Mathalani, mara kadhaa na hata wiki iliyopita, wamesema watawashughulikia ipasavyo wenye nyumba za ibada, kumbi za starehe na wengine ambao wamegeuka kuwa kero kwa wananchi kwa kuwa wanaendesha shughuli zao hadi usiku wa manane.
Kwa sasa, kasi ya kufungua baa na kumbi za starehe inaongezeka na mbaya zaidi ni ambazo hazina vifaa vya kuzuia sauti huku zingine zikiwa katikati ya makazi ya watu.
Mathalani, maeneo ya Tabata na Sinza kwa sasa kumekucha kwa kuwa na kumbi za starehe zinazopiga muziki hadi usiku wa manane kiasi kwamba wananchi wanaoishi jirani hushindwa kupumzika, inakuwa nao wako kwenye hizo kumbi kwa kuwa muziki ni mkubwa sana.
Pia nyumba za ibada zinazoendesha mkesha usiku kucha kuanzia Jumapili hadi Jumapili, zinazidi kuongezeka na mbaya zaidi hazizingatii vigezo vya ujenzi ili kudhibiti kelele ambazo ni kero kwa wengine.
Kwa hayo yote tumewasikia NEMC wakitoa onyo kali lakini bado hatujaona watu wa mfano waliokamatwa na kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria, ili wanapojenga kumbi hizo wazingatie vigezo vyote kwa kuzuia sauti.
Kuna wakati NEMC ilitoa orodha ya kampuni zinazomiliki vituo vya mafuta ambavyo vilijengwa bila kupata vibali vya mazingira, baadhi vilikuwa mjini na vilishaanza kuendesha shughuli.
Swali la kujiuliza ni kwa nini wanafikia kufanya hivi na nani yuko nyuma ya wawekezaji hawa kiasi cha kuidharau mamlaka halali kama NEMC kuanza kazi bila kuwa na cheti cha ukaguzi wa mazingira?
Hii inazidi kuleta wasiwasi juu ya nguvu za NEMC kama inaachwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria,yawezekana mbele tukawaona wao kwamba wameshindwa kukamata au kufungia nyumba za ibada au kumbi za starehe ila kumbe wanavutwa 'shati' kutekeleza wajibu wao.
Ziko familia zimehama nyumba zao kutokana na uwapo wa kumbi na nyumba hizo za ibada. Mtu anatoka nyumbani kwake kwenda kutafuta anarudi hapati muda wa kupumzika na mbaya zaidi nje ya geti lake anakuta wamejaa madada poa wanaojiuza na kufanya ufuska bila woga.
Kwenye nyumba hizo kuna wagonjwa, wazee na wanafunzi ambao wanahitaji utulivu lakini tunalea vijana ambao wanaposikia haya mambo na kuyaona mara kwa mara wanaona ni jambo la kawaida wanatakiwa kulifanya.
Nakumbuka kuna wakati jijini Dodoma ilianzishwa operesheni ya kukamata wanaopiga muziki hadi usiku mnene. Cha ajabu kwa sasa wamerudi kama kawaida na wako wanaokesha hadi asubuhi kuanzia Ijumaa hadi Jumatatu.
Bila kuchukua hatua kwamba tumeamua kuondoa uchafu wa kelele tutaendelea kuwa na sehemu kubwa ya jamii ya mjini ya hovyo na kuendelea kuharibu watoto.
Lazima kuwe na usimamizi thabiti wa kumbi za starehe ni kweli nchi inataka kodi na tunataka kuona biashara zinastawi ili kurahisisha maisha ya watu, lakini ustawi wa watu kiafya na kiakili ni muhimu mno.
Kwa mfano katika jiji la Arusha kuna eneo linaitwa stress free zone huko ni balaa lingine, unakutana watoto wa umri wa kati wanajiuza kiasi cha kujiuliza ni kizazi cha aina gani cha baadaye kinaandaliwa.
Kote huko muziki ni usiku kucha kiasi cha kujiuliza mamlaka za serikali hazioni?, hatua gani zinachukuliwa kwanini kusiwe na utaratibu wa kutengeneza maeneo haya yasiwe kero kwa wengine?
Unapotembelea nchi zilizoendelea kama Marekani, Thailand na Denmark wanafanya starehe, wana kumbi nzuri za kisasa na huwezi kukuta inakuwa kero kwa wengine,utamaduni huo umejengwa na umezoeleka.
Tunaweza kusema huenda nchi hizo ni kwa sababu zina baridi muda mwingi, lakini kuna nchi kama Afrika Kusini na Botswana ni nadra kukuta kelele za kumbi za starehe, maana yake ni kiwango cha juu cha kustaarabika na usimamizi thabiti wa sheria unaofanywa na mamlaka husika.
Ni muhimu NEMC ikachukua hatua ili kukomesha tabia hizi,naamini wakichukuliwa hatua pasipo kuangalia vyeo au fedha walizonazo, bali kujali ustawi wa wengine na siyo kujali fedha hali itakuwa nzuri.
Kama ni eneo la starehe tupu kama Mlimani City ambako hakuna makazi ya watu karibu hiyo haina neno,lakini ikiwa ni jirani kabisa na watu ni kuwaumiza kwa makusudi na kuwanyima haki yao ya kikatiba.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








