Tuache lawama, tuisaidie serikali kufikia malengo

25Jan 2016
Sema Usikike
Tuache lawama, tuisaidie serikali kufikia malengo

KUWAPO kwa migomo ya wafanyakazi katika viwanda na taasisi za umma katika maeneo mbalimbali kote nchini, kunaonyesha wazi kuwa huenda hali hiyo inatokana na kutoridhiswa na utekelezaji wa ahadi za Serikali zinazotolewa kwa wafanyakazi kila wakati.

Baadhi ya wafanyakazi wa TRL wakiwa kwenye mgomo

Ingawa kuwapo kwa migomo hiyo hakuashirii taswira njema kwa ustawi wa taifa, lakini kunatoa jibu la ukubwa wa majukumu ambayo serikali inalazimika sasa na baadaye kutokwepa kuyasimamia na kuyapa vipaumbele vya dhati.
Katika mazingira yoyote yale, kuwapo kwa migomo na maandamano ya mara kwa mara kunaweza kuchochea matumizi ya muda yasiyo na tija kwa taifa hasa ikizingatiwa migomo mingine inahusisha taasisi binafsi.
Hata jinsi ambavyo vyombo vya ulinzi na usalama vinavyoshiriki katika kutafuta suluhu, bado kunaonyesha kuibua hasira za watu wakiwamo watumishi wa umma ambao wanaamini kuandamana labda kunaweza kuwasaidia kufikisha ujumbe wao.
Kwa wanaofuatilia kwa karibu maendeleo ya nchi na uwajibikaji wa serikali kwa watumishi wake na watu wa kawaida, watakubaliana nami kuwa kwa miaka mingi sasa malalamiko juu ya kutotimiziwa kwa mahitaji yao au kutopewa uhuru wa kufanya mambo bila kuvunja sheria yanazidi kuongezeka.
Mbali na watumishi, malalamiko yameendelea kusambaa hadi katika maeneo mengine ikiwamo ngazi za maamuzi ambapo watu wamekuwa wakihoji kwa nini ahadi mbalimbali za serikali hazitekelezeki.
Baadhi yao wanaweza kudai kuwa huenda ufinyi wa bajeti unaotokana na mapato kidogo unachangia serikali kushindwa kuwahudumia watumishi wake, lakini sasa tunashughulikia serikali ya awamu ya tano wakikabiliana vikali ili kutafuta njia bora za kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato.
Wengi wanafahamu fika kuwa, serikali ya Dk.John Magufuli imeanza kwa mkakati maalum wa kukusanya fedha kutoka katika vyanzo vyake na tayari kwa mwezi mmoja wa 12 ilikusanya zaidi ya Sh.trilioni 1.3 na kuvunja rekodi ya Sh.bilioni 900 iliyowekwa na serikali ya awamu ya nne.
Kabla ya Dk. Magufuli kuingia Ikulu, malalamiko yalikuwa yamesambaa hadi katika ngazi za mitaa ambako watu wa kawaida wanasikika wakilalamikia maamuzi mbalimbali yanayotolewa na viongozi dhidi ya raia kiasi cha kukatisha tamaa kimaisha.
Kwa mfano malalamiko yanayoendelea kuwapo ndani ya kampuni ya Reli (TRL) zamani ikijulikana kama shirika la Reli ambapo kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, tishio la migomo limekuwa likichukua nafasi kubwa pengine hata watu kufanyakazi.
Tangu shirika hilo likiwa chini ya wizara moja ya Miundombinu na sasa Uchukuzi, pande zinazosuguana zimeendelea kunyoosheana vidole, kila upande ukilalamikia mwingine.
Mfano mwingine ni jinsi ambavyo serikali inavyosuasua kufuatilia malalamiko ya Watanzania walio wengi walioajiriwa au kufanyakazi katika kampuni binafsi ambako kilio cha kulipwa fedha kidogo kimekuwa kikisikika mara kwa mara.
Katika hili, Watanzania wengi wamejikuta wakitumikishwa kwa ujira mdogo usiofika hata kima cha chini cha mshahara cha Sh.100,000 jambo ambalo kila wakati linasababisha malalamiko.
Siamini kama kweli serikali haijui kuwapo kwa kampuni za aina hii na pia sina uhakika kama haiwezi kuchukua hatua kumaliza ili kujenge imani kwao, licha ya kwamba hivi sasa inajuhusisha na ufuatiliaji wa vibali vya wafanyakazi wa kigeni jambo linaloonyesha kwamba dhamira yake ni kukusanya zaidi mapato.
Maeneo hayo ni mfano tu wa maeneo mengi ambako kuna malalamiko mengi kati ya yote yakielekezwa kwa viongozi wa serikali wa ngazi tofauti, ingawa huu ni wakati muafaka kwa Watanzania kusaidia kila jitihada inayofanywa na serikali ili kufikia malengo.