Taratibu wageni wanaanza kuiteka 'dabi' Simba, Yanga

02May 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Taratibu wageni wanaanza kuiteka 'dabi' Simba, Yanga

ILIKUWA ni kawaida miaka kadhaa nyuma kusikia majina ya wachezaji wa Kitanzania yakitajwa mara baada ya mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga kumalizika.

Hata kama wageni walikuwapo, lakini ni Watanzania ndiyo kwa kiasi kikubwa walionekana kucheza kwa kujituma na kupambana kwa sababu wao ndiyo wanaojua homa ya 'dabi' ya Simba na Yanga inavyokuwa huko mitaani tofauti na wageni.

Mara nyingi wageni wanakuwa wanahadithiwa tu namna watu wanavyoichukulia mechi hiyo, na kama watawaona mashabiki wanavyokuwa huko mitaani, lakini si kama wachezaji ambao wamezaliwa na kukulia kwenye maisha hayo.

Ndiyo maana huko nyuma tuliona wachezaji wa Kitanzania walivyokuwa wakipambana kufa au kupona, na kucheza kwa kujitoa mara mbili tofauti na inavyokuwa kwenye mechi za kawaida, kiasi cha kuwashangaza hata wageni.

Tunawakumbuka wachezaji kama kina Sunday Manara, Kitwana Manara, Gibson Sembuli, Juma Mkambi wa Yanga na Abdallah Kibadeni, Adam Sabu, Abdallah Mwinyimkuu, Thuwen Ally wa Simba miaka ya 1970 hadi mwanzoni mwa 1980 walivyoipamba 'dabi'.

Kuanzia miaka ya 1980 walikuja kina Omari Hussein, Rashid Hanzuruni, Makumbi Juma, Sanifu Lazaro kwa upande wa Yanga na kina Zamoyoni Mogella, Edward Chumila, Malota Soma kwa upande wa Simba. Mwanzoni mwa miaka ya 1990, ndipo walipoanza kuja wageni kama kina Damin Kimti, William Fuhnbulleh, Contastine Kimanda na kuwika, lakini bado walikutana na upinzani mkali wa wenye 'dabi' wenyewe kina Sekilojo Chambua, Edgar Fongo, na wengine wengi kwa upande wa Yanga, huku Simba ikiwa na kina Nteze John, John Makelele na wengine wengi.

Hata miaka ya 2000, walipokuja wageni kama kina Emmanuel Okwi, Hamisi Kiiza, Didier Kavumbagu, Haruna Niyonzima na marehemu Patrick Mafisango, ambao ndiyo kwa kiasi kikubwa walioanza kuleta mapinduzi ya wachezaji kutoka nje, kung'ara kwenye dabi, lakini bado pia walikutana na upinzani mkali kutoka kwa kina Jonas Mkude, William Lucian 'Gallas', Haruna Chanongo, Salum Athumani, Kudra Omari, Ibrahim Ajibu, Shiza Kichuya, Mrisho Ngasa na wengine wengi. Hawa ni wachezaji ambao wanaijua 'dabi' toka bado wadogo kule mitaani.

Na wanajua jinsi mashabiki wanavyotaniana, wanavyoteseka, na wanavyoichukulia timu moja inaposhinda au kufungwa, ndiyo maana na wao wanachukua hisia wanazozipata mitaani wanazipeka uwanjani. Kwa sasa naona jambo hili linaanza kupungua kwa kiasi kikubwa.

Wachezaji wa kigeni sasa ndiyo kama vile wanaonekana kuanza kujua thamani ya 'dabi' kuliko wenyeji wenyewe.

Jumamosi iliyopita tuliona wachezaji wachache tu walioonekana kucheza kama 'dabi', huku wengine hasa Watanzania wakicheza kama mechi nyingine tu ya Ligi Kuu. Wachezaji kama Fiston Mayele na Henoc Inonga ambao ni Wakongomani, wameonekana kuitawala 'dabi' hiyo na kufanya vitu ambavyo vilikuwa vikiwafurahisha mashabiki waliokuwapo uwanjani na waliokuwa wakiangalia televisheni.

Walicheza hasa 'kidabidabi', Mayele akitafuta nafasi kwa kila hali ili afunge bao, lakini Inonga akitibua kila jaribio lake la kutaka kufunga na hii ndiyo iliyokuwa burudani kubwa waliyoipata mashabiki, kwani mechi yenyewe haikuwa na mashambulizi ambayo yangeweza kuwafanya wasimame vitini na kushangilia.

Mchezaji pekee wa Kibongo aliyeonekana kuitendea haki 'dabi' ni Kibwana Shomari, kwani uchezaji wake uliakisi aina ya mechi yenyewe alivyokuwa akicheza kwa kujituma na kwa kiwango cha hali ya juu.

Tunajua kuwa ni kweli kwa sasa timu za Simba na Yanga zina wachezaji wengi wa kigeni, huku ikiruhusiwa kila timu kusajili nyota 12 kutoka nje ya nchi, lakini inaonekana ni kama vile wachezaji wa Kitanzania wamekuwa ama hawajitumi kwenye 'dabi' hiyo au kwa miaka ya karibuni wamezidiwa sana viwango na wachezaji wa kigeni.

Hii ni kengele ya hatari kuwa huko tuendako, dabi zote zikiisha watakuwa wakizungumzwa wachezaji wa kigeni jinsi walivyong'ara. Na hii si dhambi, kama wao ndiyo wanaona umuhimu wa mchezo huo tofauti na Watanzania kwa nini wasisifiwe? Kinachotakiwa sasa ni wachezaji wa Kitanzania kuanza kujitazama upya kupitia mchezo huu.

Wachezaji wengi wa zamani hupata jina, sifa na kujulikana nchini kupitia michezo kama hii, hivyo hujituma sana linapokuja suala la mechi ya Simba na Yanga. Mchezaji wa Kitanzania anayecheza mechi ya Simba na Yanga kama anacheza mechi nyingine tu ya Ligi Kuu, basi ataendelea kuwa vile vile tu.