Tangu aingie madarakani, Dk. Magufuli ameshafanya uamuzi mgumu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) mara mbili, baada ya kujionea uhalisia na kielelezo cha hospitali nyingine zilivyo.
Kwa mara ya mwisho alipokwenda kumjulia hali Sheikh Mkuu, Sheikh Abubakary Zubeiry bin Ally, msafara wake ukasimamishwa na wanawake na kumlazimu kutii ombi lao, kuitembelea wodi ya wazazi.
Tayari ameshachukua hatua kadhaa kukabiliana na sehemu ya kadhia zinazowakabili wajawazito hasa kuhusu kero ya kuchangia kitanda huku wengine wakilala chini.
Si vema kurejea kila jambo lililofanywa katika ziara hizo za Rais Magufuli kule Muhimbili, lakini kwa uhalisia wake, Kiongozi Mkuu huyo wa nchi anapaswa kutambua kuwa hali katika sekta ya afya, pamoja na umuhimu wake bado haijatengemaa.
Nimesema pamoja na umuhimu wake kwa maana pasipo na afya nzuri hakuna mwanadamu atakayepata nguvu za kumuwezesha kutekeleza majukumu yake.
Hata akiwa komandoo wa kijeshi aliyefuzu mafunzo yote, ama mhadhiri wa Chuo Kikuu mwenye taaluma ya juu kutoka pande tofauti za dunia au mwingine yeyote, kama hana afya nzuri hawezi akatimiza wajibu wake ipasavyo.
Kwa upande mwingine, taifa linawategemea watoto wa leo kuwa wajenzi wa taifa la kesho. Lakini hilo litafanikiwa ikiwa jitihada za dhati zitatekelezwa katika kulinda na kuwafanya wawe na afya nzuri.
Kiwango cha uzalishaji viwandani na utoaji huduma maofisini kitakuwa chenye ufanisi ikiwa watu watakuwa na afya bora.
Hiyo ni sawa na kusema afya ni mhimili na msingi wa utendaji wa mwanadamu. Ndio maana madaktari wapo, si kwa ajili ya walio wazima wa afya bali wagonjwa.
Sasa baada ya ziara zake ‘zilizozaa matunda’ kule Muhimbili, Rais Magufuli anapaswa kuyatafakari mazingira magumu aliyoyakuta, kwamba yapo kwenye hospitali ya Taifa iliyopo jijini Dar es Salaam.
Ajiulize na kutafakari, je, hali ikoje kwa hospitali za mikoa, wilaya, vituo vya afya na zahanati kwa kuwa huko kuna wananchi wengi hususani wasiokuwa na uwezo mzuri kiuchumi?
Kabla ya kuingia huko ni vizuri kuendelea kuijadili Muhimbili na namna inavyopaswa kutekeleza sera ya afya kwa maslahi ya umma mpana.
Kwa mfano sera ya afya inazungumzia watoto wa chini ya miaka mitano kupata huduma za afya pasipo malipo.
Suala hilo lipo kwa namna mbili ingawa zote zinahusu gharama kubwa wanazotozwa watoto; mosi ni kwa wanaotokea hospitali za umma na pili; wanaotokea zile za binafsi.
Kutokana na sababu ana vigezo walivyoviweka, MNH wanatoza fedha nyingi kwa wagonjwa wanaotoka hospitali za binafsi, wakiwamo watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.
Swali la kujiuliza, mtoto wa aina hiyo asiyejua sababu ya kufikishwa kwake MNH anaadhibiwa vipi kwa ukubwa wa gharama zinazolipwa na mzazi ama mlezi wake?
Kwa maana ni jambo lililo wazi kwamba hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati za umma zipo chache, tena kwenye maeneo ya mbali na walio wengi.
Mzazi ama mlezi anapotaka kuokoa maisha ya mtoto wa Kitanzania, hawezi kukiacha hospitali binafsi iliyopo jirani inayoweza kumpa rufaa ya kwenda Muhimbili, akatumia muda mrefu kufuata ya umma huku maisha ya mtoto yakiwa hatarini.
Hivi karibuni nimeshuhudia mtoto mwenye umri wa chini ya mwaka mmoja, aliyelazwa Muhimbili kwa siku nne akitokea hospitali moja maeneo ya Mbezi, akatozwa Shilingi, 620,000 za matibabu, vipimo na ziara za madaktari wodini!
Hivi ni maisha ya watoto wangapi yatapotea kutokana na wazazi ama walezi wao kushindwa kugharamia kiasi kama hicho ama kinachozidi?
Hata gharama ya Shilingi 30,000 kwa siku kwa mtoto anapolazwa wodini, haiwezi kuwa sababu ya mzazi ama mlezi asiyekuwa na uwezo, kutumia mbadala kama tiba asilia ama vidonge vya kupunguza maumivu ili mradi ‘siku ziende’?
Wanasiasa wanapoielezea hali ya huduma za afya na namna Tanzania inavyojidhatiti kuhakikisha inakuwa bora, uhalisia wake unazifanya kauli zao kuwa mfano wa mchezo wa kuigiza!
Ndio maana hata baada ya Rais Magufuli kuagiza ‘fedha za Bunge’ zitumike kununua vifaa Muhimbili, ikaenezwa hasa kupitia mitandao ya kijamii kwamba vitanda vimejaa hospitalini hapo hadi wagonjwa wanabadilisha vitanda kwa namna wanavyotaka.
Watu wasiofika Muhimbili wanaweza wakaamini hivyo. Lakini uhalisia wake haupo hivyo.
Kwenye wodi ya watoto pekee, watoto wanaofikia wanne wanalazwa kwenye kitanda kimoja na wengine wakilala sakafuni!
Yaani ni kama Rais Magufuli mwenyewe alivyoshuhudia alipofanya ziara ya ghafla kwenye wodi ya wazazi. Mkuu huyo wa nchi anastahili heshima inayomstahili.
Mfano wa pili ni tukio la Jumamosi iliyopita, fundi ujenzi mmoja alianguka kutoka juu wakati akiezeka nyumba, akaumia sehemu ya uti wa mgongo na kufikishwa kwenye Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) akitokea hospitali ya Amana.
Ninachelea kuyataja majina ya mtoto aliyelazwa na kutozwa takribani Shilingi 620,000 ama fundi huyo kwa vile sina ridhaa yao, ingawa vielelezo vyote vipo.
Licha ya kufikishwa MNH mapema, haikuwa rahisi kwake kupata kitanda. Alibaki `akiyasikilizia’ maumivu makali hadi alfajiri ya siku iliyofuata, ndipo akapelekwa wodini na kupata kitanda!
Lakini umma unaaminishwa kwamba hivi sasa hali ya huduma Muhimbili inaridhisha. Ni kweli inaridhisha tofauti na ilivyokuwa kabla ya utawala wa Rais Magufuli, lakini si kwa kiwango kinachoaminishwa kwa umma.
Rais Magufuli anapaswa kuutambua ukweli unaoweza kufichwa na wasiotaka kuonekana wameshindwakazi.
Kama afya za Watanzania akiwamo Rais wao zitadorora, hakuna uzalishaji na utendaji kazi utakaofanyika kwa ufanisi.
Kutokana na umuhimu wake, kila kinachopaswa kufanyika kinastahili kifanyike ili kufikia lengo la Watanzania kuwa na afya bora huku vifo hasa vya watoto na wajawazito vikidhibitiwa.
Mungu ibariki Tanzania.
Mashaka Mgeta ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana +255754691540,0716635612 ama barua pepe:mgeta2000@yahoo.com ama mashaka.mgeta@guardian.co.tz.
Mwisho.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








