Katika idadi hiyo wavulana ni 584 wakati wasichana ni 379, ambao wote kwa ujumla wao ni sawa na asilimia sita ya walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka huu.
Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Ofisa Elimu wa mkoa huo, Nelas Mulungu, katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichokutanisha wadau mbalimbali wa elimu.
Inasikitisha kusikia idadi hiyo ya wanafunzi kutofanya mtihani, kwa sababu ya utoro, licha ya serikali kutoa maelekezo kwamba, wanafunzi wote waliosimama kutokana na sababu mbalimbali warudi shuleni.
Kuendelea kuwapo kwa utoro huo ni sawa na kukwamisha juhudi za kutaka kila mtoto apate elimu, hivyo ingekuwa ni vyema jamii ikichukua hatua kukabiliana na mtindo huo.
Katika karne hii ya 21 elimu haipaswi kuwekwa pembeni hasa kwa kuzingatia kwamba kila jambo linahitaji kujua kusoma, kuandika kuhesabu na ujasiriamali, hivyo ni vyema wadau wa elimu wakiwamo wazazi, walimu, viongozi na walezi kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni.
Njia hiyo inaweza kusaidia kupunguza kama si kumaliza utoro shuleni ambao umeendelea kuwapo licha ya serikali kumfanya kila jitihada za kuhakikisha kila mtoto anapata elimu kuanzia ya awali na kuendelea.
Ninaamini kwamba, Tanzania bila utoro shuleni inawezekana, iwapo kila mmoja atafanya sehemu yake kuhakikisha wanafunzi wanahudhuria vipindi vyote vya masomo, badala ya kudhani ni jukumu la kundi fulani.
Katika kuonyesha umuhimu wa elimu kumekuwapo kaulimbiu mbalimbali nchini, zinazotumika kueleza umuhimu huo, miongoni mwake ikiwa ni 'elimu ni ukombozi, ni kazi', msingi wa maendeleo na elimu ni ufunguo wa maisha.
Kaulimbiu hizo zinalenga kutaka kuonyesha ni kwa kiasi gani elimu ni muhimu katika nyanja mbalimbali za maisha ya binadamu, lakini inasikitisha kusikia kuwa bado kuna watu hawaoni umuhimu wa kusoma, wala kuwapeleka watoto wao madarasani licha ya serikali kugharamia masomo.
Ikumbukwe, miaka ya mwanzo ya uhuru wa Tanganyika ambao sasa umetimiza miaka 61, ujinga uliorodheshwa na waasisi wa taifa letu kama miongoni wa maadui wa maendeleo.
Hatua hiyo ilitokana na kwamba, ikiwa jamii ingeondokana na ujinga ingekuwa imepiga hatua mojawapo ya maendeleo, na kwa kutambua hilo, serikali ilitumia mbinu mbalimbali, kuhakikisha kila mtoto anapata elimu.
Ilikuja na mpango wa elimu kwa wote, ukilenga kuwapatia watoto wote wenye umri wa kuanza shule kuwa madarasani.
Mambo mengine mengi yalifanyika na hadi sasa inaendelea kufanyika, lengo likiwa ni kutaka kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu tena katika mazingira ya karibu.Mazingira hayo ya karibu yanachagizwa na kuwapo kwa shule za sekondari za kata ambazo zimeenea kote nchini, ingawa sasa inaonekana bado wapo baadhi ya wanafunzi ambao hawaoni umuhimu wa elimu.
Kuendelea kuwapo kwa utoro shuleni, kunaweza kuathiri lengo namba nne la Maendeleo Endelevu (SDGs) ambalo linaelekeza kuwapo elimu bora yenye usawa inayotoa fursa kwa wote kujiendeleza.
Kama wanajamii, mashirika ya umma na binafsi, tuna nafasi ya kuhamasisha elimu bora yenye usawa katika mikakati ya maendeleo ya kiuchumi na kuhakikisha mafunzo yanaleta tija katika soko la ajira.
Lakini utoro shuleni unaweza kuwa ni moja ya tishio la kutotimiza lengo hilo iwapo jukumu la kuhamasisha elimu litabaki kwa serikali na wadau wachache, ni vyema jamii nzima ikavalia njuga utoro huo na kuukomesha.
Ni muhimu kutafuta chanzo cha utoro huo na kama kitakuwa ni kukosekana chakula shuleni, basi wadau wa elimu, wazazi na walezi, wahakikishe watoto wanapata chakula cha mchana shuleni ili kupunguza utoro huo.
Viongozi wa Kamati ya Maendeleo ya Kata nao wafanye juu chini ili chakula kwa wanafunzi shuleni, kiwe ajenda ya kudumu katika mikutano yao, kwani ukosefu wa chakula umekuwa ukidaiwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia utoro kwa baadhi ya wanafunzi.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







