Matumizi ya simu yanavyoathiri uhusiano wa wanandoa – 1

15Aug 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Makala ya Jamii
Matumizi ya simu yanavyoathiri uhusiano wa wanandoa – 1

​​​​​​​MAWASILIANO ni jambo muhimu katika uhusiano na katika maisha ya kila siku. Mawasiliano yanapokosekana huathiri uhusiano. Hata pale mawasiliano yanapokuwapo lakini yakakosa nidhamu na utaratibu pia kuharibu uhusiano.

Utafiti unaonyesha kuwa, asilimia 90 ya sababu za kuvunjika kwa ndoa ni hutokana na mawasiliano mabaya ya wanandoa. Wanandoa wanahitaji kufahamu ukweli huu na kujifunza kuishi kwa utaratibu na kuwasiliana vizuri ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima katika ndoa.

Simu za mkononi ni chombo cha mawasiliano. Simu hizi zimerahisisha mawasiliano na zimeleta mapinduzi makubwa katika kuboresha mawasiliano duniani. Pia zimechangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kiwango kikubwa.

Mara nyingi simu zetu haziko mbali nasi. Watu wengi tunazo simu zetu wakati wote. Simu za mkononi zimechukua maisha yetu na sehemu kubwa ya muda wetu. Tunaziangalia na kuzitumia mara kwa mara. Ni uhusiano ambao unaonekana kuwa utadumu kwa muda mrefu, hivyo, nidhamu binafsi (self-discipline) inahitajika katika matumizi yetu ya simu.

Simu ya mkononi ni chombo kizuri sana na muhimu. Utafiti unaonyesha kuwa simu ya mkononi ndicho kifaa cha elektroniki kinachouzwa kwa wingi zaidi duniani. Pamoja na mazuri mengi ya simu za mkononi, simu hizi zimeleta matatizo katika ndoa na kuvunjika kwa uhusiano.

Jambo la muhimu na la msingi la kuzingatia ni kwamba simu zenyewe si tatizo bali tatizo ni watumiaji wa simu. Simu inaweza kusababisha changamoto nyingi katika uhusiano kutegemeana na  mtu anavyoitumia.

Baadhi ya wanandoa wamekuwa wasaliti katika ndoa zao kutokana na matumizi ya simu. Simu zimetumika kupanga mipango ya udanganyifu katika uhusiano. Simu pia  zimeondoa uaminifu, upendo, na ukaribu wa wanandoa.

Hata hivyo, kwa wengine, simu za mkononi zimeboresha na kuimarisha uhusiano wao na kuwafanya wanandoa kuwa karibu zaidi kutokana na uaminifu na kujengeka kwa tabia ya uwazi na ukweli miongoni mwao.

Mawasiliano yanaweza kuboreshwa na kuendelezwa. Kama kweli wanandoa tumejitoa kwa ajili ya ndoa na familia zetu, kila mmoja atafanya jitihada katika kujifunza namna bora ya kutumia simu yake ya mkononi. Matumizi mazuri ya simu na mawasiliano mema huepusha migogoro isiyo ya lazima katika ndoa.

Mwanandoa kuzama katika simu yake wakati mwenzi wake anamhitaji au anapenda kuzungumza naye ni dalili ya kutokujali na kutokuthamini. Kumbuka, kumpa mwenzi wako muda na kumsikiliza ni kuonyesha upendo kwake na namna ya kueleza kwamba unajali na kuthamini.

Unapoendelea kusoma makala hii, wewe uliye mwanandoa, tafadhali jiulize na kutafakari maswali haya: Je, una uhuru na simu ya mwenzi wako? Unaruhusiwa kuishika au kuitumia? Unaweza kupokea simu inapopigwa katika simu ya mwenzi wako pale anapokuwa hayuko karibu na simu yake?

Pia jiulize, je, ukipigiwa simu na mtu wa jinsia tofauti wakati ukiwa na mwenzi wako, unajisikia amani moyoni mwako kuongea mbele yake? Kati ya simu na mwenzi wako, kipi kimechukua nafasi kubwa zaidi kwako?

Kadhalika, je, una muda na mwenzi wako? Umewahi kugombana na mwenzi wako kwa sababu ya matumizi ya simu yako? Ulichukua hatua zipi? Je, kiwango cha mawasiliano na mwenzi wako kwa njia ya simu kimeongezeka au kimepungua? Unadhani kwa nini? Simu yako ina nywila (password)? Kama ndiyo, je, mkeo au mumeo anaijua nywila hiyo? Kama haijui, unadhani kwa nini? Maswali haya yakusaidie kujitathmini katika  matumizi ya simu yako/zako.

Mawasiliano ya simu yametajwa kuwa chanzo cha ndoa nyingi kuvunjika. Utafiti na uzoefu wangu katika mashauri ya ndoa vinaonyesha kuwa kukosekana kwa uaminifu na heshima miongoni mwa wanandoa imekuwa chanzo kikubwa cha matatizo katika ndoa nyingi.

Wanandoa wengi, kama ilivyo kwa watu wengine, hawafahamu maadili (etiquette) ya simu; kwani simu hizi za mkononi kwa bahati mbaya zilikuja na kuanza kutumika kabla ya watu kupata semina juu ya matumizi yake.

     Itaendelea Jumapili Ijayo

[Dk. Mlyuka ni mchungaji wa KKKT na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Marriage and Child Care Foundation (TaMCare), asasi inayojishuhulisha na masuala ya ndoa, familia na malezi. Kwa maelezo zaidi, tembelea www.tamcare.or.tz. Fuatilia mafunzo zaidi katika tamcaretv online. Kwa maoni na ushauri wasiliana naye kwa: info@tamcare.or.tz au +255744000066].