Utashangiliaje Stars umevaa jezi ya klabu?

26Mar 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Utashangiliaje Stars umevaa jezi ya klabu?

NAANZA kwa kuipongeza timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars kwa ushindi wa mabao 3-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Afrika ya Kati.

Ilikuwa ni mechi ya kirafiki iliyo kwenye kalenda ya FIFA. Yalikuwa ni mabao ya Dismas Novatus, nahodha Mbwana Samata na Geogre Mpole ambayo yaliifanya Stars kutoka kifua mbele.

Kuna wanaobeza kwa kusema kuwa Stars huwa inashinda kwenye mechi za kirafiki, lakini kwenye mechi halisi za mashindano, inachemka.

Inawezekana ikawa kweli, lakini ukweli mwingine unabaki pale pale kuwa mechi kama hizi zinaisaidia Tanzania kupanda kwenye viwango vya FIFA kama timu inapata ushindi.

Labda baadhi ya mashabiki hawajui faida ya kupanda kwenye viwango vya FIFA. Ni kwamba ukiwa juu kidogo, unapata faida hata kwenye upangaji wa ratiba ya mechi za kufuzu CHAN, AFCON na hata Kombe la Dunia.

Nchi inapokuwa ipo chini, tabu inayoipata kwanza ni kuanza kwenye hatua za awali, huku zile za juu zikisubiri raundi ya kwanza.

Kuna nchi ni aghalabu sana kuona zikicheza mechi ya mtoano. Pili ni kwamba ukiwa chini sana unapangwa na timu kongwe, ngumu na zoefu kwenye michuano mbalimbali ya Afrika, hivyo inakuwa ngumu 'kutoboa'.

Angalau usogeesogee unaweza kupata kigogo mmoja, lakini kama kwenye viwango vya FIFA uko chini, unaweza kujikuta umewekwa na vigogo wawili na hapo ndipo inapokuwa mtihani.

Utamaduni na soka kote duniani ni kwamba timu zenye viwango vya juu, zinakuwa kwenye kapu moja, hivyo ni nadra sana kukuta zikiwa kwenye kundi moja.

Lakini zile za chini ndizo zinapata tabu sana kwa sababu zinatafutiwa vigogo vya kuwekwa nao kundi moja, hivyo kusaka ushindi kwenye mechi kama hizi ili kupanda viwango japo taratibu taratibu ni jambo la msingi sana na linaweza kuwa na faida kubwa hapo baadaye.

Kwenye mechi dhidi ya Afrika ya Kati nimeona tabia ambazo zimeanza kuota mizizi kwa baadhi ya mashabiki kuvaa jezi za klabu zao badala ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Hii haipendezi na si uzalendo kabisa, kwani timu ya taifa ndiyo inaanza na klabu zinakuja baadaye.

Nimeshuhudia baadhi ya mashabiki wa Simba wamevaa jezi za klabu yao, halafu eti wanaishangilia timu ya taifa. Huo ni utovu wa nidhamu. Wale wa Yanga nao wamevaa jezi za klabu yao, lakini wanaishangilia Stars. Si uzalendo hata kidogo.

Sasa kuna wengine walionekana kuvaa jezi za Liverpool, Manchester United, Chelsea, lakini wapo Uwanja wa Benjamin Mkapa wakiishangilia Stars. Hii haikubaliki.

Sitaki kusema kuwa eti walinzi wa mlangoni wawazuie mashabiki waliovaa jezi za timu zingine wasiingie uwanjani, lakini nataka kuwashauri mashabiki waanze utamaduni wa kuvaa jezi ya timu ya taifa, kama Stars inacheza.

Kuishangilia Stars huku umevaa jezi za timu nyingine ni sawa tu na unafiki. Hii ni timu ya Watanzania, inabidi watu wawe na Utaifa, mengine baadaye. Ikicheza Simba, Yanga wanavaa jezi ya klabu, lakini kwa nini ikicheza Stars wanashindwa kuvaa jezi ya timu ya taifa.

Nchi nyingine huwezi kuona hilo, kwa sababu watu wanajivunia mno nchi yao. Niliangalia mashabiki wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakati ikijiandaa kucheza na Morocco jana jinsi walivyovaa, na ushangiliaji wao, ni hatari tupu na huwezi kujua nani ni shabiki wa timu gani.

Hivi kama shabiki unaweza kununua jezi ya klabu yako, unashindwa kununua ya Taifa Stars? Kama huwezi kweli una uzalendo? Timu hii pia ina wadhamini wake, na jezi zake zinauzwa na mashabiki wanatakiwa wanunue ili kuichangia timu, lakini pia kuitangaza kampuni ambayo inaidhamini, badala yake mashabiki waendelea kuzitangaza zile ambazo hazihusiki na timu hiyo ya taifa.

Nadhani imefika wakati Watanzania kuipenda Stars kama wanavyozipenda timu zao za hapa nchini na nje ya nchi na si kuipenda kinafiki, ili watu wasiwafikirie vibaya.

Halafu si lazima, mtu hataki kununua jezi, au haoni umuhimu huo, basi aje tu uwanjani akiwa amevaa kiraia tu, wala haikatazwi.Tununue jezi za Stars na kuzivaa inapocheza. Sivyo nenda na nguo za kawaida tu.

Lakini kuvaa jezi za klabu nyingine kwenye mechi ambayo inacheza Taifa Stars, kunashangaza, kusikitisha na kufikirisha kwa wakati mmoja.