Wala siyo siri kabla ya wachambuzi hakukuwa na idadi kubwa ya mashabiki kama hivi sasa, lakini wachambuzi kutokana na kulizungumzia soka kwa ufasaha na ufafanuzi wa kina, limeonekana kupiga hatua kwa kupendwa na wengi.
Sipendi sana watu wanaowasakama wachambuzi kwa sababu watu hao ndiyo wameleta utamu wa mchezo huo, ingawa ni kweli baadhi yao wameonekana ni tatizo.
Tatizo la mtu mmoja mmoja, haliwezi kuwafanya wachambuzi wote waonekane wabaya.
Ni kwamba Maofisa Habari na wasemaji tu, ingawa hao wanaonekana hawaonyeshewi vidole baadhi yao hawatofautiani na baadhi ya wachambuzi. Kuna wakati wanakiuka na kwenda mbali zaidi ya kazi yao ya usemaji.
Wapo wasemaji badala ya kuzisemea timu zao, wao kutwa kazi yao kuelezea ubaya wa timu nyingine.
Sisemi kama kusiwe na utani, upo, lakini kwa asilimia ndogo. Msemaji kwa kiasi kikubwa anatakiwa kuiongelea na kuisifia timu yake kama vile anavyofanya Masau Bwire, hata kama haipo katika kiwango au ubora anaoizungumzia. Na asilimia chache zilizobaki utaitania timu ambayo unacheza nayo, huu ndiyo mpira kwa sababu kutaniana kupo na hata kupigana vijembe.
Sijaona Masau au Thobias Kifaru wakienda kwenye vyombo vya habari kuizungumzia timu nyingine kwa muda mwingi, kuliko kile kilichompeleka kuizungumzia timu yake.
Wakati mwingine inakuwa si utani tena, bali ni kuidhalilisha, kuitupia lawama taasisi nyingine na kuituhumu vitu ambavyo kama si kujificha kwenye kivuli cha soka, basi ni kesi kubwa inayoweza kumpeleka mtu mahakamani.
Pia kwa siku za karibuni kumezuka na mtindo wa wasemaji kuanza kuwasema watu binafsi, mambo binafsi badala ya klabu au timu.
Unashangaa kwenye redio, watu hawataniani tena mpira, badala yake mambo binafsi, na kutuhumiana uchawi na mambo yasiyofaa inashangaza.
Hapo ndipo nalia na watangazaji na wachambuzi, kumwacha mtu akituhumu mambo ya uchawi, kitu ambacho kwa kawaida hakina ushahidi na si vizuri kumwacha mtu kuelezea kitu ambacho kisheria iwapo mtuhumiwa akitaka ushahidi huwezi kuupata.
Najua inafanywa kwa kisingizio cha utani, lakani kwenye chombo cha habari ni hatari kwa sababu inaaminisha watu wengine kuamini mambo ya kishirikina, si kwenye soka tu, hata kwenye mambo mengine ya maisha, wakapatikana watu ambao kila anachotaka kukifanya, au kinachompata, basi anaamini ni uchawi tu.
Vipindi vya michezo vya asubuhi kwa sasa vinafuatiliwa na watu wengi na vinapendwa, hivyo visiruhusu sana wasemaji wanaokuja kupotosha kwa makusudi au kwa bahati mbaya kwa sababu, mashabiki wengi wanawaamini sana wachambuzi na wasemaji hao, hivyo kulishwa uongo ambao nao wanakuwa wanausambaza.
Inashangaza kuona msemaji anasema timu yake msimu ujao itaanza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika moja kwa moja katika raundi ya kwanza na si ya awali, huku wachambuzi wakimwacha tu akipotosha.
Sijajua kama na wao walikuwa hawajui au la. Ni hivi, ili timu icheze raundi ya kwanza ni lazima iwe angalau kwenye zile 20 bora za juu.
Ni klabu 10 tu za juu ndizo zinazotakiwa kuanza raundi ya kwanza, zilizobaki zote zinaanzia awali. Sasa inawezekana kuanzia ya 11 hadi ya 20 ikacheza kama zile 10 za juu hazitokuwa bingwa kwenye nchi zao. Mfano timu inayoshika nafasi ya 10 kama si bingwa au ya pili kutegemea nchi hiyo inaingiza timu ngapi, basi ya 11 inachukua nafasi.
Kama ya nane, tisa na 10 hazikuwa bingwa nchini mwao, basi ya 11, 12 na 13 zinachukua nafasi hizo kama watakuwa mabingwa, ili mradi zile 10.
Sasa unashangaa timu inashika nafasi ya 50, 60 hadi 70, leo unaambiwa haitocheza awali. Labda timu 40 hadi 50 zote za juu zisiwe mabingwa nchini mwao, kitu ambacho hakiwezekani.
Mtu aongea kwenye redio na wachambuzi wako kimya. Mbali na kuchambua mechi husika, wachambuzi pia wanatakiwa kusoma vitu vingi tofauti vya soka, ili kukabiliana na aina hii ya upotoshaji. Siku hizi vitu vyote viko kwenye mtandao,
wala haitumii nguvu kuvipata, nibando lako tu. Fanyeni hivi ili kuusaidia mpira wa Tanzania kuendelea na si kila siku kuendeleza mipasho, na upotoshaji usio na kichwa la miguu, ambao pia unaweza kuvishushia heshima vyombo hivyo, watangazaji na wachambuzi wenyewe.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








