Jamani tuwe na subira, kukamilika miradi hii itaipa tija uchumi wetu

07Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Jamani tuwe na subira, kukamilika miradi hii itaipa tija uchumi wetu

DHANA ya ukuaji uchumi inaweza kuzua kitendawili kwa viongozi wa serikali na hata wananchi wa chini, ndani ya lengo lake la kutaka maendeleo katika taifa.

Nikitazama miradi ya kimkakati inayofanywa na serikali naona ina tija kubwa kitaifa, huku ikisadikika kukuza uchumi wa taifa, kuzalisha ajira na kupunguza madeni tunayodaiwa.

Nchi yetu Tanzania ilibahatika kupandishwa daraja la kufikia uchumi wa kati, mwaka 2020 na Benki ya Dunia. Ni wazi kuwa nchi nyingi duniani zilitetereka kiuchumi wakati wa janga la virusi vya corona, ambavyo bado ni tishio duniani katika wimbi hili la sita.

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan, ameshuhudia hafla ya utiaji saini mkataba wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Makutupora - Tabora, kinachotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh. trilioni nne.

Katika hafla hiyo, Rais Samia alieleza umuhimu wa kukamilisha miradi hiyo katika kukuza uchumi wa taifa letu.

"Mimi nipo pamoja nanyi, tutaangalia mikopo inayotufaa, tukiongozwa na Gavana wa Benki Kuu (BOT) na waziri yupo hapa, tutachukua tumalize reli kama tulivyopanga ili ifanye kazi, itengeneze fedha tuweze kulipa mikopo tunayoichukua," alitamka.

Kukamilika miradi hiyo kunaonyesha taswira halisi ya kuja kuzalisha ajira kwa vijana, pia kuongeza pato nchini hasa katika ulipaji kodi. Nchi yetu ina miradi mingi inayopaswa kukamilika na bado serikali inajitahidi kuhakikisha inakamilisha miradi hiyo.

Wakati ambao Watanzania tunapaswa kuwa wamoja ni huu, kwa kushikamana na Rais Samia katika kutekeleza shughuli za maendeleo ya nchi yetu.

Haya nayathibitisha pale Rais aliposema katika miradi hii ya kimkakati, wapo baadhi ya watu waliokuwa wanasubiri kuona miradi hiyo inakwama, ili wapate la kuzungumza, lakini Rais alisisitiza hakuna utakaokwama.

Alitamka: "Kuna mradi wa Bwawa la Nyerere, Daraja la Busisi, sijui miradi ya barabara, sijui reli na mingine yote, hakuna hata mmoja ambao tunadaiwa pesa, makandarasi wameshalipwa yote, sisi ndio tumebaki tunadai kazi".

Kauli ya Wahenga ya ‘umoja ni nguvu Utengano ni udhaifu’ tunapaswa kuishi nayo Watanzania katika kuhakikisha lengo letu la kukamilisha miradi hii linafikia suluhisho bora.

Mradi huu wa SGR utakuwa na faida lukuki si kwa Tanzania pekee hata katika maendeleo ya Afrika. Wakati Rais Samia alipoweka jiwe la msingi la ujenzi huu kutoka Mwanza hadi Isaka mwezi Juni mwaka huu, alieleza moja ya umuhimu wa miradi huu.

“Moja ya mambo yanayotajwa kukwamisha kasi ya maendeleo Afrika ni kutokuwapo miundombinu imara ya usafiri. Utafiti unaonyesha kuwa ukosefu na ubovu wa miundombinu sio tu unachelewesha usafirishaji wa watu na bidhaa, bali unaongeza gharama za bidhaa kwa asilimia 40,” alisema Rais Samia.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa, anasema ujenzi kutoka Mwanza kwenda Isaka utawazalishia Watanzania ajira zaidi ya 86,000.

Ni faida lukuki kukamilika kwa miradi yote ya kimkakati kutawezesha kupunguza gharama na usumbufu kwa wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi na kulazimika kusafiri hadi mkoani Dar es Salaam kupokea mizigo yao.

Tukiishi na imani kwa viongozi wetu wa serikali, tukishikamana wananchi kwa umoja, tutaweza kufanikisha zoezi letu la kufikia malengo ya maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania.