Chako ni chako…....

14Aug 2021
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Chako ni chako…....

“CHAKO ni chako cha mwingine sio chako.” Maana yake kitu unachokiita chako ni kizuri na huweza kukufaa tena una uhuru nacho kuliko cha mtu mwingine.

Twafunzwa tuvitegemee vitu vyetu wala sio vya watu wengine. Pia hutukumbusha kuvithamini vitu vyetu ingawa sio vizuri kama vya wengine. Sizungumzii vitu bali nazungumzia watu, hasa wacheza kandanda/kabumbu wetu wa Tanzania.

“Bura yangu sibadili na rehani (debwani).” Maana yake kitamba changu duni (bura) sibadili na kingine cha thamani kubwa (rehani) methali hii yatufuza tutosheke na vitu vyetu kwa kuwa vina faida kwetu kuliko vya watu wengine ambavyo haviwezi kutufaidi.Tusividharau vitu vyetu hata kama ni vibaya.

Wachezaji wanaoingia uwanjani kucheza kandanda huwa 11 mbali ya wachezaji wa akiba wanaokuwa nje ya dimba kusubiri jambo litakalomsibu mchezaji yeyote atakayepangwa mchezoni na atakayetolewa uwanjani ama kwa kuumia, kutolewa nje ya uwanja kwa kadi nyekundu au anayeshindwa kucheza kama atakavyo mwalimu.

Timu zinaruhusiwa kusajili wachezaji 10 wageni kutoka nje ya Tanzania. Kuna wakati timu zenye wachezaji wengi wa kigeni huchezesha wageni wapatao 7 ilhali wenyeji ni 4 tu! Hivi kweli Tanzania yenye zaidi ya watu milioni 54 na ushei (na ziada na zaidi kidogo) inakosa wachezaji hata ilazimike kuchukua wachezaji wengi kutoka nje ya nchi?

Twapaswa kutambua kuwa “Si kila mwenye kucha huwa samba.” Maana yake sio wanyama wote wenye makucha huwa simba. Methali hii huweza kutumiwa kwa mtu anayejidai kuwa na sifa au uwezo ambao hana.

Wallahi (kwa jina la Mwenyezi Mungu) wachezaji wageni wanaosajiliwa humu nchini na Simba na Yanga huwaambia wezao huko kwao, kuwa wachezaji wa kigeni wanalipwa mishahara mikubwa kuliko wanayolipwa huko kwao. Kwa hiyo huwa tayari wakati wote kujiunga na timu za nje hasa za Yanga, Simba na Azam FC, za Dar es Salaam. Naam, Bandari ya Salama!

Ni wangapi waliokuja Tanzania lakini wakashindwa na wenyeji kisha wakawekwa nje ya uwanja wakati wachezaji wenyeji wakicheza vizuri kuliko wageni walioletwa kwa mbwembwe na kulipwa mishahara mikubwa kuliko wachezaji wenyeji? Hali hiyo huwafanya wachezaji wetu kucheza kwa manung’uniko ya kimoyomoyo.

Kama Tanzania ina vijana wengi wenye uwezo wa kusakata gozi la ng’ombe, kwa nini Serikali isiwe na shule maalum ya vijana kujifunza kandanda ili timu zetu zinapotaka wachezaji ziwachukue kutoka huko na kupatiwa fedha wanazolipwa na timu zinazohitaji wachezaji kutoka huko?

“Mwenye busara mara hunasihika.” Maana yake mtu mwenye hekima huufuata ushauri apewao. Hutumiwa kutukumbusha umuhimu na faida za kuyafuata mashauri tunayopewa na wazazi wetu au na watu wanaotuzidi maarifa.

Kwa Simba na Yanga nawaambia: “Mchimba kisima huingia mwenyewe.” Maana yake mtu anayemchimbia mwingine shimo kwa dhamira mbaya huishia kuingia yeye mwenyewe.

Methali hii huweza kutumiwa kumshauri mtu anayemfanyia mwenzake ubaya, kuwa huenda ubaya huo ukamrudia yeye.
marobarnabas@yahoo.com
0784 334 096