Hili la daladala Mwanza kukatiza ‘ruti’ linakera kuliko maelezo

25Mar 2022
Anthony Gervas
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hili la daladala Mwanza kukatiza ‘ruti’ linakera kuliko maelezo

BAADHI ya madereva, kondakta wa daladala za mabasi madogo jijini Mwanza, mnaofanya safari njia ndefu kwanini mmegeuka kero kubwa kwa abiria, mnakatisha ‘ruti’ za safari kabla ya gari kuwafikisha kwenye kituo husika.

Nauliza hivi hamuoni kwamba mnawasababishia wateja wenu usumbufu na kero ya kulipa nauli mara mbili kinyume cha sheria, kwanini mnageuzia magari njiani na kuwashusha abiria kibabe, huku mkiwatolea lugha chafu na vitisho, kuwadhalilisha wakati leseni zenu zinawataka mfanye safari hadi kituo cha mwisho.

Tabia hii mmeitoa wapi? Iwe asubuhi, mchana na jioni sasa ndiyo usiseme, mnatoa hadi vitisho vya kutaka kuwapiga abiria bila kujali utu wanapodai haki zao za kufikishwa kwenye vituo husika, nafikiri kuna haja ya kunyang’anya leseni hizo sababu mnaonekana mmechoka kutoa huduma hiyo.

Katika jiji hili magari ya njia ndefu ni pamoja na yanayofanya safari zake kutoka uwanja wa ndege kwenda Kisesa, Nyashishi hadi Kishiri, kutoka Kisesa kwenda Nyashishi - Usagara, pia Nyashishi kwenda Uwanja wa Ndege. Hawa ndiyo vinara wa kukatisha safari za abiria.

Mimi nasema hakuna mteja aliyekwenda kwa wahusika Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuwaombea leseni ya kusafirishia, mlikwenda wenyewe mkapewa mkaridhika kwenda safari za njia ndefu, halafu tena mnaanza kutusumbua kwa visingizio mara eti gari ni bovu haliwezi kufika kituo cha mwisho wakati liko barabarani.

Kama unajua gari lako bovu, kwanini umelileta barabarani kutoa huduma hiyo, badala ya kulipeleka gereji kutengenezwa, unataka kutupotezea maisha yetu bila ya sababu za lazima, wala hamwogopi mkono wa sheria za usalama barabarani nani kawaroga?

Kazi yangu wiki hii mimi binafsi ni kukemea upuuzi huo unaofanyika katika jiji letu la Mwanza, utasikia kondakta na dereva wake wakitangaza eti “gari haliendi hadi huko tunaishia Igoma hatufiki Kisesa’ mara tena ‘tunaishia Pasiansi au Buhongwa hatufiki Nyashishi’.

Wanatoa tangazo hilo bila kuogopa sheria, wateja wakiuliza wanaambiwa gari hilo ni bovu, linatakiwa kupelekwa gereji au kwa fundi wakati limepakia abiria na linaendelea kupakia wale wanaoishia lilipotangaza kugeuzia.

Lakini, ukiandika namba zake na kulifuatilia kama kweli limepelekwa kutengenezwa, utaona linapita tena barabarani likiwa limepakia abiria hadi wamesimama mpaka mlangoni mwa kondakta likirudi lilikotoka. Lini tabia hiyo itakomeshwa na mamlaka husika sababu ni kero kwetu wateja.

Ndiyo maana nauliza tabia hii ya uongo na uvunjifu wa sheria za usalama barabarani kwa hawa wenye magari wanazitoa wapi? Kwenye majiji makubwa kama letu, hawajifunzi kutoka katika majiji mengine kama vile Dar es Salaam. Dereva na kondakta hawawezi kufanya ulaghai kizembe kwa abiria bila ya sababu za msingi.

Naomba abiria tuwe na ushirikiano wa pamoja, kuhakikisha hatunyanyaswi na madereva au makondakta tunapopanda magari hayo, sababu tunalipa nauli halali ili tupate huduma ya usafiri ambayo ni haki yetu. Tukatae kushushwa njiani kabla hatujafika vituo vyetu tunavyokwenda.

Pia kama haitoshi wahusika watoe namba za simu kwenye kila gari la daladala hizo, ili abiria iwe rahisi kutoa taarifa kituo cha polisi au kwa askari wa usalama barabarani, aweze kupata msaada zaidi au LATRA.

Wananchi wanatupia lawama zao kwa baadhi ya askari wa usalama barabarani kuwa hawasimamii vema sheria, sababu na wao ni sehemu ya umiliki wa magari ya daladala, namdokeza mkuu wa kitengo cha usalama barabarani mkoani hapa afuatilie na kutatua kero.

Kwa leo dozi yangu imetosha tukutane tena siku nyingine bila kumung’unya maneno, zama hizi za ukweli na uwazi, kurunzi langu linaishia hapo kuwamulika wahusika kila mmoja kwa nafasi yake.