Mechi hiyo ilikuwa ya marudiano baada ya ile ya awali wiki mbili zilizopita nchini Morocco, Simba kukubali kichapo cha mabao 2-0, hivyo kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi nne sawa na USGN ya Niger huku RS Berkane ikivuna alama sita kileleni na Asec Mimosas ikiburuza mkia kwa pointi zake tatu.
Hivyo, matokeo ya jana kwa timu hizo nne yalitarajiwa kubadili msimamo mzima wa kundi hilo ambalo linaelezwa kuwa gumu zaidi kuliko makundi mengine kwenye michuano hiyo ya pili kwa utajiri barani Afrika baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa.
Kwa ujumla kila mwenye nia njema ya kuona soka la Tanzania linapiga hatua na nchi kutangazika kimataifa kimichezo, hana budi kuendelea kuitakia mema Simba kusonga mbele katika michuano hii.
Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba, hakuna njia ya mkato kwa Tanzania kuingiza timu nne kwenye michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu msimu ujao; mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho Afrika, kama Simba hatafanikiwa kufuzu robo fainali na kuendelea mbele zaidi.
Ikumbukwe hadi sasa imebaki nafasi moja tu kwa nchi ambazo zinawania kuwa miongoni mwa mataifa 12 yatakayopata tiketi ya kuingiza timu 12 katika michuano hiyo msimu ujao, hivyo njia pekee ya kwa Tanzania kukata tiketi hiyo ni Simba kufika mbali katika michuano hii.
Lakini mbali na Tanzania inayowania nafasi hiyo kwa karibu, kuna Libya ambayo ina timu mbili zinazoiwakilisha kwenye michuano hiyo, hivyo ina nafasi kubwa ya kukata tiketi hiyo, endapo tu Simba haitatinga robo fainali na timu zao kufika hatua hiyo na zaidi.
Hata hivyo, wakati tulitarajia kuona wadau wa soka nchini na, mashabiki na Watanzania kwa ujumla wakiungana kuwa kitu kimoja katika kuisapoti Simba ili kupigania nafasi hizo nne, wapo baadhi ambao wanajifanya kujitoa ufahamu kwa kutoona umuhimu huo na wanachotaka ni kuwashusha wawakilishi wetu hao kimataifa ili warejee walipo wao.
Ndiyo, tunasema hivyo hasa baada ya kushuhudia baadhi ya mashabiki wapinzani wa ndani wa Klabu ya Simba jana wakiishangilia RS Berkane kama ilivyokuwa Ijumaa iliyopita walipojitokeza kwa wingi kwenda kuipokea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere huku wakieleza dhamira yao ya kuwaona wawakikilishi wa Tanzania wakiishia hatua hiyo ya makundi.
Si hilo tu, lakini wapo baadhi tena viongozi wakuaminika katika mchezo uliopita ambao Simba ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Asec Mimosas katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, walithubutu kutoa kauli za kipuuzi eti wakiwataka wapinzani hao wa Simba kuwa makini katika vyumba vya kubadilishia kutokunywa maji ya wenyeji wao uwanjani.
Sisi tunasema huu ni ushabiki uchwara na ulimbukeni uliopitiliza kwani kwa kauli kama hizo huziichafui Simba pekee bali Tanzania kwa ujumla, hivyo hatuna budi kila mmoja kwa nafasi yake kuzikemea kwa nguvu zote huku tukiimiza umoja na mshikamano katika kuwasapoti wawakilishi wetu wa nchi kimataifa.
Tanzania ni nchi ya amani na salama kwa wageni na wenyeji, lakini tunaamini Klabu ya Simba ina viongozi weledi na makini ambao wamewahi kushika nyadhifa kubwa serikalini, hivyo hawawezi kushiriki kwa namana yoyote ile katika kuchafua sifa ya taifa eti kwa sababu tu ya mpira.
Hivyo, Nipashe tukiwa wadau namba moja wa soka na michezo kwa ujumla, tunapenda kuona nguvu kubwa inayotumiwa na wapinzani wa ndani wa Simba kisoka katika kutaka kuishusha hapo ilipo, ikielekezwe katika kuziinua klabu zao na zingine ili misimu ijayo tuwe na wawakilishi wengi kimataifa katika hatua hii ya makundi, robo fainali, nusu na hatimaye fainali na ikiwezekana kubeba ubingwa wa michuano hiyo miwili mikubwa Afrika.
Kwetu sisi tunaendelea kushikilia msimamo wetu wa kuziunga mkono klabu zote zinazoiwakilisha nchi kimataifa kwa kuwa yoyote ile itakayopata mafanikio ni Tanzania imeshinda.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








