Ajali hizi zitufunze pia kukabili karaha za wenzetu barabarani

28Jan 2022
Anthony Gervas
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ajali hizi zitufunze pia kukabili karaha za wenzetu barabarani

JAMANI Watanzania wenzangu inauma kusikia ajali za huku na kule, tena baadhi zinatisha. Tujitahidi kuepuka ajali hizo zisizokuwa za lazima, uzembe, kuendesha mwendokasi, kutumia simu wakati dereva anaendesha gari, usingizi na unywaji pombe ni katika orodha ya yanayochangia ajali barabarani.

Ajali hizo watu wengi wamekuwa wakiziona kama vile za kawaida, kumbe zinapoteza maisha ya wengi wasio na hatia kila kukicha. Niseme kila kitu kina mwisho jamani! Ifikie mahali wananchi tupaze sauti zetu pamoja, ili tujinusuru kwenye mtego wa ajali za kila mara.

Utakuta dereva anaendesha basi la abiria safari ndefu kutoka mkoa kwenda mwingine anaongea na simu muda mrefu, gari liko mwendokasi halafu hataki kupunguza wala kumsikiliza abiria. Wakati mwingine anaweza kuwa na usingizi au alikunywa pombe bado iko kichwani, baadaye anaweza kusababisha ajali hiyo ya watu kupoteza maisha bila ya sababu.

Serikali wakati ikipigana kupata dawa rasmi ya kuhakikisha inapata mbadala wa kudumu katika kudhibiti ajali hizo zisizokoma, ni busara sura ya ufumbuzi wa kudumu iwapo kwa kuanza na kuyaondoa magari mabovu barabarani.

Hilo linaendana na wahusika wa usalama barabarani kama Polisi Trafiki kuwawajibisha wote wanaokumbatia uzembe huo, ikiwamo kupokea rushwa za wakosaji barabarani.

Mimi nampongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kuitaka serikali kuchunguza ajali ya watu 14 waliofariki dunia katika wilaya ya Busega mkoani Simiyu.

Hapo iliwajumuisha wanahabari wenzetu wa hapa Mwanza waliokuwa wakielekea wilayani Ukerewe kikazi na abiria wanane waliokuwa basi dogo aina ya Toyota Hiace, pia dereva wa gari la serikali walilokuwamo manahabari watano. 
       
Waziri Nnauye aliagiza polisi mkoani humo kuchunguza zaidi chanzo cha ajali hiyo na kutoa majibu, baada ya kushitushwa na ajali hiyo iliyotikisa Kanda ya Ziwa na Taifa, asubuhi saa 12:30 huko kijiji cha Shimanilwe wilayani Busega, baada ya gari la serikali kugongana uso kwa uso na hilo la abiria.

Ndugu wasomaji nawageukia wahusika wanaosimamia kitengo cha usalama barabarani(Trafiki), baadhi ambao huenda siyo waaminifu na wanasumbuliwa na pepo la kupokea rushwa, sababu mimi mwenyewe huwa napanda daladala na mabasi makubwa ya kusafiri na kuona mazingira nisiyokubaliana nayo.

Utashangaa pengine trafiki anasimamisha gari la daladala au basi kubwa la abiria, anapogundua lina makosa anazunguka nyuma yake na kumuita dereva au kondakta anayeshuka kumfuata, bila ya kujali ushuhuda fulani kutoka kwa abiria.

Baada ya hapo, anaendelea kukagua na baadaye anaruhusu gari liondoke, kukiwapo mazingira ya ukaguzi wenye kiulizo.

Sasa nawauliza enyi mnaolinda maisha yetu ya kila siku barabarani, baadhi yenu kuachia gari bovu katika mazingira hayo tata, hatujui tunaidhinisha mazingira ya ajali kwa gari hili bovu? Je,huo ni uungwana?

Hapa Mwanza nitoe kauli ya kuwakemea wenye pepo la rushwa waliepuke ili kunusuru maisha yetu Watanzania wana Mwanza. Nawaombeni mtumie busara na hekima, pia maadili ya kazi zenu.

Ndugu zetu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) naamini hili liko kwenye dhamana yenu kulichukulia hatua na ibaki simulizi. Mtafanya vipi, jibu limo kwenye stadi zenu kikazi, pia mna nafasi ya kushirikiana kiutawala na mabosi wao hao wakosaji, muangalie namna gani mnaweza kulimaliza.

Nichangie kidogo tu. Takukuru nawafumbua macho hebu mthubutu kupanda daladala kwa siri na kushuhudia yanayotokea humo, niweke mfano wa Mwanza ninakopatikana, mjionee uhalisia unaotia karaha nafsi yangu huwenda na wengine.

Msisubiri mpaka kuletewa malalamiko au taarifa ofisini, nanyi jiongezeni. Huenda inaweza kufika pabaya watu wamenogewa na tabia, wanashindwa kuacha.

Tumeingia 2022, ugonjwa uleule na tabia ile ile ya mwaka jana inaendelea na huenda imekolezwa zaidi.