Kubana matumizi ni sawa, tatizo lipo katika utekelezaji

19Jun 2022
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
Nawaza kwa Sauti
Kubana matumizi ni sawa, tatizo lipo katika utekelezaji

​​​​​​​BAJETI pendekezwa ya serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 imeshawasilishwa bungeni na sasa wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, wanaichambua na kushauri mambo mbalimbali ambayo yatamnufaisha mwananchi.

Pamoja na mambo mengine, bajeti hiyo imejikita katika kubana matumizi ya serikali kwa kupunguza idadi ya vigogo wanaotakiwa kununuliwa magari, kukopeshwa ili wafanye matengenezo wenyewe na kununua vipuri, lakini kupunguza gharama za mafuta.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, akiwasilisha mapendekezo hayo ya bajeti Juni 14, mwaka huu, alisema serikali ilibaini fedha nyingi inapotea kwenye kugharamia mafuta, vipuri na kila ofisa mwenye cheo cha kupewa gari kuwa na gari.

Alieleza mifano kuwa wakati mwingine wanakwenda kuhudhuria mkutano mmoja, lakini kila mmoja anasafiri kwa gari lake na dereva wakati wangeweza kutumia gari moja, jambo linaloendelea kuongeza gharama.

Alisema mabosi wengine wanasafiri kwenda mkoa fulani kwa ndege lakini gari linasafiri kwa barabara likiwa na dereva ambalo hutangulia siku moja au mbili kabla, jambo linaloendelea kuwabebesha Watanzania mzigo.

Pia, viongozi husafiri na kukusanyika kwenye mkutano kwa siku kadhaa au nusu siku, wakati wanaweza kufanya kwa kutumia mtandao kuliko kutumia gharama nyingi kwenda eneo la mkutano.

Eneo lingine aliloligusia ni ununuzi ambao umekuwa ukiigharimu serikali kwa kuwa mara nyingi haufanyiki kwa kuangalia bei za soko kwa wakati huo, bali muhusika huweka bei za juu kutokana na taratibu zenye urasimu ikiwamo kucheleweshewa malipo.

Jitihada za kubana matumizi hazijaanza kwenye bajeti hii, bali miongo mingi iliyopita. Kwenye kitabu chake cha 'Mzee Rukhsa, Safari ya Maisha Yangu', Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, anakiri kwamba alichukua hatua kama hizo mwaka wa fedha 1989/90 kwa kubana matumizi, akiwafuta kazi watumishi zaidi ya 300 wa ATC (sasa ATCL) na kufunga ofisi zao sita nje na ndani ya nchi.

Vilevile, wakati wa awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda, alielekeza kupunguza matumizi kwa viongozi kuacha kununua mashangingi na badala yake watumie magari ya kawaida ili kupunguza gharama.

Jambo hilo lilipata upinzani mkali kiasi cha kushindwa kutekelezwa na kuendelea kama awali kwa mashangingi ya mamilioni kununuliwa kila uchao, na kwa sasa ndiyo kuna magari ya kifahari zaidi wanayotembelea viongozi, ni ya kisasa ambayo hayana miaka mingi sokoni.

Mwananchi anaweza kujiuliza kwani wakitumia magari ya kifahari au hizo gharama zinanihusu? Kila Mtanzania anahusika kuchangia mshahara, posho na matumizi mengine ya viongozi au waajiriwa wote serikalini na mashirika ya umma.

Maumivu yapo kwa kuwa kila mmoja analipa kodi kupitia bidhaa na huduma mbalimbali, kodi ndiyo hukusanywa na kusaidia miradi ya maendeleo na ueneshaji wa serikali, lakini sehemu kubwa ya fedha ni kwenye matumizi ya mishahara na matumizi mengine.

Kwa sasa unakuja utaratibu wa kila Mtanzania mwenye miaka 18 na mwenye kipato kulipa kodi kulingana na miamala yake, na ndiyo maana umeandaliwa utaratibu wa kumiliki namba ya mlipakodi, ili iwe rahisi kulipa kokote ulipo, zote hizo zinakwenda kufanya maendeleo ya nchi.

Nia ya kiongozi anayeanzisha hilo kama alivyoeleza Waziri Mwigulu, ni njema kabsa, shida itakuwapo kwa watekelezaji ambao ndiyo wanufaika, kwamba sasa hawatafuatwa na madereva, lakini watajua uchungu wa kununua vipuri na kuweka mafuta kwenye magari.

Lazima kujifunza kwa wengine, nchi zilizoendelea viongozi wake wanagharamiwa kama wa nchi zetu hizi? Niliwahi kutembelea Bunge la Denmark, niliona baiskeli nyingi, niliuliza nikaambiwa baadhi ya mawaziri wanazitumia kwenda kazini.

Tunaweza kusema kwa mazingira ya miundombinu yao na hali ya hewa kuendesha baiskeli ni kawaida kwao, lakini kwa namna nyingine wanaona ni kawaida kabisa, nasi tunaweza kuwa na namna yetu ya kupunguza matumizi.

Ni juzi tu, Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, alieleza namna halmashauri zinavyogawana fedha za matumizi ya kawaifa, huku akitoa mfano wa mgawanyo ulivyofanyika kwenye Halmashauri ya Arusha.

Alishauri fedha za matumizi ya kawaida zisiachwe wao kuamua bali matumizi halisi yaangaliwe, ili zinazobakia zikajenge miundombinu ya barabara na maji ambayo inanufaisha wengi zaidi.