Tangu ripoti hiyo itoke, nashukuru kwamba serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kurekebisha kasoro hiyo, ikiwemo uzinduzi wa ujenzi wa barabara za juu katika eneo la Tazara.
Aidha, serikali ilibuni mradi wa mabasi yaendayo haraka kama moja ya njia za kupunguza msongamano huo wa magari barabarani, lakini binafsi ninaona bado kuna eneo ambalo halijaguswa, hasa katika kupata suluhisho la haraka.
Barabara za juu na mradi wa mabasi yaendayo haraka ni njia sahihi, lakini unafuu wake ni matokeo ya muda mrefu kama ambavyo kusuasua kwa safari za Uda-DART kunavyoonyesha na miaka miwili inayohitajika kukamilisha ujezi wa 'flyover' za Tazara.
Tatizo kubwa la foleni za magari jijini liko kwenye makutano ya barabara, ambapo magari hukwama hapo hata kwa saa nzima yakisubiri trafiki ayaruhusu yapite.
Kwa maana nyingine ni kwamba trafiki waliowekwa kwenye makutano ya barabara ndiyo wanaosababisha foleni za magari kwa mtindo wao wa kuruhusu magari ya upande mmoja kwa muda mrefu.
Mimi nadhani suluhisho la haraka la foleni ni kuruhusu taa zifanye kazi huku trafiki wakisimama karibu na makutano ya barabara ili kuangalia madereva wasioziheshimu taa hizo na kuwachukulia hatua.
Lakini mtindo wanaotumia sasa ni kero na tatizo kubwa, kwani taa zimesetiwa kwa mauda maalum na siyo kama ambavyo trafiki wamekuwa wakiruhusu magari kwa kujisikia ni upande gani upewe kipaumbele.
Matokeo yake ni kuendelea kupoteza pesa nyingi ambazo zingeokolewa iwapo wangeruhusu taa zifanye kazi huku wao wakibaki kushughulika na madereva wanaovunja sheria kwa kuvuka barabara bila kuruhusiwa na taa.
Aidha, ikumbukwe kwamba magari yanazidi kuwa mengi wakati miundombinu ya barabara ni ile ile ya mwaka 47, hivyo tatizo litaendelea kuwa kubwa na kupoteza fedha nyingi zaidi iwapo mbinu za kumaliza tatizo hili zitakuwa ni mabasi yaendayo haraka tu.
Kama nilivyosema awali, serikali imeanza mikakati ya kujenga barabara za juu kwa lengo la kupunguza foleni lakini suluhisho hilo litasaidia maeneo machache kama Tazara na Ubungo, wakati mengine yakiendelea kukumbwa na foleni.
Siyo vibaya pia baada ya kuanza kwa mabasi ya haraka, kuweka ushuru mkubwa kwa wale wanaotumia magari binafsi kuingia katikati ya jiji ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na foleni.
Kuwapo kwa ushuru mkubwa kwa wenye magari binafsi inaweza kusaidia kupunguza wingi wa magari barabarani na hata foleni na hivyo kufanya watu wawahi kwenye shughuli zao za kila siku.
Wakati hayo yakifanyika, serikali pia haina budi kujenga ofisi zake mpya maeneo mbalimbali ya pembezoni mwa jiji ili kupunguza wingi wa watu wanaoingia katikati ya jiji kupata huduma kwenye ofisi za serikali.
Ninaamini kwamba haya yakifanyika, upotevu wa fedha uliopo sasa utapungua kama siyo kumalizika kabisa na pia watu hawatalazimika kuamka usiku kuwahi foleni kama ilivyo sasa.
Kwa sasa imekuwa kama jambo la kawaida mtu kuamka saa 10 alfajiri kutoka Kibamba, Ukonga, Tegeta, Temeke kwenda katikati ya jiji kwa muda wa saa mbili badala ya nusu saa ama dakika 45 za kawaida.
Mbali na hilo, wingi wa malori ya mizigo ni tatizo lingine na hasa kutokana na ukweli kwamba yamekuwa yakiharibika hovyo na kuachwa katikati ya barabara kwa muda mrefu na kusababisha foleni.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







