Azam FC yaitamani Simba, Yanga

09May 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Azam FC yaitamani Simba, Yanga

NAONA kama haitaki kubaki kama Azam FC. Inataka kuwa kama klabu za Simba na Yanga. Sifa za kuwa na mashabiki wengi nchini wasioisadia lolote lile zaidi ya kushangilia inaonekana imewakolea mno Azam.

Inaona kama klabu hizi ndizo klabu za mfano Tanzania. Ukweli ni kwamba Simba na Yanga zinaishi kisiasa zaidi na si vinginevyo.

Azam, klabu iliyoundwa si miaka mingi sana, lakini ikatabiriwa kuwa moja ya klabu zitakazoleta mapinduzi kwenye medani ya soka nchini.

Ni kweli imefanya hivyo kwa baadhi ya vitu, ikiwemo kuwa na uwanja wake yenyewe, lakini bado kuna makandokando na udalili kuwa inapenda sana kuwa kama Simba au Yanga.

Uchumi ilionayo nilidhani kuwa ni klabu yenye uwezo wa kusajili wachezaji wenye viwango vya hali ya juu kutoka ndani na nje ya nchi ambako klabu kongwe zinasajili.

Sidhani kama Azam hii ingekuwa na akili ya kusajili mchezaji kutoka Simba au Yanga ambao mara nyingi wakishatoka huko, moyoni wanakuwa tayari wameshamaliza shughuli za soka na sasa wanakula pensheni tu.

Kama Azam kweli wangekuwa wanataka kuwa tishio, sidhani ni klabu inayobebwa zaidi na wachezaji wawili tu au watatu wa kigeni, wakati ina wachezaji saba.

Kwa uwezo wa hali na mali iliyonayo ni klabu yenye uwezo wa kusajili wachezaji saba wa kigeni wenye uwezo wa hali ya juu kutoka pembe zote za Afrika.

Kama Yanga, klabu inayosaidiwa tu fedha kutoka mifukoni mwa watu ina uwezo wa kununua straika wa hali ya juu kama Donald Ngoma, sidhani Azam inashindwa kununua mwenye uwezo mara mbili au tatu ya mchezaji huyo.

Ingekuwa na wachezaji saba wa viwango vya kina Pascal Wawa na Kipre Tchetche, nina uhakika ingekuwa si timu ya kutisha Tanzania tu, bali Afrika nzima.

Yote hii ni kwa sababu badala ya kutoka hapa ilipo kwenda mbele, inataka kufanana na Simba au Yanga ambazo ziko hapo miaka nenda rudi.

Ndiyo maana hivi majuzi imenyang'anywa pointi tatu kwa sababu ya kumchezesha beki Erasto Nyoni ambaye alikuwa na kadi tatu za njano.

Huu ni uzembe wa kutunza kumbukumbu uliowashangaza wadau wa soka nchini ambao wanaamini kuwa uendeshaji wa klabu hiyo ni wa kisasa zaidi kuliko Simba au Yanga.

Klabu hizo kongwe zimeshawahi kunyang'anywa pointi tatu kwa kuwachezesha wachezaji wenye kadi tatu za njano. Wengi hawakushangaa kwa sababu zinaendeshwa kizamani.

Simba ilishawahi kufanyiwa hivyo mara mbili kwa nyakati tofauti kwa kumchezesha Mussa Hassan 'Mgosi' na Juma Nyosso, Yanga ilikumbana na adhabu hiyo kwa kumchezesha Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Haikutarajia kabisa kwa klabu kama Azam kukumbana na kadhia hiyo.Inawezekana kabisa kuwa klabu hiyo sasa inatamani kuwa kama Simba au Yanga kiuendeshaji.