TFF ijibu kwanza Yanga kutofanya uchaguzi

11Apr 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
TFF ijibu kwanza Yanga kutofanya uchaguzi

IMEBIDI sasa serikali kuingia kati suala la uchaguzi wa klabu ya Yanga.

Imeiagiza Yanga kuanza mchakato wa uchaguzi kuanzia Aprili 15.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikaiandikia barua klabu ya Yanga ifanye uchaguzi mwaka huu.
Yanga imekwishapokea barua hiyo kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Klabu hiyo imekuwa ikilalamikiwa na baadhi ya wanachama wake kutofanya uchaguzi tangu muda wao halali ulipomalizika 2014.

Pamoja na malalamiko hayo, Shirikisho la Soka Nchini (TFF) limeonekana kwa muda mrefu kama kuziba 'pamba' masikioni na kutoigusa klabu hiyo kuhusu suala la uchaguzi.

Ingawa mara kwa mara baadhi ya viongozi wa TFF walikuwa wakiibuka na kusema kuwa watahakikisha klabu hiyo kongwe inafanya uchaguzi, lakini imeonekana ni maneno ya mdomoni na hakuna dalili yoyote ile ya kuinyooshea vidole.

Uongozi wa sasa uliingia madarakani Julai 15, mwaka 2012 katika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi za viongozi waliojiuzulu chini ya Lloyd Nchunga.

Uongozi ulimaliza muda wake 2014, lakini uliongezewa muda wa mwaka mmoja Mei 2014 kwenye mkutano mkuu wa wanachama kwa kile kilichoelezwa kuwa kukamilisha masuala ya katiba na kuweza kuandaa mkutano wa uchaguzi baada ya katiba kupitishwa na TFF.

Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa Yanga walipinga na kudai kuwa uchaguzi ulitakiwa ufanyike Julai ili wapatikane viongozi halali na si kuongezeana muda.

TFF ilikaa kimya katika hili. Mwaka ulioongezwa umekwisha 2015, wako kimya.

Na hadi serikali inatoa maagizo kulikuwa hakuna dalili zozote za Yanga yenyewe kufanya uchaguzi, wala shirikisho kutoa msisitizo.

Cha ajabu ni kwamba TFF hiyo hiyo imekuwa na meno makali kwa klabu nyingine kufanya chaguzi zake haraka na kupeleka wasimamizi.

Hata klabu ya Simba iliwahi kukumbwa na mkono wa TFF kuagizwa kufanya uchaguzi mara moja, ingawa ilikuwa ni kinyume cha katiba kwa mujibu wa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo Ismail Aden Rage.

Timu zilizopanda daraja msimu huu, African Sports na Coastal Union nazo pia ziliagizwa mara moja kufanya uchaguzi.
Lakini kwa upande wa pili TFF ikawa 'inajisahaulisha' linapokuja suala la Yanga iliyokuwa haina viongozi halali tangu 2014.

Jambo hili linafanana sana na mzazi ambaye anawalazimisha watoto wake kwenda shule na siku wakitega anatwanga bakora, lakini yupo mtoto mmoja ambaye yeye hataki kabisa suala la kusoma na baba haongei chochote juu yake.

Anamuacha afanye anavyotaka. Aseme anavyotaka. Yeye anakaa kimya, akisubiri watoto wengine anaowamudu.
Mzazi huyu anadhani kuwa anampenda au kumbeba mtoto huyo ‘kipenzi’, lakini kumbe anamharibu.

Kufanya uchaguzi ni suala la kikatiba, lakini TFF ikawa iko tayari kuona ikivunjwa kwa klabu moja tu ya Yanga na si nyingine.

Ingekuwa klabu zote au mwanachama mwingine wa TFF hajafanya uchaguzi hadi leo, tungeongea kuwa TFF ni wazembe, lakini kumbe inajua kuwa klabu lazima zifanye uchaguzi isipokuwa Yanga tu, kuna namna.

Sidhani kama suala la kuitaka Yanga kufanya uchaguzi ilibidi litoke serikalini kupitia chombo chake (BMT) ambacho ndiyo kinasimamia vyama vya michezo nchini.

Nafikiri serikali ilisahau kitu kingine tu katika hilo. Nalo kwanza ni kuiuliza TFF ni kwa nini imeiacha Yanga kwa kipindi chote hiki bila kufanya uchaguzi?

Pamoja na hayo, wakati sasa Yanga inaelekea kwenye uchaguzi, TFF inabidi ijitokeze iwaeleze wadau wa soka ni kwa nini imekuwa ikiiacha klabu hiyo bila kuamuru kufanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya FIFA, CAF, TFF na klabu yenyewe?

Ilikuwa ni kigugumizi gani hadi ikawa inashindwa kabisa kuigusa Yanga kuhusu uchaguzi?
Kulikuwa na uswahiba gani kati ya viongozi wa TFF na Yanga hadi kusaidiana kusigina katiba?

Nina wasiwasi kama serikali isingeingilia kati suala hili, basi huenda klabu zote zingekuja kufanya tena uchaguzi kwa muhula mwingine hata wa TFF yenyewe, lakini Yanga ingeendelea kuwa klabu 'maalum' nchini isiyoguswa.

TFF inaweza ikawa ina sababu nzuri na za maana, hivyo wadau wa soka wanasubiri zijibiwe kwa ufasaha ili kurudisha imani kwa shirikisho hilo kuwa linafanya kazi bila upendeleo.

Vinginevyo wengi wataendelea kuwa na dhana ile ile inayosemwa kwenye mitandao ya kijamii na mitaani na kwenye vijiwe vya soka, kuwa ndege wa rangi moja huruka pamoja.