Kupitia mtandao rasmi wa Instagram wa Shirikisho la Soka nchini na Bodi ya Ligi, wamewataka wadau wote wa soka kutuma maoni kuhusu maboresho ya kanuni ili kuifanya iwe bora zaidi.
Ikataka mdau anayetaka kutoa mapendekezo ya maoni yake, au maboresho kutuma kwa barua pepe 'maoni@ligikuu.co.tz.'
Maoni hayo hupelekwa kwenye kamati husika kuchakatwa, kurekebishwa na hatimaye kupitishwa kwa ajili ya msimu husika.
Wakati Ligi Kuu msimu huu ukiendelea, baadhi ya mashabiki wa soka, wakiwamo hata baadhi ya viongozi wa klabu mbalimbali wamekuwa wakilalamika baadhi ya kanuni hasa pale zinapoanza kufanya kazi.
Hata hivyo, ni hao hao baadhi ya viongozi wa klabu ambao nao wanahusika kuziunda na kuzipitisha, lakini zinapoanza kuwagusa wanalalamika.
Tumekuwa tukiona viongozi, waandishi wa habari na wachambuzi wa masuala ya michezo wakilalamikia baadhi ya maamuzi yanayotolewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi kwa madai kuwa hayakutenda haki, au yamepitwa na wakati.
Lakini kwenye nyakati kama hizi huwa watuwasikii wakipeleka maoni mapya, au kuhitaji marekebisho ya kanuni zilizopita.
Hiki ndiyo kipindi ambacho husikii wachambuzi au mashabiki wa soka wakihamasishana kupeleka maoni, lakini ngoja siku maamuzi ya adhabu yatoke kwa mujibu na kanuni ambazo zimeletwa, kuchakatwa na kupitishwa na kamati husika, ndipo mapovu yanapoanza kuwatoka.
Uzuri ni kwamba maoni anapeleka mtu yeyote, shabiki, mpenzi, mwandishi, mchambuzi, mdau, kiongozi wa soka na yoyote yule anayeguswa na mchezo huo. Hayabagui.
Huwa nashangaa sana wanavyokurupuka na kulalamika mtu anayefungiwa kujihusisha na soka miaka mitano kuwa ni mingi na imepitwa na wakati.
Lakini kwenye nyakati hizi za kupeleka maoni na maboresho kuwa soka letu kwa sasa limekuwa la kulipwa na makocha, viongozi kwa sasa hiyo ndiyo kazi yao inayowapatia kipato cha kuendesha maisha na familia zao, na si kama zamani soka lilikuwa la ridhaa, hivyo kumfungia mtu miaka mitano ni kama vile kumkamlisha ubaoni bila kazi yoyote, hivyo kuifanya familia yake iathirike.
Huu ndiyo wakati wa kupeleka maoni ya kurekebisha kanuni hiyo kuwa ni ya kizamani, enzi za soka la ridhaa ambapo soka ilikuwa ni burudani, kuleta mahusiano, upendo, mshikamano na afya, huku makocha, viongozi na wachezaji wakifanya kazi zingine kwenye makampuni mbalimbali.
Hivi karibuni tumeona jinsi Mbeya Kwanza ilivyonyang'anywa pointi kwa kulazimisha kutocheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Namungo kwa madai ya kuchelewa kwa gari la wagonjwa, ingawa inadaiwa lilikuja ndani ya muda.
Sasa ni wakati wa kupeleka mapendekezo ya maboresho kwa jinsi unavyoona kuwa kanuni hiyo haifai. Na kama inafaa gari inatakiwa iwe mwanzo wa mechi hadi mwisho isiondoke katikati na kurudi, au vyovyote unavyoona.
Nilimsikia Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, akilalamika kuhusu kukatazwa kuchezesha wachezaji wote 12 wa kigeni waliosajiliwa kwenye Ligi Kuu, badala yake wanatakiwa kucheza nanane kwa mechi moja.
Si yeye tu, mashabiki wengi wanaipinga kanuni hiyo, huu sasa ndiyo wakati wake wa kwenda kupeleka maoni kuwa irekebishwe, wachezaji wote wanatakiwa waanze iwe wa kigeni wa wa kibongo bila ubaguzi.
Kuna faini za timu kupitia milango isiyohusika. Wengi wanalalamika, wanasema ni ndogo sama na ndiyo maana timu hazijali, zinaendelea tu na tabia hiyo.
Kinachotakiwa sasa ni kupeleka maoni ya kutaka faini iongezwe, ili timu ikipigwa, basi ijifikirie tena kurudia kosa.
Maoni yapo mengi sana kuhusu kanuni ambazo zimeonekana kuwa kero, lakini mashabiki na wachambuzi wamekuwa ni kama kawajui msingi wake umetokea wapi.
Ni kwamba wakati zinatumia haipaswi kulalamika, kwani watu wametoa maoni wakiwamo hao hao viongozi na makocha na zikapitisha.
Kanuni pekee ambayo inaonekana kutiliwa mkazo sana na hasa viongozi wa klabu za mikoani ni ile ya wao kuchukua mapato yote ya milangoni zikicheza na timu za Simba au Yanga.
Ndiyo maana hii ipo kwa misimu mitatu sasa, lakini zingine wanaziacha hadi pale zinapowachapa wenyewe ndipo wanaanza kupigia kelele watu.
Nawasihi wanamichezo wote kupeleka maoni ya mapendekezo ya kanuni mpya, au kuboresha zilizopo ili zitakazoanza kutumia msimu ujao zile ni zile zilizopendekezwa na wadau wenyewe na si vinginevyo.
Kama wanavyosema wenyewe Bodi ya Ligi ni kwamba, "Kanuni bora na rafiki huzaa ligi bora."



.jpg?itok=nfwjwDzv)








