Banda amesajiliwa Simba kukaa benchi?

26Mar 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Banda amesajiliwa Simba kukaa benchi?

DAKIKA ya saba tu ya mchezo, Kocha Mkuu wa Simba Jackson Mayanja alimnyanyua Abdi Banda apashe ili kuchukua nafasi ya mchezaji mwingine.

Ilikuwa kwenye mechi ya Ligi Kuu kati ya timu hiyo dhidi ya Coastal Union na Simba kushinda mabao 2-0.

Aliyetakiwa kutoka ni Mohamed Hussein 'Tshabalala', ambaye anadaiwa kupiga krosi mbili 'mkaa' ambazo kama zingepigwa vizuri, Simba ingeweza kuandika japo goli moja mapema.

Banda kwa kauli yake mwenyewe alikiri kumjibu kocha kuwa ni mapema kumtoa 'Tshabalala', badala yake amuacha endelee kucheza kwani atajirekebisha.

Majibu hayo yalimkasirisha kocha Mayanja na kumtaka kuondoke na kwenda kukaa juu, yaani jukwaani.
Banda hakufanya hivyo, badala yake alikaa hapo hadi mechi ilipomalizika.

Kwa sasa yuko hatarini kupewa adhabu na klabu yake kutokana utovu wa nidhamu.

Sitaki kuelezea madai kuwa mchezaji huyo aliandika maneno yaliyoonekana kumpinga kocha wake kwenye mtandao mmoja wa kijamii.

Mimi najikita kwenye tukio lenyewe.

Yeyote anayejua soka kiundani na utaratibu wote wa mpira wa miguu, hili alilofanya Banda ni utovu ni nidhamu.
Wapo wanaomtetea kuwa alikuwa sahihi kuwa hakuona busara mchezaji mwenzake kutolewa dakika ya saba tu ya mchezo, hivyo kumshauri kocha aendelee kumchezesha.

Cha kujiuliza hapa ni kwamba, hivi kweli Banda alikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kama kocha wake alikuwa anataka kumuingiza au alitaka anyanyuke, apashe ili kumpa ujumbe 'Tshabalala' kuwa anachokifanya uwanjani sicho, hivyo kuna mtu punde atakuja kuchukua nafasi yake ili ajirekebishe?

Kwanini hakutekeleza amri kwanza ili aangalie kama ataingizwa au la?

Ni wachezaji wangapi huwa tunawaona wanafanya mazoezi kwa ajili ya kuingia, lakini hawaingii uwanjani kucheza?
Lakini hata kama angeingizwa, kuna tatizo gani kama kocha aliona aliyekuwepo uwanjani hafuati maelekezo?
Hivi Banda ameridhika kukaa benchi kiasi cha kukataa kuingia uwanjani?

Amesajiliwa kukaa benchi? Mkataba wake ni kukaa benchi au kucheza soka?
Kama ni kucheza soka kwa nini anakataa?

Kwa mawazo yangu, mchezaji anayekataa kucheza atakuwa ni wa ajabu sana.

Mchezaji anayeridhika kukaa nje ili kupisha mwenzake acheze ana wema wa ajabu sana.
Lakini mawazo yangu yananielekeza mbali zaidi. Najiuliza, hivi Banda alikataa kwa sababu ya kumuacha mwenzake aendelee kwa nia njema, au alikuwa anasusa baada ya kutopangwa kwenye mechi kadhaa tangu aonyeshwe kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya Yanga?

Sina uhakika sana, lakini nadhani kati hayo mawili moja litakuwa sahihi.

Pamoja na hayo yote, alichofanya ni kosa kwa kuonyesha nidhamu mbovu dhidi ya kocha hadharani.
Kwa hili klabu ya Simba wala haitolaumiwa kutoa adhabu ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine ambao wanaweza kuiga alichofanya mchezaji huyo kama jambo hili litaachiwa.

Kote duniani, tunaona makocha wakiwatoa wachezaji ambao wanaona wanashindwa kutekeleza majukumu waliyopewa na wala haijalishi mpira umechezwa muda gani, au mchezaji amecheza dakika ngapi.

Msimu kwa 2013/14 hapa nchini tuliona kocha mwenye msimamo mkali ya Simba wakati huo Zdravko Logarusic akimtoa mshambuliaji Betram Mombeki aliyeingia kuchukua nafasi ya mtu, lakini baada ya kushindwa kufanya kile alichoambiwa atekeleze alitolewa kwa muda usiozidi hata dakika 10 tangu aingie dimbani kwenye mechi moja ya Ligi Kuu.

Mimi nadhani Banda kama kweli Mayanja alikuwa na lengo la kumuingiza, ingekuwa ni fursa yake nzuri ya kuwaonyesha wanachama na mashabiki wa Simba kuwa kilichotokea kwenye mechi dhidi ya Yanga ilikuwa ni bahati mbaya na kuanza ukurasa mpya.

Baada ya kufanya makosa kwenye mechi dhidi ya Yanga, hakucheza mechi zilizofuata, lakini hakumkatalia kocha wake pale aliponyanyuliwa kutokea benchi na kushangiliwa na mashabiki Uwanja wa Taifa.

Ikumbukwe kuwa beki, Novatus Lufunga alikuwa akikaa benchi, lakini baada ya Hassan Isihaka kuonyesha utovu wa nidhamu, alipewa nafasi na mpaka sasa anaitumia vema kiasi cha kuwakosha wanachama na mashabiki wa Simba.

Tangu aliposajiliwa kutokea Coastal Union, bado alikuwa si mchezaji wa kikosi cha kwanza cha kutegemewa na Simba.
Nafikiri kocha Mayanja alikuwa bado hamuamini Lufunga. Kama ingekuwa sasa, nadhani beki huyo ndiye angecheza kati na Juuko Murshid na si Banda.

Inashangaza kuona akikaidi alipoambiwa aingie ili na yeye afanye vitu vya uhakika vitakavyomfanya kocha kuanza kukuna kichwa jinsi ya kupanga mabeki wake ambao wote wako vizuri.

Ndiyo maana hadi sasa bado najiuliza, hivi Banda alisajiliwa kwa ajili ya kukaa benchi?