareja yanafahamika mahali yalipo, hivyo mamlaka za serikali zikishirikiana ni wazi kuwa, zitafanikiwa kudhibiti uingizwaji na kusambaa kwa nguo hizo mapema.

Kwa sasa kinachofanyika anayeshikwa na mbuzi ndiye mwizi wa mbuzi, pasipokuangalia mzizi wa tatizo husika unaanzia wapi.
Navyofahamu kila mzigo unaopita katika njia halali za nchi yetu kuingia nchini TBS huhusika katika kuangaliaubora wa bidhaa husika, kabla haijamfikia mlaji au mtumiaji.

Katika hili la nguo za ndani inashangaza zinapokamatwa kwa muuzaji, ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo maarufu kama machinga, wakati ingewezekana kuzikamata kwa muingizaji wa jumla (wholesale) kabla ya kwenda kwa muuzaji wa kati (middle men) na baadaye kwa muuzaji wa mwisho ambaye ni mtu anayeganga maisha mtaani.
Machinga wengi wamekutwa na janga la mali zao kuteketezwa kwa moto, kwa kuwa wanauza nguo ambazo zimepigwa marufuku, lakini wahusika wanaozileta nchini wanafahamika lakini hatuoni hatua zikichukuliwa dhidi yao.
Kuliko kuhangaika na dagaa au unayekamatwa na mbuzi, ni vyema akatafutwa anayeleta mbuzi na achukuliwe hatua ili aache kuagiza mizigo kama hiyo, kwa kuwa hairuhusiwi nchini.
Hakuna ubishi, leo hii ukitembelea soko maarufu la mitumba la Memoria mjini Moshi, kuna eneo maalum la kuuza nguo hizo, pia masoko ya Mchikichini, Mwenge, Ilala na kwingine jijini Dar es Salaam hutumia muda mwingi kuelekezwa zinakouzwa.
Ukitembelea zaidi maeneo ya Ilala na Kariakoo ndiko kuliko na maduka ya jumla ya nguo husika, hivyo kama mamlaka za serikali zimedhamiria kukabiliana na jambo hilo, ni vyema zikaanzia huko kuliko kuhangaika na wanaobeba mbili au tatu.
Nguo hizi zinapigwa marufuku kila uchao, elimu inatolewa lakini wauzaji hawaachi kununua kwa sababu mbalimbali.
Kubwa inaelezwa ni ubora wake, kwa kuwa unaponunua sidiria ya mtumba baadhi huamini kuwa itatumika kwa muda mrefu zaidi.
Bila kujali madhara anayoweza kupata kinachoangaliwa ni kutumia fedha kidogo aliyonayo kununua kitu kitakachodumu kwa muda mrefu, kuliko kutumia fedha mara kwa mara kununua bidhaa ya dukani ambayo haidumu.
Kwa upande wa matairi, hili halihitaji kulindwa au kuachwa liendelee kuwapo kwa kuwa madhara yake ni ya haraka zaidi kuliko nguo za ndani.

Kila siku idadi ya watu wanaopoteza maisha kutokana na ajali za barabarani, na hivi karibuni Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani, Mohamed Mpinga, alieleza chanzo cha ajali nyingi ni magari yanayoingizwa nchini ambayo ni ya mtumba yana kasoro nyingi kwenye breki na matairi.
Unakuta mtu ana gari la mtumba, matairi ni yale aliyonunua ambayo yamechoka na anapotaka kubadili hukimbilia kununua ya mtumba, hivyo tunaitaka TBS kuongeza ukali katika utekjelezaji wa majukumu yake.
Elimu kwa umma inatolewa, lakini sasa ni wakati wa kuhakikisha utekelezaji unaingia kwenye vitendo katika kuzikataa bidhaa hizo, ambazo kwa namna moja au nyingine zimesababisha madhara kwa watumiaji.
Pamoja na tahadhari hiyo, kinachotarajiwa kwa sasa ni kuona wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza nguo hizi wanachukuliwa hatua, zinateketezwa kabla ya kumfikia mtumiaji kuliko kuzikamata kwa machinga anayedunduliza kujiendeleza kimaisha.