Mazingira yanayosababisha kipindipindu yaondolewe

13Mar 2016
Christina Mwakangale
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Mazingira yanayosababisha kipindipindu yaondolewe

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu hivi karibuni aliutaja mkoa wa Iringa kuongoza kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wapya wa kipindupindu ikilinganishwa na mikoa 11 nchini.

Iringa ulikuwa na wagonjwa 199 ukifuatiwa na mkoa wa Mwanza 87, Mara 84, Morogoro 54, Arusha 49, Simiyu 16, Dodoma 11, Mbeya 8, Kilimanjaro 8, Dar es salaam 6 na Manyara 6.

Hali hiyo inaweza kuwa inasababishwa na baadhi ya mazingira ambayo ni chanzo cha ugonjwa huu, hasa katika makazi ya watu na maeneo ya kazi.

Kukithiri kwa uchafu katika maeneo, ni sababu mojawapo ikisindikizwa na matumizi ya maji yasiyo safi na salama iwapo yakatumiwa katika chakula na mtu kunywa wakati hayajachemshwa kwa kiwango kunachohitajika.

Kwa nchi zilizoendelea, ugonjwa huu ni historia lakini kwa zinazoendelea ni tatizo, kutokana na hali ya kiuchumi kwa nchi, miundombinu hafifu wa kuweka mazingira bora hususan mfumo wa maji taka.

Tangu ugonjwa wa kipindupindu ulipoanza jumla ya watu 15,853 wameugua ugonjwa huo na kati yao 243 wamepoteza maisha hadi kufikia Februari 14, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Waziri Mwalimu, kipindupindu kimeendelea kusambaa kwa kasi ya ajabu hata katika maeneo ambayo walifanikiwa kudhibiti ugonjwa huo.

Anasema kuwa tangu Julai, mwaka jana Iringa ilifanikiwa kuudhibiti kwa kuwa na wagonjwa wawili tu, lakini inashangaza baada ya miezi minane ugonjwa huo kuibuka ghafla.

Ni kwa sababu hiyo Waziri Mwalimu amesema wizara yake inaendelea kutoa rai kwa jamii, wataalamu na viongozi katika ngazi zote kila mmoja kutimiza wajibu wake katika harakati za kuudhibiti ugonjwa wa kipindupindu.

Mwalimu aliwahi kutoa tamko la kupiga marufuku uuzwaji wa matunda yaliyokatwa ama kumenywa katika maeneo ya wazi; ambayo yanaweza kusababisha ugonjwa huo.

Biashara hii ni kubwa katika maeneo ya mjini. Jijini Dar es Salaam, ukipita pembezoni mwa barabara karibu zote utakutana na uuzwaji wa matunda hayo.

Ingawaje wauzaji huwa na maji kidogo katika vyombo vya kuhifadhia maji kwa ajili ya kuosha na kunawa mikono, kiasi hicho kinaweza kuwa hakitoshi kuyatakasa matunda haya ili yawe salama kwa mlaji.

Kwa mujibu wa wataalamu, maji yanayotiririka kutoka katika bomba yanafaa zaidi katika kuosha matunda au kusafisha mikono kabla ya kuanza kula chakula.

Hatua mbalimbali zinaweza kuanza kuchukuliwa ili kuepikana na ugonjwa huu, kwa kutoa elimu katika jamii na kufuata kanuni za usafi kwa kuhakikisha maeneo yanakuwa safi.

Kufanyika kwa usafi kuanzia katika makazi pamoja na maeneo ya kufanyia kazi ikiwamo biashara ni silaha tosha ya kupambana na ugonjwa wa kipindipindu.

Kudumisha tabia ya kunawa mikono baada ya kutoka maliwato kutapunguza pia milipuko, huku watoto wadogo wakianza kufundishwa kutumia utamaduni huo.

kipindupindu kitakwisha iwapo mazingira bora ya kukiepuka yatakuwapo, huku jamii nzima na mamlaka zikitekeleza majukumu yake.