Tuchangamkie uwekezaji Hati fungani za benki

06May 2016
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mtazamo kibiashara
Tuchangamkie uwekezaji Hati fungani za benki

WIKI iliyopita katika safu hii , tuliangazia kuhusu umuhimu wa mfanyabiashara kujali muda kwenye biashara yake.

Kwamba kabla ya wewe mfanyabiashara kutoa lawama kuwa unawekeza juhudi zaidi katika biashara yako, lakini huoni mafanikio, ni vyema ukajiuliza ni muda kiasi gani unaoutumia kuwekeza juhudi hizo.

Tukasema kwamba, juhudi zako zitazalisha ufanisi mzuri pale utakapofanya yaliyo muhimu kwa biashara, na kuacha yasiyo na umuhimu mkubwa ambayo kimsingi yatakuwa yanakupotezea muda.

Leo nimeona nijikite tena kwenye eneo moja la uwekezaji ambalo kimsingi si jipya masikioni mwa wasomaji wa safu hii, kwa sababu tulishaliona na tukatumia muda mrefu sana kulizungumzia.

Eneo hili ni la uwekezaji kwenye hati fungani, ambalo sasa linazidi kuchukua nafasi yake kwenye shughuli za kiuchumi hapa nchini.

Hata hivyo, uwekezaji kwenye hati fungani nitakaouzungumzia leo kwa kiwango fulani, ni tofauti na ule wa hati fungani ama dhamana za serikali ambazo tuliziona katika safu hii, mfulizo kwa karibu miezi miwili mizima.
Uwekezaji ninaouzungumzia leo ni wa hati fungani za benki ya NMB.

Katika kukumbushana, hati fungani ni aina ya uwekezaji ambao mwekeaji anawekeza katika taasisi hasa serikali au shirika la kibiashara kama ilivyo kwa benki ya NMB sasa.

Mwekezaji anaweza kuwa mfanyabiashara ama raia mwingine mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea, anaikopesha fedha benki kwa muda maalumu na kwa riba inayoweza kubadilika au riba isiyobadilika.

Mwanzoni mwa wiki hii, Benki ya NMB ilitangaza kuuza hati fungani zake kwa wananchi wa kada zote, ikilenga kupata kiasi cha shilingi bilioni 20 hadi 25, fedha itakazozitumia kutoa mikopo mbalimbali kwa wananchi.

Kwa Mujibu wa Meneja Uhusiano wa wawekezaji Anna Mwasha, mauzo hayo ya hisa yataanza Mei 10, 2016 na kufungwa Juni 8, mwaka huu katika matawi yote 176 ya NMB nchini.

Lakini pia mauzo hayo yatafanyika kupitia kwa mawakala waliosajiriwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Kila mtu anaruhusiwa kununua hati fungani hizi za NMB, na kwa faida ya safu hii mfanyabiashara yeyote ili mradi awe na kiwango cha fedha cha kuanzia shilingi 500,000 na kuendelea.

Sasa kwa maana hiyo, mfanyabiashara ama mwananchi anaponunua hati fungani za NMB, anakuwa ameikopesha benki hiyo fedha zake.

Tofauti na ilivyo kwenye hati fungani za serikali, ambazo zipo za muda mfupi na za muda mrefu, hati fungani za NMB zitakuwa za kipindi cha miaka mitatu.

Katika kipindi hicho cha miaka mitatu ya kuiva, mwekezaji atakuwa akilipwa riba ya asilimia 13 kila mwaka.
Aidha riba hiyo, itakuwa ikilipwa mara mbili kwa mwaka, yaani kila baada ya miezi sita.

Yaani kwa mfano mtu akinunua hati fungani za shilingi milioni moja, riba ya asilimia 13 ya kiasi hicho cha fedha ni shilingi 130,000.

Na kwa kuwa inalipwa mara mbili kwa mwaka, ina maana kila baada ya miezi sita mwekezaji atakuwa akilipwa shilingi 65,000 kwa kipindi chote cha miaka mitatu ya fedha yake kuwa benki.