Niseme, Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa nguzo muhimu ya kuunganisha Watanzania na kuwa wamoja wenye mshikamano na amani, ambavyo vimewaunganisha kwa lugha moja ya Kiswahili na kuwawezesha kutambuana na kuishi kama ndugu licha ya wingi wa makabila yaliyoko nchini.
Ninaamini, bidii yake katika kuwatumikia Watanzania kwa bidii, weledi na uadilifu mkubwa, vitaendelea kumfanya kuwa Mwalimu muhimu wa siasa safi kwa Watanzania na hata nje ya mipaka ya Tanzania.
Kwa mtazamo wangu, amani, mshikamano wa Watanzania umoja wao na maendeleo, mzizi mkuu wa hayo ni Baba wa Taifa, kwani hilo hakulifanya tu kwa Tanzania, bali hata kwa mataifa mengine.
Ninaamini kuwa wale waliofuatilia historia yake, watakuwa wanamjua wajihi wake, alikuwa yu daima tayari kusaidia mataifa mengine ya Afrika kujikwamua katika madhila ya harakati za ukombozi, umaskini, misukosuko na hali tete ya kisiasa.
Alisisitiza mambo mengi kuanzia masuala ya uchumi, siasa na dini na ukabila, ambalo ni nyeti Baba wa Taifa aligusa katika hotuba nyingi alizowasilisha akiukemea kwa kuwa alijua madhara yake.
Mwalimu Nyerere, amekemea suala la ukabila kila alipopata nafasi ya kuzungumza na hakutaka kuwapo maswali kama ‘wewe ni kabila gani’, kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kwani hadi sasa Watanzania hawaulizani kabila.
Nyerere aliamini katika itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea na hakutaka udini upewe nafasi, kwa kuwa alijua kwamba mambo hayo yakichochewa na kupewa nafasi hayana simile, ikifika wakati ukashika kasi hakuna wa kuzuia.
Kwenye suala la uongozi na maadili ya uongozi, ni jambo ambalo Baba wa Taifa aliliweka mbele, kwa lengo la kupata viongozi ambazo wanawatumikia Watanzania badala ya kufanya kazi kwa manufaa binafsi.
Hata alipoona ndani ya CCM mambo yanakwenda ndivyo sivyo, hakusita kutamka haradharani kuwa Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM, watayapata nje ya CCM.
Kauli hiyo inaonyesha wazi kuwa alikuwa na dhamira ya dhati ya kutaka viongozi wawe wa serikali au chama, kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ili waaminike kwa wananchi badala ya kwenda kinyume.
Aidha, alitamani kuunganisha nchi za Afrika Mashariki, na kuwa na uongozi wa pamoja, ingawa hakufanikiwa katika hilo, lakini akafanikiwa kuunganisha Tanganyika na Zanzibar na kuwa na nchi moja inayoitwa Tanzania.
Yapo mengi ambayo Baba wa Taifa alikuwa akiyasisitiza katika uongozi wake na hata baada ya kung'atuka, lakini lingine zaidi ni suala la kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.
Kabla ya kurejeshwa kwa mfumo huo, iliundwa tume ya kukusanya maoni ya Watanzania ili kuona kama wanautaka mfumo huo, asilimia 80 ya Watanzania walitamani kuona nchi inaendelea kuwa na mfumo wa chama kimoja.
Hata hivyo, Baba wa Taifa aliingilia kati na kushawishi Watanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi kwa kuwa isingekuwa busara kwenda kinyume na mabadiliko ya dunia na pia isingekuwa vyema kuwapuuza asilimia 20 waliotaka mfumo wa vyama vingi.
Baada ya maelezo hayo, ndipo nchi ikaingia ndani ya mfumo huo, huku vyama vya siasa vikianzishwa kama utitiri na kisha uchaguzi wa kwanza ndani ya mfumo huo ukafanyika mwaka 1995, kurejea ilivyokuwa kabla ya mwaka 1964.
Wakati makongamano, shamrashamra na mambo mengine, maeneo mbalimbali kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 100 tangu alipozaliwa Baba wa Taifa, ni muhimu kukumbuka mchango wake kwenye mageuzi nchini.
Ingawa kuwa na mfumo wa vyama ilikuwa ni kwenda kinyume na matakwa ya Watanzania wengi, matamanio yake yalikuwa ni kwamba, Watanzania wanaotaka kushiriki siasa nje ya CCM wasibanwe bali wawe huru.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







