haziwezi kufikiwa na timu yoyote ile.
Wanachama na mashabiki wa Yanga waliusubiri ubingwa huo kwa misimu minne ambapo ni kama ulikuwa umehamia kwa watani zao wa jadi, Simba.
Baada ya dhiki faraja, unaweza kusema hivyo, kwani ilipitia kipindi kigumu, lakini viongozi, wanachama na mashabiki walikuwa wavumilivu na kupambana kuhakikisha wanairudisha timu kwenye hali ya ushindani.
Walichofanya kabla ya msimu huu ni kusajili kikosi ambacho kimekuja si tu kuleta ushindani kwenye Ligi Kuu bali kuwa tishio.
Hadi kinachukuwa ubingwa bado hakikuwa kimepoteza mechi yoyote ile na mpaka sasa timu hiyo imesalia mechi tatu ili iweze kuweka rekodi ya kucheza msimu mzima bila kupoteza.
Pamoja na kufanya usajili wa wachezaji wengi, lakini ulioweza kuwafanya kuwa tishio na kuwapa ubingwa ni wa kipa Djigui Diarra wa Mali, Yannick Bangala, Mayele, Djuma Shaaban na Jesus Moloko kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Khalid Aucho kutoka Uganda.
Kwa hakika wachezaji hawa wakichanganyika na wengine waliowakuta na wachache waliosajiliwa kutoka klabu mbalimbali hapa nchini ndiyo kwa kiasi kikubwa waliofanya Yanga kuwa timu isiyoshindika.
Nitoe pongezi kwa viongozi, wanachama na mashabiki wa timu hiyo ambao kwa pamoja wameiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa msimu huu, ikiwa ni mara ya 28 tangu kuanza kucheza ligi nchini Tanzania mwaka 1965.
Hata hivyo, ukweli lazima usemwe kuwa pamoja na kwamba Yanga ndiyo timu iliyotwaa ubingwa mara nyingi nchini Tanzania, lakini rekodi yake kwenye michuano ya kimataifa hairidhishi hata kidogo.
Imekuwa ikijitutumua mara kadhaa, lakini imekuwa ikiangukia pua, wakati mwingine mechi za awali, raundi ya kwanza au ya pili.
Ina rekodi nzuri ya kuwa ndiyo timu ya kwanza kuingia hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998, lakini hata hivyo haikushinda mechi yoyote.
Hapa nazungumzia michuano ambayo inakwenda kushiriki ya Ligi ya Mabingwa na si Kombe la Shirikisho.
Ni miaka 24 sasa Yanga haijaweza kutinga tena hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya kuwa kuna wakati ilikuwa na kikosi madhubuti ambacho kilitakiwa kiwe kimeingia kwenye hatua hiyo.
Achana na kikosi cha kina Bernard Mwalala, au Boniface Ambani na wala sitaki kuizungumzia Yanga bora kabisa kuwahi kutokea Tanzania ya miaka ya 1980, ngoja tukizungumzie kikosi cha mwaka 2014 mpaka 2015.
Nadhani Yanga ilikuwa na kikosi bora zaidi naweza kusema kuliko hiki, lakini hakikuweza kutinga hatua hiyo, hivyo hapo viongozi wanaweza kuanzia, waangalie tatizo lilikuwa nini ili waanze kuliangalia na kulirekebisha mapema.
Kuna wakati kikosi cha Yanga kiliundwa na Deogratius Munishi 'Dida', Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, Mrisho Ngassa, Hamisi Kiiza, Juma Abdul, David Luhende, Athumani Idd 'Chuji', Hassan Dilunga, Said Bahanuzi, Didier Kavumbavu na wengine.
Hebu pata picha, kikosi kama hiki bado kilishindwa kutinga hatua japo ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa misimu miwili mpaka mitatu hadi kilipoanza kupanguka tena. Hapa kuna tatizo.
Ina maana viongozi wa Yanga hawakukaa tena vizuri na akili yao kuelekeza kwenye michuano ya kimataifa, hata kikosi hiki kinaweza kutolewa.
Hapa inaonyesha tatizo halipo kwenye timu, bali viongozi. Labda kwa sasa ambapo uongozi unakwenda kubadilika.
Ni aibu kwa zama hizi kwa timu za Simba na Yanga kuwekeza nguvu kubwa kwenye kutwaa ubingwa wa bara, huku zikishindwa kutinga hata hatua ya makundi. Kwa sasa naona Simba imeanza kujipambanua.
Simba na Yanga ni timu za zamani sana na zimechelewa sana kujua kimataifa ndiko kunalipa.
Kinachotakiwa sasa Yanga ni kuacha kuchukua muda mrefu kusherehekea ubingwa kwani hiyo kwake si mara ya kwanza, bali kujiandaa sasa na michuano ya kimataifa ambayo kwake imekuwa mwiba mchungu.
Tuliona msimu uliopita timu hasimu za Sudan, Al Hilal na El Merreikh zikiwa kundi moja kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hivyo ndiyo Watanzania wengi wanahitaji na si miaka nenda rudi kupigiana kelele humu humu ndani na kuzifunga timu dhaifu, wakati mwingine kwa msaada wa makocha na waamuzi.
Tunataka kuziona Simba na Yanga zote zikitinga makundi Ligi ya Mabingwa msimu ujao kwa kuziandaa timu zao kikamilifu na viongozi hasa wa Yanga kuwa na dhamira ya dhati kwenye michuano hiyo.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








