Tuwe makini na wizi wa mitihani, tusipoziba ufa, tutajenga ukuta

04May 2023
Adolf F. Mkenda
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tuwe makini na wizi wa mitihani, tusipoziba ufa, tutajenga ukuta

MITIHANI ya mwisho ya kidato cha sita nchini, imeanza rasmi tarehe mbili mwezi huu wa tano na itakamilika tarehe 22 ya mwezi huu. Mitihani hii itafanyika, sambamba na mitihani ya wanafunzi wanaosomea ualimu.

Kadhalika, wapo wanafunzi ambao matokeo yao ya kidato cha nne yalifutwa na wameruhusiwa kurudia mitihani yao katika kipindi hiki cha mitihani. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, kupitia akaunti yake ya ‘Twitter’ ametuma salamu za heri kwa watahiniwa wote.

Mimi, pamoja na wenzangu wote kwenye Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia tunaungana na Rais wetu kuwatakia watahiniwa wote kila la heri kwenye mitihani hii.

Pamoja na salamu hizi, natoa wito kwa watahiniwa wote kuzingatia masharti na taratibu zote za mitihani. Kutokuzingatia masharti ya mitihani kunaweza kupelekea mtahiniwa kufutiwa matokeo yake ya mitihani. Walimu, wasimamizi wa mitihani, wazazi na walezi wote kwa pamoja, tuhimize watahiniwa wetu wafanye mitihani yao kwa kuzingatia masharti na taratibu zilizowekwa.

Napenda kutumia fursa hii, pia kutoa wito kwa Watanzania wote tushirikiane kutokomeza udanganyifu na wizi wa mitihani. Ni kweli kwamba, tatizo la wizi na udanganyifu wa mitihani ni dogo sana hapa nchini, lakini tusipoziba ufa tutajenga ukuta. Tutakosea sana, tukifumbia macho tatizo hili hata kama ni dogo sana. Kufumbia macho na kunyamaza hakuondoi tatizo. Kuficha tatizo na kutokuchukua hatua madhubuti ni sawa na kulea na kukuza tatizo.

Madhara ya kuenea kwa wizi na udanganyifu wa mitihani ni makubwa sana kwa taifa letu. Kwanza, wizi na udanganyifu wa mitihani unaathiri haki za watahiniwa wanaofanya mitihani yao kwa uadilifu.

Kwa kawaida, wizi na udanganyifu wa mitihani unaoratibiwa na watumishi wasio waaminifu, hunufaisha watahiniwa wenye uwezo zaidi wa kifedha; wenye uwezo mdogo wa kiuchumi hawawezi kulipa gharama za mitihani ya wizi.

Pili, wizi na udanganyifu wa mitihani unadumaza weledi katika taifa letu na kukuza ubabaishaji. Hatimaye, tutakuwa na madaktari wababaishaji, marubani wababaishaji, walimu wababaishaji na kadhalika.

Tatu, wizi na udanganyifu wa mitihani unaharibu malezi ya watoto na vijana wetu kwa kufundisha wizi na udanganyifu kwamba njia ya kutafuta mafanikio. Serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaojihusisha na wizi na udanganyifu wa mitihani.

Tunao maofisa ambao wako mahabusu wakikabiliwa na mashtaka ya madai ya kuratibu na kuwezesha wizi na udanganyifu wa mitihani. Zipo baadhi ya shule ambazo zimefutwa kama vituo vya mitihani kwa sababu ya wizi na udanganyifu wa mitihani.

Endapo itatulazimu, tutafuta usajili wa shule zinazoratibu wizi na udanganyifu wa mitihani. Ni matumaini yetu kwamba hatutalazimika kufuta usajili wa shule, lakini ni vyema ikafahamika kuwa hii ni hatua inayoweza kuchukuliwa.

Endapo sote tutashikamana na kukemea udanganyifu kwenye mitihani hapana shaka tutafanikiwa kutokomeza jambo hili. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuwa macho na kutoa taarifa endapo tutaona dalili zozote za udanganyifu kwenye mitihani. Mtu yeyote atakayekuwa na taarifa kuhusu vitendo vya wizi na udanganyifu wa mitihani tunamwomba atoe taarifa kwa mamlaka yoyote ya serikali iliyo karibu naye.

Namba ya simu ifuatayo itatumika pia kupokea taarifa zozote kwa siri za wizi na udanganyifu wa mitihani: Taarifa zinaweza kutumwa kwa simu 0759 360 000 na namba barua pepe ifuatayo:esnecta@necta.go.tz. Mwisho napenda tena kuwatakiwa watahiniwa wote kila la heri katika mitihani yao.

  • Mwandishi ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Top of Form

Bottom of Form