Serikali za Afrika Mashariki zimekuwa zikilaumu uagizaji wa nguo na viatu vilivyotumika kama moja ya sababu zinazofanya viwanda vya nguo na ngozi kufa na hivyo kuwanyima wenyeji nafasi za ajira.
Nguo, viatu na bidhaa nyingine za mitumba hutegemewa sana na watu wa kipato cha chini kutokana na bei yake nafuu lakini biashara hiyo pia inachangia pato la nchi na kutoa ajira kwa maelfu ya watu ambao hufanya biashara ya kuuza mitumba ya nguo, viatu na vitu vingine ambavyo huagizwa kutoka Ulaya na Marekani.
Hatua hiyo ya kupiga marufuku mitumba iliyochukuliwa na viongozi hao imepokelewa kwa mtazamo tofauti miongoni mwa wananchi, hata hivyo, baadhi wakipongeza uamuzi huo na wengine wakipinga.
Binafsi naunga mkono uamuzi huo ambao kimsingi unalenga kuimarisha viwanda vya ndani na hivyo kuongeza ajira kwa vijana, ambao wengi wao wamekuwa watu wa kuishi kwa 'kubangaiza' tu.
Jambo la kuzingatia ni kwamba ili kufikia maendeleo ni lazima kuwe na upande ambao utaathirika, kwa maana hiyo ili Tanzania ya Magufuli kwa mfano iwe ya viwanda, baadhi ya watu wataathirika na mipango hiyo ya maendeleo.
Kwa kutaka kufufua viwanda vya nguo ni lazima wamachinga waathirike na ndio maana wameanza kulalamika.
Hata serikali inapoamua kupanua barabara kwa ajili ya maendeleo, baadhi ya watu hubomolewa nyumba ili kupisha upanuzi huo, hivyo kwa hili la kupiga marufuku mitumba kwa lengo la kufufua viwanda lazima baadhi ya watu wataumia.
Na tayari hapa kwetu wafanyabiashara na hasa wa mitumba wanadai kuwa hatua hiyo itaathiri biashara zao na kurudisha nyuma juhudi za kujiajiri katika sekta binafsi.
Hilo ni kweli, lakini kama nilivyosema, hiyo ni moja ya athari za maendeleo.
Bahati nzuri ni kwamba nguo za ndani: shimizi, sidiria, soksi na nyingine za aina hiyo za mitumba zilishapigwa marufuku zaidi ya miaka mitatu iliyopita kutokana na kile kinachoelezwa kuwa zina madhara kiafya.
Baadhi ya wafanyabiashara wameendelea kuziingiza nchini na kuziuza kama kawaida kana kwamba hakuna marufuku yoyote na kusababisha kufukuzana huku na kule na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Shirika hilo ambalo liko chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ndilo lenye jukumu la kudhibiti uingizwaji wa nguo za mitumba na hasa za ndani, lakini sasa serikali imeamua kupiga marufuku nguo zote za mitumba.
Hatua ya viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kukubaliana kupiga marufuku nguo za mitumba kwa ujumla na vitu vingine vilivyotumika zinaweza kuirahisishia TBS kazi ya kupambana na uingizwaji wa vitu hivyo.
Ninasema hivyo kwa sababu kasi ya kukabiliana na uingizwaji wa nguo hizo nchini itaongezeka ili kuhakikisha kwamba viwanda vinafufuliwa na vinafanya kazi kwa ufanisi na kupata soko la uhakika.
TBS imekuwa ikitekeleza matakwa ya agizo la sheria ya mwaka 2009 inayozuia matumizi ya nguo za ndani zilizokwishatumika, lakini linakumbana na changamoto ya kuendelea kuwapo kwa nguo hizo.
Hatua ya viongozi wa jumuiya hiyo kutangaza marufuku ya uingizwaji wa mitumba katika nchi zao, ina maana kwamba kila nchi itafanya juu chini ili kuhakikisha kwamba kile walichokiamua kinatekelezwa kikamilifu.



.jpg?itok=nfwjwDzv)






