Kwa nini rushwa imekithiri kiasi hiki? Jibu lake ni: “Mwana umleavyo ndivyo akuavyo.” Kwa kawaida mwana (mtoto) hukua jinsi alivyolelewa. Akilelewa vibaya ataishia kuwa na tabia mbaya.
Ni methali ya kuwanasihi wazazi wawalee watoto wao vizuri ili wawe na tabia nzuri na kuwa watu wa kutegemewa. Kwa muktadha huu, ‘wazazi’ ni serikali na ‘watoto’ ni wananchi.
Wakati Mwalimu Julius Nyerere akiongea na waandishi wa habari wa ndani na n-nje Machi 14, 1995 kuhusu rushwa, alisema:
“Rushwa katika Tanzania yaelekea sasa imefikia pabaya. Kila nchi ninayotembelea naulizwa kuhusu rushwa Tanzania. Serikali ikishakuwa ya kuwatumikia matajiri, haiwezi kushinda vita dhidi ya rushwa na wala haiwezi kukusanya kodi.”
Siku hizi magazeti hununuliwa sana kutokana na kufichuliwa kashfa za rushwa. Hakuna eneo lililosalimika kwa rushwa.
Serikalini, taasisi na mashirika ya umma, vyama vya ushirika, vyama vya michezo, wakandarasi wa ujenzi wa barabara na majengo, na kampuni za watu binafsi.
Kama si ukwepaji wa kodi wa makampuni makubwa, hususan zenye migodi ama kutoa bidhaa bandarini bila kulipia ushuru wa forodha, rushwa imekuwa ikigawanywa kwa wakubwa ili kupata upendeleo wa aina fulani.
Mpaka sasa nashindwa kuelewa yule mfanyabiashara aliyegawa mamilioni na mabilioni ya hela kwa watendaji wakuu wa serikali, viongozi wa dini na watumishi wa benki alikuwa na maana gani. Kuna waziri aliyesema mamilioni aliyopewa ni “hela za mboga!”
Hivi karibuni timu nne za daraja la kwanza zilishushwa daraja kwa kosa la kupanga matokeo ya mechi zao za mwisho ili mbili kati ya hizo zicheze Ligi Kuu ya Vodacom msimu ujao.
Timu hizo ni Geita Gold ‘iliyoifunga’ JKT Kanembwa mabao 8-0 na Polisi Tabora iliyopata ‘ushindi’ wa mabao 7-0 dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha. Baada ya minong’ono na Shirikisho la Kandanda Nchini (TFF) kutakiwa zichunguze kashfa hiyo, likachukua uamuzi wa kushangaza!
Yashangaza kwa sababu kumtoza mcheza kandanda wa timu ya daraja la pili faini ya Sh. milioni 10 ni sawa na kupakia mzigo wa tani 10 kwenye Bajaji! Watu watakushangaa kama tunavyoishangaa TFF sasa. Sijui viongozi walikusudia kuficha jambo gani wakati maji yesha mwaika!
Viongozi waliofungiwa maisha kwa kashfa hiyo ni Yusuph Kitumbo (Mwenyekiti wa Tarefa), Fateh Remtulla (Katibu Mkuu wa Tarefa) na kocha msaidizi Bernard wa timu ya Polisi Tabora. Pia yumo Mwenyekiti Amos Mwita wa JKT Oljoro Arusha na kocha msaidizi Choki Abeid wa Geita Gold.
Wengine ni mwamuzi Salehe Nang’ola aliyechezesha mechi kati ya Kanembwa JKT na Geita Gold na aliyekuwa kamisaa wa mchezo huo, Moshi Juma.
Masoud Mkeremi aliyechezesha mechi ya Polisi Tabora na Oljoro JKT na mwamuzi wa akiba wa mechi ile, Hamisi Machunde na kipa Dennis Richard wa Geita Gold wametozwa faini ya Sh. milioni 10 kila mmoja na kufungiwa kwa miaka 10.
Wakati hayo yakitendeka, Yapo madai kuwa baadhi ya viongozi wa TFF waliomba rushwa ya Dola 25,000 (Shilingi milioni 50 na ushei) kwa uongozi wa Geita Gold ili waisaidie timu hiyo kupanda daraja icheze Ligi Kuu ya Vodacom msimu ujao.
Kwa usemi uliozoeleka siku hizi, mmoja wa watuhumiwa alisema: “Kama wao wamemwaga mboga, sisi tutamwaga ugali. Ushahidi tunao … walitaka tuwape Dola 25,000 ili watusaidie kupanda daraja.
“Isitoshe kuna muda (anatajwa kiongozi mmoja kwa jina) alipigiwa simu akasema anamaliza kazi ya jamaa. Ameagizwa na (anataja jina la kiongozi wa juu wa TFF) aikamilishe. Huyo jamaa ni nani na aliingia kwenye kamati kama nani?” anauliza msemaji huyo.
Kashfa ya kupanga matokeo haikuanza leo wala jana. Ni ya miaka mingi iliyopita ila TFF imeziba masikio. Pia viongozi wa Polisi na Takukuru ni kama hawapo! Mbona walikuwa kimya hata baada ya kusikia tetesi za shutuma hizo? Au wanasubiri walalamikiwe ndipo wafuatilie?
Nilidhani vyombo hivyo vingetumia intelijensia zao kuchunguza na kuwatia mbaroni wahusika lakini ni kama havihusiki. Kuna wakati mchezaji Nsa Job alitangaza hadharani kuwa viongozi wa timu fulani walimwahidi kumpa rushwa kuisaidia timu pinzani ishinde.
Huo ulikuwa ushahidi tosha kwa Polisi na Takukuru kufuatilia na kuwakamata wahusika kwani tayari kulikuwa na ushahidi usio na shaka. Leo ni miaka mitatu hivi mhusika hajakamatwa na yasemekana ni kiongozi mkubwa!
marobarnabas@yahoo.com
0715/0784 33 40 96


.jpg?itok=nfwjwDzv)








