Uwanja wa Taifa unapokosa kibendera

07Mar 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Uwanja wa Taifa unapokosa kibendera

KWA mara ya tano msimu huu, mechi baina ya Azam FC na Yanga imeshindwa kutoa mbabe ndani ya dakika 90 baada ya juzi timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hizo ziliuanza msimu wa soka wa 2015/16 kwa kutoka sare katika mechi ya robo-fainali ya Kombe la Kagame, kisha zikashindwa kufungana kwenye Ngao ya Jamii kabla ya kutunguana bao 1-1 katika mechi ya duru la kwanza Ligi Kuu ile ya hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar Januari 5.

Mechi ya juzi ilikuwa na matukio kadhaa yakiwamo ya mashabiki kung'oa viti na kutwanga makonde kipindi cha kwanza, lakini kuvunjika kwa mti wa kibendera cha kona ya kaskazini mashariki mwa Uwanja wa Taifa ndiko kulichefua zaidi.

Katika dakika ya nne ya mechi hiyo ya raundi ya 21, Mchezaji Bora wa ligi hiyo msimu uliopita, Simon Msuva aliuvunja mti huo wakati akijaribu kusaka mahali pa kujishikiza baada ya kukumbana na daruga la beki 'aliyeshiba', David Mwantika wa Azam.

Na katika kuhakikisha Sheria Namba Moja ya Soka (Uwanja) inazingatiwa, marefa wa mechi hiyo walisimamisha mchezo ili kiwekwe kibendera kingine, lakini hakikupatikana na kuifanya mechi hiyo isimamishwe kwa dakika tano kabla ya mti uliovunjika haujaungwa kwa plasta.

Uwanja wa Taifa unaoongoza kwa kuwa mkubwa zaidi nchini na pia kwa kuingiza 'mpunga' mwingi zaidi kila msimu huu tangu ulipoanza kutumika mwaka 2007. Mapato makubwa zaidi kwenye uwanja huo ni Sh. bilioni 1.8 zilizopatikana katika mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na Brazil iliyochezwa 2010.

Swali la kujiuza ni vipi uwanja huo wenye uwezo uwezo wa kuketisha watazamaji 57,558 ukose kibendera cha kuonyesha alama muhimu kama kona?

Ikumbukwe kuwa Uwanja wa Taifa uliojengwa kwa Sh. bilioni 56 kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Serikali ya Watu wa China, ni hazina kwa taifa. Ulikuwa unaongozwa kwa ukubwa barani Afrika kabla ya kujengwa kwa Uwanja wa Soccer City nchini Afrika Kusini mwaka 2010.

Mechi kati ya Azam na Yanga ilikuwa kubwa zaidi kwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizochezwa juzi na bila shaka ilitazamwa na watu wengi zaidi kwa sababu ilikuwa inaonyeshwa moja kwa moja kwenye runinga. Kusimama kwa dakika tano kwa mechi hiyo eti kutokana na kukosekana kwa kibendera cha akiba, ni fedheha kwa Serikali ya Tanzania ambayo ndiyo inaumiliki uwanja huo.

Mapato yanayopatikana kwenye Uwanja wa Taifa kila msimu kupitia viingilio vya milangoni ni zaidi ya shilingi bilioni moja na Serikali inachukua asilimia 15 ya mapato hayo. Kwa nini kusiwe na vifaa vya zaida kwenye uwanja huo, mfano, nyavu, magoli na vibendera kama cha juzi kilichovunjika?

Binafsi ninafikiri kuna haja wizara yenye dhamana ya michezo, inayousimamia uwanja huo, 'kuwatumbua' watendaji wa Uwanja wa Taifa kutokana na 'fedheha' ya juzi ya kukosekana kwa kibendera cha akiba.

Uwanja huo umekuwa na kashfa nyingi zikiwamo za watendaji wa wizara yenye dhamana ya michezo kubeba na kusafirisha kwenye 'viroba' fedha za mgawo wa mapato ya milangoni, huku mfumo wa tiketi za kiektroniki ukisitishwa 'kibabe' kutumika kwenye uwanja huo na kurejesha mfumo wa kizamani wa tiketi za vishina.