Kwa utoro huu serikali ‘isipoe’

28Dec 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kwa utoro huu serikali ‘isipoe’

MOJA ya matukio yanayochafua maendeleo ya  elimu mwaka huu ni utoro wa baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, jambo linaloweza kuchangia kukwamisha maendeleo yao kielimu.

Karibu mwaka mzima kulikuwa kunaripotiwa utoro kutoka shule mbalimbali hasa za sekondari. Kwa mfano, Februari mwaka walikuwapo watoro  436 katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani Mtwara .

Hawa walitakiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, lakini walikuwa bado hawajaripoti shuleni. 

Utoro huo ulisababisha viongozi kutangaza msako wa wazazi wa wanafunzi hao, huku watendaji kuanzia ngazi ya vijiji na kata katika halmashauri hiyo wakishiriki msako huo. 

Wakati Mtwara kukiwa hivyo, wanafunzi 405 wa Shule ya Msingi Kumkambati iliyopo Kijiji cha Mvugwe mkoani Kigoma wameshindwa kumaliza elimu ya msingi.Sababu inayotajwa na Mwalimu Mkuu , Ndabilole Raphael, ni utoro sugu, mimba na ndoa za utotoni. 

Ni katika mahafali ya 19 ya shule hiyo, tatizo linafichuliwa, akifafanua kuwa ni wanafunzi 163 pekee walioandikishwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi katika shule hiyo kati ya 568 walioanza darasa la kwanza mwaka 2016. 

Kwa ujumla matukio ya utoro yapo mengi katika shule mbalimbali, lakini hili la wanafunzi  963 wa shule za sekondari mkoani Njombe, kutofanya mtihani wa kidato cha pili nalo mwiba wenye ncha kali. 

Hayo yalibainishwa hivi karibuni, katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na Ofisa Elimu Nelas Mulungu, akifafanua kuwa mojawapo ya sababu za kutofanya mtihani ni utoro. 

Aidha, janga hilo limesababisha wanafunzi wa kiume 584 na wasichana 379 kutofanya mtihani, kitendo ambacho ni vyema kitafutiwe dawa ya kudumu ili elimu ipewe kipaumbele. 

Inashangaza wakati huu serikali inagharamia elimu kuanzia ya awali hadi kidato cha sita lakini kuna watu wanaopuuza kusomesha watoto, haipendezi. Aidha, karne  ya 21 elimu haipaswi kuwekwa pembeni, badala yake ipewe msukumo mkubwa kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya mtu mmoja na taifa kwa ujumla. 

Wazazi na walezi ni wadau wakubwa wa elimu, hivyo wangesimama kidete kwa kufuatulia kwa karibu maendeleo ya watoto wao shuleni, wanaweza kubaini nyendo zao kirahisi na kama ni mbaya wazitafutie ufumbuzi haraka. 

Vilevile ingependeza kama utoro huo utaishia mwaka huu wa 2023 na kuanza upya mwaka ujao kwa kuzingatia umuhimu wa elimu kuwa ndiyo ufunguo wa maisha. 

Ikumbukwe kuwa, serikali imekuwa ikifanya mikakati mbalimbali ikiwamo kutoa elimu bure, kwa lengo la kutaka kila mtoto aipate elimu tena katika mazingira mazuri. 

Kwa nini wanafunzi waendelee kuwa watoro wakati mazingira ya kupata elimu yamesharahisishwa, ikiwamo elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita? Jamii inataka nini kifanyike ndipo ione umuhimu wa elimu? 

Mtindo wa kuendelea kuendeleza utoro,  ni sawa na kukwamisha juhudi za serikali za kutaka kila mtoto apate elimu ambazo zinaonekana wazi hasa baada ya kuamua kutoa elimu bila malipo. 

Inasikitisha kuona kukiwa na jitihada hizo, halafu kunakuwapo na baadhi ya wanafunzi wa sekondari ambao wanaamua kuwa watoro au kuacha shule, kitendo cha kuendelea kumkumbatia adui ujinga. 

Tunapoelekea kuhitimisha mwaka huu wa 2022, ni vyema wazazi na walezi ambao watoto wao ni watoro wakatafakari na kuchukua hatua sahihi zitakazosaidia kukabiliana na utoro huo na kuutokomeza. 

Mwaka 2023 Tanzania yenye watoto wanaosoma iwe suala la kila mlezi au mzazi, iwapo kila mmoja kwa nafasi yake atawajibika kikamilifu kupambana nao kuanzia nyumbani hadi shuleni kwa kushirikiana na walimu na wadau wengine wa elimu.