Hatukuwaona, lakini tumesimuliwa na kufundishwa na tumeendelea kuwaimba na kuwaandika kama mashujaa. Hakuna hata mmoja kati yetu aliyeonyesha kuwa na shaka kama Mkwawa kweli aliwakong'ota Wajerumani.
Kuna kikundi cha watu kwa makusudi, wameamua kupotosha historia na rekodi za soka, na wamekuwa wakisapotiwa na baadhi ya watu ambao wanaheshimika, huku baadhi ya waandishi wa habari wakiwa wamekaa kimya, wakiwaangalia wapotoshaji wakichanja mbuga.
Kuna mtu mmoja aliwahi kusema mara nyingi uongo ukiachwa usemwe mara kwa mara unageuka unakuwa ni ukweli na watu wauamini.
Hivi karibuni kumezuka hoja ambazo hazina msingi zikidai eti Simba haijawahi kuingia hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wala fainali ya Kombe la Shirikisho. Kwa bahati mbaya sana kuwa watu wameanza kuamini. Kinachozungumzwa ni kwamba eti wakati wanacheza michuano hiyo ilikuwa haiitwi hivi inavyoitwa sasa.
Ukweli ni kwamba mwaka 1974, Simba iliingia nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika, ambayo kwa sasa ndiyo Ligi ya Mabingwa.
Ilianza kwa kuifunga Linale ya Lesotho jumla ya mabao 9-0, ikishinda ugenini mabao 3-0 na nyumbani 6-0, raundi ya pili ikaitandika Green Buffaloes ya Zambia jumla ya mabao 9-0, suluhu ya ugenini na mabao 9-0 nyumbani, ikatinga hatua ya robo fainali na kuifunga Hearts of Oak ya Ghana, ikitoka suluhu nchini na kwenda kushinda ugenini mabao 2-1, na kutinga hatua ya nusu fainali ambapo mambo hayakuwaendea vema wakatolewa kwa penalti 3-0 na Mehalla el Kubra ya Misri baada ya kila moja kushinda bao 1-0 nyumbani.
Mtu kuibuka leo kusema Simba haijawahi kufika hapo ni uongo mkubwa, kwani kilichobadilika hapo ni jina na mfumo tu, lakini hakuna timu yoyote iliyonyang'anywa taji. Hata Al Ahly iliwahi kutwaa kombe la Afrika wakati ikiitwa Klabu Bingwa Afrika, na mpaka sasa limebadilishwa jina linaitwa Ligi ya Mabingwa hatujawahi kusikia, Shirikisho la Mpira wa Miguu likiipunguzia idadi ya mataji kwa kufuta kile ilichokifanya wakati ikiitwa Klabu Bingwa.
Hata Kombe la Shirikisho Afrika limebadilishwa mara mbili. Lilianza kuitwa Kombe la Washindi barani Afrika, baadaye Kombe la CAF kabla ya 2004 kuitwa Kombe la Shirikisho.
Simba ilifika fainali mwaka 1993 kwa kuitoa Ferroviario de Maputo ya Msumbiji kwa bao la ugenini, suluhu nchini na bao 1-1 ugenini, ikaifunga Manzini Wanderers mabao 2-0, bao 1-0 nyumbani na ugenini, ikaenda kucheza dhidi ya USM El Harrach ya Algeria mabao 3-0, ikishinda mabao 3-0 nyumbani, na kufungwa 2-0 ugenini, ikaifunga Aviacao ya Angola mabao 3-1 nyumbani na kwenda kutoa suluhu ugenini kabla ya kutinga fainali ambapo ilitoa suluhu nyumbani na kufungwa mabao 2-0 nyumbani mgeni rasmi akiwa ni Rais wa awamu ya pili Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.
Mfumo au majina kubadilika haiwezi kufuta mataji au rekodi. Huwezi kusema Yanga si mabingwa mara 27 kwa sababu huko nyuma bingwa alikuwa hapatikani kwa kucheza ligi bali ni mfumo wa mtoano kuanzia mechi ya kwanza hadi ya mwisho.
Huwezi kuwanyima Simba ubingwa na Kagame mara sita kwa sababu kabla ya kuitwa Kagame lilikuwa likiitwa Kombe la Afrika Mashariki na watu waanze kuhesabu pale Rais Paul Kagame alipoanza kudhamini.
Yanga haiwezi kupunguziwa ubingwa wake kwa sababu wadhamini wanabadilika mara kwa mara, hivyo kila mdhamini mpya anayeingia ndiyo ianze kuhesabiwa. Wanahabari wanatakiwa wasikae kimya kwa hili. Soka ni mchezo wa rekodi na historia, bila hivyo hakuna soka na ladha yake itapungua.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







