Huduma muhimu za kijamii UBT sasa ni kizungumkuti

06May 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Huduma muhimu za kijamii UBT sasa ni kizungumkuti

KITUO cha Mabasi yaendayo Mikoani na Nchi jirani Ubungo(UBT), kinategemewa na wakazi wa jiji la Dar es Salaam pamoja na watokao na kwenda mikoa mbalimbali na nchi jirani.

Kutokana na ukuaji wa kasi kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi, kielimu katika jiji la Dar es Salaam, usafiri wa mabasi unatumiwa zaidi na watu wa kada tofauti wakiwamo wafanyabiashara, wanafunzi, wazee, wagonjwa ambao hufuata huduma tofauti jijini kama vile tiba na shughuli nyinginezo.

Ufikapo kituo cha mabasi Ubungo, hali ni tofauti na kile ambacho kinaeleza kuwa kituo hicho ni kikubwa kuliko vyote nchini.Hii ni kutokana naukweli kuwa hutumiwa kusafirisha abiria wengi kwa siku.

Tofauti na ilivyokuwa hapo awali, wakati zikipatikana walau huduma muhimu kama vile choo, eneo la kupumzikia abiria na kufanyika kwa usafi kila siku.

Huduma hizo zilikuwa muhimu kwa abiria na watu wote wanaofika kituoni hapo , ili wapate huduma ya usafiri na nyinginezo.

Kwa sasa hakuna utaratibu mzuri wa kujivunia. Mambo ya kituoni hapo ni kwamba hali hiyo inasababisha kukithiri kwa uchafu. Baadhi ya watu hujisaidia hovyo hata kuhatarisha afya za wasafiri, wapita njia na waishio kuzunguka eneo hilo wakiwemo wanaofanya biashara hususan mama lishe.

Katika kituo hicho, mabasi ya abiria zaidi ya 400 huingia na kutoka kila siku.Abiria na wasindikizaji hutozwa ushuru wa Sh 200. Watu wanaokadiriwa kuingia na kutoka kituoni hapo ni 10,000 kwa siku.

Hata hivyo kituo hicho, pamoja na kuendeleza usafiri wa kila siku hakuna kinachoonyesha kuwa kituo hicho ni rasmi kwa ajili ya kazi hiyo.Yaani kipokipo tu.

Kwa sasa hali iliyopo katika kituo hiki ni ya kukatisha tamaa.Licha ya kila abiria anayesafari au kuja kumpokea mgeni wake kuhitajika kulipia ushuru, bado hakuna majibu ya wazi kwamba fedha hizo zinakwenda katika miradi au shughuli gani za kuboresha kituo hicho ili kuwa rafiki kwa watumiaji?.

Kwa kawaida fedha ambazo hutozwa katika eneo fulani la biashara au la huduma yeyote ya kijamii, lengo tarajiwa ni kutoa huduma bora na kuziimarisha zilizopo katika eneo husika ikiwamo miundombinu yake.

Huduma hizo ni pamoja na kuhakikisha kuna kuwa na maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya kupumzika na kuwasitiri iwapo kuna jua kali ama mvua ikinyesha, eneo la kutupia taka pamoja na upatikanaji wa maji safi ya bomba.

Maeneo ya kupumzikia yanaweza kuwa na vyombo vya habari vya kieletroniki vya kutoa taarifa rasmi za usafiri na wasafiri zinazotangazwa kila mara na redio ama televisheni.

Pia eneo hilo la kupumzikia hutumika na mamlaka husika kwa ajili ya kutoa matangazo madogo madogo ya ndani ya kituo hicho kwa mfano, iwapo mtoto au mtu mzima amepotea kutokana na ugeni ama tatizo la kiakili.

Kile kinachoitwa kuwa ni ushuru au tozo la kila mtu, abiria anayeingia kituoni hapo, hakiendani na mandhari iliyopo. Hili litazamwe upya.

Iwapo mamlaka husika zinaona kituo kinafaa kuendelea kutoa huduma hiyo, ni vyema ikazirudisha huduma za awali ili kuwafanya wasafiri kuwa katika mahali salama pa kusubiria abiria na kupokea wasafiri.

Hali ya kituo hicho haiwakeri abiria tu bali hata madereva wanaoanzia shughuli zao kujitafutia riziki kila siku.

Kituo hicho, kinapaswa kuendana na hadhi ya jiji la Dar es Salaam, kwa kuwa na huduma muhimu za lazima katika kituo chochote cha usafiri wa umma.Hatua zichukuliwe kuhakikisha mazingira na huduma zinaboreshwa.