Vipimo hivyo vimeondoa matumizi ya vile vya siku nyingi vilivyokuwa vikijulikana kitaalam kama BS.
Kwa kweli kuna tofauti kubwa sana katika utoaji majibu ya vipimo vyote hivyo, kwani MRDT inatoa majibu papo kwa hapo na na BS inatoa majibu baada ya muda fulani, tena kwa saa kadhaa.
Tangu kutambulishwa MRDT, kusema kweli hali za afya za wengi zimekuwa shakani, kwani licha ya kutambulishwa vipimo hivyo ni vya haraka kuepusha wananchi kunywa dawa bila ya kufanya vipimo, nadhani kasi ya unywaji dawa umeongezeka maradufu badala ya kupungua.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, katika foleni ya watu zaidi ya 10, wanaoingia kupima malaria huenda wote majibu yao hawakutwi na malaria, licha ya kufika hospitalini wakiwa na dalili zote za ugonjwa huo.
Hapo zamani ilikuwa mgonjwa akipimwa kwa kutumia BS, atapewa hadi idadi ya wadudu wa malaria waliopo kwenye damu.
Ni ukweli tunautaka urahisi, lakini pia ieleweke si kwenye afya za watu ambazo zinagharimu maisha yao.
Malalamiko ya vipimo vya MRDT hayapo tu kwa wagonjwa, lakini hata kwa wataalam wenyewe wa afya ambao serikali imezuia kuleta dawa za kuchanganyia wakati wa kutumia kile kipimo cha zamani, hivyo kulazimika kutumia vipimo vipya.
Wataalam wenyewe licha ya hofu ya kuongea hadharani, wasionekane wanabishana na serikali, moyoni hawana imani na vipimo hivyo vipya vya MRDT,
hali inayowafanya Watanzania kwenda moja kwa moja kwenye maduka ya dawa na kununua dawa za malaria, wanakunywa hata kama hospitalini, aliambiwa hana malaria.
Swali linalojitokeza ni kwamba, je ugonjwa wa malaria umepungua kwa kasi gani? Tunashuhudia mbu wanaozagaa majumbani usiku n.k.
Hilo ni swali tunalowaomba wataalam na watafiti walifanyie kazi, kabla ya athari tunayoihisi kuwa mabaya kwa afya za Watanzania.
Tuna kila sababu za kuiomba serikali itoe majibu ya kitaalam na inayoridhisha, ili kueleza takwimu halisi za malaria na walivyofanikiwa kuidhibiti kwa haraka kiasi ugonjwa huo.
Kwani tunapata dalili za kuugua na tunapoenda hospitalini, hatuonekani Watanzania tunateswa na ugonjwa gani.
Ni imani yetu kwamba mamlaka husika litaliangalia jambo hili kwa kina na kutupa majibu ya kuridhisha kwa maslahi ya Taifa letu.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








