Maendeleo hayaletwi kwa malumbano Dar

10Apr 2016
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Maendeleo hayaletwi kwa malumbano Dar

MWISHONI mwa Februri Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Boniface Jacob alimtaka aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuacha kuingilia majukumu ya halmashauri na afanye kazi zinazomuhusu.

Meya huyo akasema kuwa amelazimika kumuonya Makonda kutokana na tabia ya kutafuta sifa ili aonekane mchapakazi, hali ya kuwa anadandia yasiyomuhusu.

Akasema kuwa ma-DC nchini wana majukumu muhimu matatu tu ambayo ni Uenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Uenyekiti wa Kamati za Mashirikiano pamoja na kuwa Kiunganishi wa Serikali ya Mtaa na Serikali Kuu.

Meya Jacob akasema kuwa kilichosababisha atoe ufafanuzi huo ni kitendo cha Makonda kuueleza umma kwamba Halmshauri ya Kinondoni imepokea dola za Marekani 300,000 kutoka Benki ya Dunia (WB) ili kujenga barabara, wakati tangazo hilo lilipaswa kutoka halmashauri yenyewe.

Akafafanua kuwa hakuna sheria inayomruhusu Makonda kushirikiana kikazi na halmashauri hadi awasilishe barua ya maombi kwa Mkurugenzi ama Meya kama anahitaji kufanya jambo lolote.

Lakini alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo dhidi yake, Makonda alijibu kwa kifupi tu kwamba linalomsumbua Mstahiki Meya Jacob ni ugeni wake katika kazi.

Miezi miwili tangu malumbano hayo, yameibuka mengine kati ya Makonda, ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita.

Viongozi hao wa serikali kuu na mamlaka ya serikali za mitaa, kwa nyakati tofauti wametoa kauli zinazokinzana, hali inayoashiria kwamba mbele ya safari huenda hali isiwe shwari na hivyo kukwamisha maendeleo.

Mara baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi wa Meya uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita, Mwita alisema atashirikiana na wote bila kujali itikadi za kisiasa ili kuleta maendeleo jijini.

Mbali na hilo, hivi karibu akasema kuwa atakuwa tayari kushirikiana na Makonda iwapo tu mteule huyo wa Rais atakuwa na nia njema ya kuleta maendeleo na siyo kufanya siasa.

Meya Mwita alisema hayo ikiwa ni siku chache tangu Makonda aweke wazi kwamba mamlaka ya uamuzi ya utendaji kazi Mkoa wa Dar es Salaam yako mikononi mwake.

Kwa kauli hizi za kupishana ni wazi kwamba huenda shughuli za maendeleo zikakwama na badala yake malumbano yakachukua nafasi kwa miaka mitano ijayo na hivyo jiji kuendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zilizopo sasa.

Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanataka kutatuliwa kero zao zikiwamo za usafiri, maji, usafi wa mazingira, lakini ajabu ni kwamba wahusika wa kusimamia maendeleo wanalumbana!

Je, kwa utaratibu huu tutafika? Kila mmoja anadai kuwa hataki kufanya siasa, lakini malumbano yao yana kila dalili ya kuwa ni siasa. Kwa nini wasikae pamoja na kupanga mipango ya maendeleo?

Ninajua kwamba Mstahiki Meya Mwita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anatokana na mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Naye Makonda ni kada wa Chama Cha Mapinduzi.

Lakini hilo lisikwamishe shughuli za maendeleo. Cha msingi ni maendeleo kwanza vyama baadaye