Ripoti imegundua kuwa uzalishaji wa gesi joto duniani uliongezeka katika muongo mmoja uliopita kwa zaidi ya asilimia 12, ukilinganishwa na mwaka 2010, hali inayorudisha nyuma kasi ya kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzi joto1.5.
Ikiwa dunia imebakisha miaka mitatu tu kufikia malengo ya kuzuia ongezeko la joto kufikia nyuzi joto 1.5, ripoti hiyo imeeleza lengo hilo pamoja na kufikia hewa chafu sifuri, halitofanikiwa bila ya kutumia mbinu mbalimbali, kama vile kupanda na kuzuia ukataji miti.
Hapo juhudi za umma zinahamia, kwenye matumizi ya nishati na teknolojia. Ni dhahiri kuwa serikali ya nchi yoyote haiwezi kufikia makubaliano hayo peke yake, bali inahitaji msaada kutoka sekta binafsi na wadau wengine wa mazingira.
Ndio maana serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, ilipofanya maboresho ya Sera ya Mazingira, ikaja na mpya ya mwaka 2021, kuleta inayoendana na hali ya sasa ya ukuaji teknolojia, kasi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na ushirikiano na sekta binafsi.
Lakini, kuonyesha ushirikiano na sekta binafsi katika sera hakutozaa matunda, kama serikali haitoonyesha kwa vitendo kufanya kazi bega kwa bega na watu hawa katika utunzaji mazingira.
Tuna taasisi za mazingira zinazofanya kazi nzuri ya utekelezaji wa agizo la asasi kimataifa katika mazingira UNFCC la kuhakikisha kila nchi kwa nafasi yake inapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kufikiwe lengo la mwaka 2025 la kuzuia ongezeko la joto.
Kuna taasisi zinafanya kampeni ya kuhamasisha upandaji wa miti shuleni kwa kuwapa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari elimu ya utunzaji miti, pamoja na kugawa miti inayopandwa katika maeneo hayo.
Pia, kuna zinazomilikiwa na wanawake, ambazo nazo zinafanya kazi nzuri ya kuelimisha jamii hasa vijana na wanawake juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuwapa njia mbadala kuepuka kukata miti wanawake, ikiwamo kutengeneza mkaa unaotokana na taka.
Hizo pamoja na nyingine nyingi, zinajitoa kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya kupunguza makali ya ongezeko la joto, lakini zinahitaji serikali kuzishika mkono ili ziweze kutimiza malengo hayo.
Shime kwa serikali kuzitafuta na kusaidia kwa hali na mali, kwa kuwa ndio waliopo karibu na jamii, hivyo kazi wanazofanya zina matokeo makubwa kwa kuwa zinafika ambako yenyewe haiwezi kufika.
Si serikali tu, hata mashirika makubwa kama vile ‘UN-Enviroment’, zinapaswa kuzifikia taasisi ndogo kwa kuzipa msaada kidogo, ikiwemo nauli na vitendea kazi, pia motisha ya kuendelea kufanya vitu vizuri katika muktadha wa kimazingira.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








