Shule zimefunguliwa, walimu mjihadhari na UVIKO-19

27Jan 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Shule zimefunguliwa, walimu mjihadhari na UVIKO-19

TAYARI shule za msingi na sekondari zimeshafunguliwa. Wanafunzi wote wawe wanaoenda na kurudi nyumbani au wa bwenini, kwa sasa wamerejea masomoni baada ya mwezi mmoja na siku kadhaa za mapumziko majumbani mwao.

Hivi karibuni nchi yetu ikiwa ni safu ya dunia, ilikumbwa na upepo mbaya, baadhi ya watu waliumwa homa kali, mafua na kukohoa, wakiwamo hata wachezaji soka kiasi cha mechi zao kuahirishwa. Wengine walicheza huku wakiwa wagonjwa. Hakuna anayejiamini kwa usalama sana.

Upepo huo mbaya unatetema tukiwa si kisiwa, nchi yetu imo katika orodha ya wanaokabiliwa na ugonjwa wa UVIKO-19. Viongozi wetu wa ngazi za juu wameonyesha dhamira ya kutaka kuupunguza, kama si kutokomeza kabisa nchini.

Wakati viongozi wakuu wakionyesha dhamira hiyo, huku chini watu wa kada mbalimbali wanatakiwa kuwaunga mkono. Ni juzi tu akizungumza na wawakilishi wa Machinga jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan, alikumbusha tusijisahau kihivyo.

Viwandani, maofisini, hata shuleni ni wajibu wa kila mmoja kutekeleza kanuni za kupiga vita ugonjwa huo ambao Watanzania tusithubutu kujidanganya kwamba umekwisha kabisa.

Ni kweli kwa sasa kuna nafuu kutokana na dhamira ya dhati ya viongozi wetu kufanya kila njia liwezekanalo, tukianza na kuukubali kwamba upo, halafu ndio tunaingia vitani kuikubali kwa njia mbalimbali.

Leo nipo upande wa walimu wote nchini, ambao ni wiki moja na nusu sasa wamewapokea mamilioni ya watoto toka pande zote za nchi. Ni lazima waweke tahadhari ya kutoambukizana, wasiambukize au kuambukizwa.

Kwa walimu na wanafunzi wanaohudhuria kutwa, yaani kwenda na kurudi, walimu wao wanatakiwa wawakumbushe kunawa mikono kabla na baada ya kula chochote, pia waweke ndoo za maji tiririka na sabuni, ili wanawe wanapoingia na kutoka madarasani.

Pia mgeni yoyote anayeingia katika himaya ya shule kiofisi, au kwa darasa lolote, ni lazima apitie mlolongo huo huo wa kinga ya Uviko.

Wale wa mabwenini, kunapaswa wawekewe utaratibu wa kuwapima wanafunzi wote ambao wamerejea, kwa vipima joto ili kuhakikisha hawana jotoridi lililozidi kawaida. Hapo ndipo wajumuike na wenzao.

Hiyo ni kwa sababu wanakaa pamoja, hawana kazi kubwa sana kama wale wa kila siku wanaoenda majumbani na kurejea kesho yake.

La hatari zaidi lipo kwa walimu wenyewe wanaotakiwa kuwa makini maradufu, kwa sababu wana nafasi kubwa zaidi ya kuwaambukiza wanafunzi kwa sababu wote wanarejea majumbani.

Wanafunzi wao inategemea kati ya mmoja na mwingine, kulingana na kama yuko bwenini au la, pia kama wa bweni anapopata ruhusa kutoka shuleni.

Kingine ni kwamba, ifikie wakati walimu shuleni waanze angalau kidogo kutoa somo kwa wanafunzi juu ya kujikinga na UVIKO-19, jambo linaloweza kuwafanya wanafunzi kuwa na uelewa mkubwa zaidi wa ugonjwa huo, jinsi ya kujikinga kuliko hali iliyoko hivi sasa.

Mara zote, kumfundisha mwanafunzi ni sawa na kuifundisha jamii, kwa sababu huwa wanarudi majumbani na kuwaelimisha wazazi, familia, ndugu na jamaa wa karibu.

Wanafunzi wanatoka kwenye familia mbalimbali, za wazazi walioelimika na ambao hawajapata bahati hiyo. Hivyo, wazazi huwasikiliza na kuwaamini zaidi watoto wanaosoma kila wanachokileta nyumbani hasa kikiwa chanya, wanakipokea kwa mikono miwili.

Kilichobaki kwa walimu ni sasa wachukue tahadhari zote za UVIkO-19 wanapokuwa na wanafunzi, pia ni wakati wa kuanza kutoa elimu darasani juu ya ugonjwa huo, jinsi ya kujikinga ikilengwa si kwa manufaa yao tu, bali dira ya kuifikia jamii nzima.

Tujitahidi walimu, mara zote mwanzo huanza na moja walimu!