Ilikuwa ni Ligi Kuu msimu uliopita wa 2014/15, lakini ukaisha bila kiungo yoyote wa kati (Na. 6 na 8) kufikia idadi hiyo ya mabao.
Kwa miaka ya hivi karibuni viungo wengi wa Kitanzania wamekuwa hawana uchu wa kufunga magoli na kazi hiyo kuwaachia washambuliaji kwa kiasi kikubwa.
Angalau wanaoonekana kufanya kazi yao vizuri ni viungo wa pembeni, kwani tumewaona kina Simon Msuva ambaye alikuwa mfungaji bora msimu uliopita na hata Mrisho Ngasa ameonekana kufikisha magoli 10 au kuzidi karibuni kila msimu kabla ya kutimkia Afrika Kusini kucheza soka la kulipwa.
Viungo wengi wa kati wa Kitanzania wamekuwa wakicheza zaidi na jukwaa, wakipenda sana kanzu, tobo, chenga, visigino na hata kutaka kufunga kwa madaha, kitu ambacho kimekuwa kikizinyima timu zao ushindi au magoli mengi kwenye mchezo husika.
Pamoja na kutokuwa na juhudi za kutaka kufunga magoli, wamekuwa wakishindwa hata kupangua ngome za timu pinzani na kuwarahisishia mastraika wao kufunga magoli rahisi kwa kutoa pasi za mwisho zisizo na doa.
Badala yake wamekuwa akichukua mipira kwa madaha, kugeuka kama pia, kupiga pasi nyingi za pembeni kulia na kushoto badala ya kusonga mbele, kupasua mabeki, au kupiga pasi za mbele.
Hii ndiyo tofauti na viungo wa zamani kina Rashid Gumbo, Athumani Idd 'Chuji' na Mwinyi Kazimoto ambao wakati walipokuwa kwenye ubora wao. Mkumbuke pia Haruna Moshi 'Boban' alipokuwa kwenye kiwango chake cha juu.
Viungo wa kileo ambao wanasajiliwa kwa mamilioni ya pesa hadi Sh.Milioni 60, ni tofauti kabisa na viungo waliokuwa na uwezo mkubwa.
Ramadhani Lenny, Athumani China, Issa Athumani, Hamisi Gaga, Mtemi Ramadhani, Octavian Mrope, Kaingilila Maufi, Hussin Masha na wengine wengi walikuwa mafundi wa pasi za mwisho na kufunga.
Mara ya mwisho kwa kiungo wa kati kufunga magoli yasiyopungua 10 kwenye Ligi Kuu Tanzania ilikuwa ni 2011/12 wakati kiungo mkabaji wa Simba, marehemu Patrick Mafisango alipomaliza ligi akiwa na magoli 11.
Sina rekodi ya pasi za mwisho, lakini nina uhakika alitengeneza pasi nyingi za mwisho kwenye timu yake ya Simba, akiwalisha kina Felix Sunzu na Emmanuel Okwi na kuifanya timu hiyo kuwa tishio na yenye mafanikio.
Kwa bahati mbaya sana, Mafisango hakuwa Mtanzania, ila Mnyarwanda mwenye asili ya Congo DR.
Kikosi chochote kikiwa na viungo wa kati ambao wana uwezo wa kufunga, basi kina asilimia nyingi ya kutwaa ubingwa au kufanya vizuri kwa sababu hata kama mastraika watawekwa chini ya ulinzi, viungo wataokoa jahazi.
Wakati nikitegemea atatokea Mtanzania kurithi za Mafisango, hali imekuwa tofauti kwani ametokea raia mwingine wa kigeni ambaye ni Thabani Kamusoko,
Mzimbabwe huyo tayari ana magoli matano baada ya mzunguko wa kwanza. Kama akiendea hivi ana uwezo mkubwa wa kufikisha magoli 10 aliyokuwa akiyataka yule jamaa, lakini pia kumpiku Mafisango na kuwaacha viungo wa Kibongo wakibaki na aina yao ya uchezaji isiyo na tija uwanjani.
Wakati viungo wa Kitanzania wakiacha 'chali' na Kamusoko, kuna Mtanzania anaitwa Shomari Kapombe. Anatisha kwa magoli! Ameibukia kuwa mfungaji stadi kwenye timu yake ya Azam kiasi cha kuibeba hata kwenye mechi ngumu.
Kapombe aliyekuwa kiungo zamani (sasa anacheza nafasi ya beki wa pembeni kulia), ameshafikisha magoli saba hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza katikati ya wiki.
Binafsi ninampongeza mchezaji huyo wa zamani wa Simba aliyewahi pia kukipiga Ufaransa kwa kuwafunda viungo wa Tanzania.
Yeye na Kipre Tchetche ndiyo wanaongoza kwa kufunga magoli mengi kwenye kikosi cha kocha Muingereza Stewart Hall cha Azam.
Lakini pia ndiye beki pekee nchini aliyefunga idadi hiyo kubwa ya mabao mpaka sasa kwenye ligi hiyo.
Wala sisiti kusema kuwa ni beki anayekifukuzia kiatu cha dhahabu pamoja na kina Amissi Tambwe, Hamis Kiiza, Donald Ngoma na wengineo.
Kama akiendelea hivi, anaweza kuingia kwenye rekodi ya kuwa beki aliyefunga magoli mengi kwenye historia ya Ligi Kuu nchini, lakini pia kuwaacha kwa mbali viungo wa Kitanzania ambao wamekuwa na mbwembwe nyingi uwanjani bila kufunga magoli.
Inawezekana Kapombe akafikisha magoli 10 au zaidi na kumzidi hata marehemu Mafisango.
Ninaamini Kapombe ni somo kwa viungo wetu wa Kitanzania kuwa soka si kupiga chenga na mbwembwe nyingi uwanjani bila kufunga magoli au kutoa pasi za mwisho.
Ni matumaini yangu kuwa watarekebika kwenye mzunguko wa pili na kuanza kufanya kazi waliyoajiriwa kuifanya badala ya kuendelea staili yao ya chenga nyingi zisizo na mashiko.
Ninaamini itakuwa changamoto na aibu kwao ikiwa Kapombe atafikisha magoli 10 au zaidi, huku viungo wakishindwa kufikia idadi hiyo ya magoli.
Viva Kapombe, umetisha!
Beki Kapombe anafunga, viungo mko wapi?
25Jan 2016
Nipashe
Beki Kapombe anafunga, viungo mko wapi?
- DONDOO MUHIMU: Mara ya mwisho kwa kiungo wa kati kufunga magoli yasiyopungua 10 kwenye Ligi Kuu Tanzania ilikuwa ni 2011/12 wakati kiungo mkabaji wa Simba, marehemu Patrick Mafisango alipomaliza ligi akiwa na magoli 11.
NILIWAHI kusoma mahali fulani mtu mmoja akitoa ofa ya Sh. 500,000 kwa Mtanzania anayecheza nafasi ya kiungo akifunga magoli 10 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ndani ya msimu mmoja.
Beki wa Azam FC, Shomari Kapombe (kulia) akiwa kazini wakati moja ya mechi za Ligi Kuu.