Ni kweli, Yanga na Azam bado zina nafasi

11Apr 2016
Renatha Msungu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni kweli, Yanga na Azam bado zina nafasi

YANGA na Azam FC mwishoni mwa wiki iliyopita zilikuwa dimbani kupeperusha bendera ya nchi katika mashindano ya klabu Afrika.

Mabingwa wa Bara, Yanga walikuwashuka dimbani kucheza na Al Ahly ya Misri kwenye Uwanja wa Taifa, huku Azam wakicheza dhidi ya Esperance ya Tunisia.

Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Azam kushinda mchezo wao kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi.
Matokeo hayo siyo mabaya kutokana na ukweli kwamba, mechi za marudiano ndiyo muhimu kwa sasa.

Kocha wa Yanga Hans va der Pluijm alisema baada ya mchezo kuwa, matokeo waliyopata yanaziacha timu zote kwenye nafasi sawa ya kusonga mbele.

Kwamba, kwao siyo jambo rahisi kukubalia kuwa sare hiyo ni kama tayari timu imeondolewe kwenye mashindano kama wengi wanavyosema.

Kauli ya Pluijm ina ukweli ndani yake, lakini tu kama watafanya vizuri kwenye mechi ya marudiano, ambayo historia haizipi nafasi timu za Tanzania dhidi ya Waarabu hasa zipocheza nchi ya Tanzania.

Kadhalika kwa Azam FC, ushindi wao wa nyumbani, haina maana kuwa tayari wameshasonga mbele.

Ushindi wao ni chachu ya kufanya vizuri kwenye mechi ya marudiano itakayochezwa wiki mbili zijazo.

Bila kujali matokeo ya mechi hizo, kuna mambo muhimu wawakilishi wetu lazima wafahamu kabla ya kusafiki kwa ajili ya mechi za marudiano.

Kwanza, makocha wa timu zote Azam na Yanga wameshazisoma timu hiyo. Wanajua jinsi zinavyocheza na mbinu wanazotumia.

Hilo peke yake ni darasa la kuwaanda kufanya marekebisho ya makosa yote waliyoyaona kwenye mechi za kwanza.
Kwa mfano, Pluijm aliwalalamikia wachezaji wake wa safu ya kiungo kucheza vibaya, hali iliyowaruhusu wapinzani wao kupitisha mipira mingi kwenda kushambulia.

Kama hili ni tatizo kwa Yanga, basi naamini kocha atalifanyia kazi na kurekebisha makosa yote ili mwelekeo wa ushindi uonekane.
Lakini pia, safu ya Yanga bado ina shida ya muda mrefu. Washambuliaji wake wanashindwa kutumia nafasi nyingi wanazopata kufunga mabao.

Katika nafasi tano, wanaweza kutumia moja tu kufunga. Naamini mwalim ameliona hili na atalifanyia marekebisho.
Lakini pia Yanga na Azam wanapaswa kuwa makini na mbinu chafu za timu za Waarabu hasa zinapocheza kwenye viwanja vyao.

Wachezaji lazima wajenge nidhamu ya hali ya juu kutokana na ukweli kwamba, Waabu wana mbinu nyingi zinazoweza kuwakwaza wachezaji uwanjani na kusababisha hata kupewa kadi.

Azam tumeshuhudia mechi yao. Ushindi walioupata lazima waulinde. Haitakuwa na maana kwa wao kuingia uwanjani na kujiona kama tayari wameshashinda mechi hiyo kwa kigezo cha matokeo ya mechi ya kwanza.

Azam kama Yanga nao wanapaswa kutumia kila nafasi wanayopata kufunga bao. Kucheza kwa kujilinda bila kushambuliwa kwa sababu tu tayari wametanguliza mguu mmoja mbele, hiyo haitawasiadia.

Wawakilishi wetu mkumbuke kuwa, maandalizi mazuri kwa ajili ya mechi za marudianoa ndiyo kiini cha wao kusonga mbele.

Kwa sisi wanamichezo, tunaamini kuwa timu inayojiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano ndiyo inakuwa jirani na mafanikio kuliko ile isiyofanya hivyo. Kila la Heri Yanga, Azam FC