TFF inapompiga kalenda Waziri Mkuu Majaliwa

14Mar 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
TFF inapompiga kalenda Waziri Mkuu Majaliwa
  • Juni 4, 2014, Bunge la Tanzania liliiagiza TRA kuisimamia TFF kuhakikisha inatumia tiketi za elektroniki kwenye viwanja vyote vya soka nchini.

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokutana na viongozi wa vyama vya michezo nchini jijini Dar es Salaam hivi karibuni, aliliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhakikisha linarejesha mara moja mfumo wa tiketi za elektroniki kwenye viwanja vya soka.

Machi 4, mwaka jana shirikisho hilo kwa kushirikiana na iliyokuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, lilisitisha matumizi ya mfumo huo wa kisasa kwa madai kuwa umekughubikwa na changamoto kadhaa.

Kusitishwa kwa matumizi ya mfumo huo wa kisasa kulikorejesha mfumo wa kizamani wa tiketi za vishina, kulikuwa kinyume cha tamko la Bunge la Tanzania la Juni 4, 2014 lililoitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuisimamia TFF kutumia tiketi za kielekroniki viwanjani.

"Serikali haipati mapato ya kutosha kutokana na mpira wa miguu kwa sababu ya tiketi bandia kuendelea kutumika, kukosekana kwa uwazi katika mapato halisi, uwezo mdogo wa kusambaza tiketi nchi nzima na rushwa kwenye mageti ya viwanja," aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luhaga Mpina aliliambia Bunge mjini Dodoma siku hiyo.

"Kamati inashauri TRA iweke sharti la lazima la kuitaka TFF kutumia mfumo wa tiketi za kielektroniki katika kuuza tiketi zake ikiwa ni jitihada za kuongeza mapato ya serikali."

Na kwa kutambua umuhimu wa mfumo huo wa kisasa, Waziri Mkuu Majaliwa hajawa nyuma katika kupigania maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Wakati Watanzania wanasubiri kuona utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliuambia mkutano mkuu wa wanachama wa shirikisho hilo kuwa tiketi za elekroniki zitaanza kutumika katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengine ya kimataifa msimu ujao na si msimu huu kama ilivyoagizwa na Serikali.

Katika maelezo yake, Malinzi alisema kuwa kwa sasa agizo hilo halitekelezeki kutokana na upungufu aliodai upo kwenye mfumo huo.

Lakini, wakati TFF ikimpiga kalenda Waziri Mkuu Majaliwa, hujuma za mapato ya milangoni zinaendelea kupitia mfumo unaong'ang'aniwa na shirikisho hilo wa tiketi za vishina.

Hili linathibitishwa na TFF yenyewe kupitia ripoti yake ya 2011. Kwenye ukurusa wa 29 hadi 33 wa Ripoti ya Kamati Maalum na Kuboresha Mapato ya TFF, kunaelezwa kwa kina namna maofisa wa shirikisho hilo wanavyoshirikiana na polisi, makomandoo wa milangoni na wadau wengine wa soka kuhujumu mapato ya milangoni.

Binafsi ninaamini, kitendo cha TFF kumpiga kalenda Waziri Mkuu Majaliwa katika utekelezaji wa agizo la matumizi ya tiketi za kielektroniki ni mbinu ya kulinda 'ulaji' unaoendelea kupitia tiketi za vishina.

Na inazua maswali mengi yasiyo na majibu -- TFF imepata wapi utashi wa kupuuza maagizo ya Bunge na Serikali?