Urafiki na wapinzani usigeuzwe usaliti CCM

27Mar 2016
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Urafiki na wapinzani usigeuzwe usaliti CCM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa kinaendelea na mkakati wake wa kuwasimamisha, kuwavua uongozi na hata kuwatimua uanachama makada wake ambao watabainika kuwa walikisaliti katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa kinaendelea na mkakati wake wa kuwasimamisha, kuwavua uongozi na hata kuwatimua uanachama makada wake ambao watabainika kuwa walikisaliti katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Hatua hii inazua maswali mengi kwamba hivi chama tawala ili kiwe bora, inabidi kiwe na uhusiano mbaya na vyama vya upinzani ama wanachama wake wawe na chuki na vyama vya upinzani?

Je, ili chama cha upinzani kiwe bora, kinatakiwa kuwa na uhusiano mbaya na chama tawala, au wanachama wake wanatakiwa kuwa na uadui na wale wa chama tawala?
Je, siasa za aina hii zina maslahi kwa umma?

Binafsi sidhani kwamba siasa za aina hii zina maslahi kwa umma, kwani ni miongoni mwa mambo yasiyostahili kushabikiwa na watu wanaojitambua na wanaojua umuhimu wa kujenga nchi hii kwa ushirikiano.

Mkakati huu wa kushughulikia kinachoitwa usaliti, tayari umesababisha wanachama 21 waliokuwa viongozi ndani ya CCM Mkoa wa Morogoro kuvuliwa uongozi.

Katika mkakati huo, makada 29 wamefukuzwa kwenye chama kutokana na sababu hizo hizo za usaliti wakati wa Uchaguzi Mkuu, hatua ambayo binafsi nadhani chama hicho kinatakiwa kuiangalia kwa jicho la ziada.

Ndani ya mazingira haya kumekuwapo na tabia ya baadhi ya wanachama wa vyama vya siasa ya kutopenda kushirikiana kwa vile tu huyu anatoka chama kile na mwingine hiki!

Mara unaweza kusikia mbona fulani ni wa chama hiki lakini ni rafiki wa fulani wa chama kile? Ama mbona inaonekana kuna watu wengi wa chama fulani wanakipenda chama kingine?

Wamekuwa wakiuliza hayo bila kutambua kwamba siasa siyo uadui na inawezekana kwa mkakati huu wa CCM wa kuwatimua wasaliti unaweza kuwakumbuka hata wale ambao hawana makosa, ila kwa sababu tu walionekana wakizungumza na wenzao wa upinzani!

Niwakumbushe tu kwamba, chama kinachoonekana kufanikiwa ni kile ambacho kinaweza kushawishi kuungwa mkono kutoka kwa watu wasio na vyama na vile vile kikaweza kushawishi na kupata uungwaji mkono kutoka kwa wanachama wa vyama vingine.

Kwa maana hiyo chama hiki kikongwe kinapoendelea kuwashughulikia wanachama wake 'wasaliti' ni vyema kikatambua kwamba, wakati mwingine urafiki miongoni mwa wanachama wa vyama vya siasa ni jambo la kawaida, hivyo usigeuzwe kuwa usaliti.

Katika siasa ni jambo la kawaida wanachama wa vyama tofauti kuwa marafiki, ndiyo maana hivi karibuni mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Leo Lwekamwa alikaririwa na gazeti hili akikosoa timuatimua inayoendelea sasa.

Lwekamwa alisema, mwanachama siyo mfungwa au mateka ama mfugo wa aina fulani, na hata kwa kutambua kuwa chama cha siasa hakina ukoo, hivyo siyo mama, baba au mjomba na kwamba mwanachama yuko huru kuhama au kukiacha chama akipenda.

Siyo siri kwamba CCM ilikuwa imeyumba sana na hata viongozi wake wakuu walikuwa wakikiri hilo, kwa hiyo ilikuwa ni rahisi kwa wanachama kukata tamaa na kutafuta mgombea kutoka chama kingine ambaye waliamini anaweza kuwavusha.

Hivyo CCM iangalie ilikojikwaa badala ya ilipoangukia kwani kufanya hivyo siyo kukisaidia chama bali kuendeleza mpasuko kwa vile wanaweza kuingizwa wasiokuwamo.