Tunaelezwa kwamba, hadi kufikia Desemba 18, mwaka jana, ambayo ni wiki mbili na nusu iliyopita, kuna watu milioni 1.27 waliokwishapata chanjo kamili ya kujikinga na ugonjwa huo.
Katika jitihada za kuhakikisha Watanzania wanapata huduma hiyo, mikoa mitano inatajwa kuongoza kwa kufanya vizuri kwa utoaji chanjo hiyo, ambayo ni Mwanza, Ruvuma, Mara, Kagera na Dodoma.
Inapoenda kinyume chake, ni kwamba wananchi wa mikoa mingine mitano ya Manyara, Songwe, Njombe, Singida na Iringa wanadaiwa kufanya vibaya katika utoaji chanjo hiyo.
Tanzania Bara ina mikoa 26 ambayo mikoa 10 kati ya hiyo, taarifa zake zimejulikana kuhusu jinsi inavyotoa chanjo, lakini bado kuna mingine 16 ambayo wizara yenye dhamana ya afya za Watanzania haikutajwa
Pamoja na hayo, ni wazi kwamba kuna haja kwa mikoa 21 ikiwamo inayodaiwa kufanya vibaya, inajifunza kitu kutoka mitano ambayo wizara inaitaja kuwa imefanya vizuri katika utoaji chanjo.
Kujifunza kutoka kwa wengine, kunaweza kugeuza makosa kuwa mafanikio. Hivyo, si vibaya mikoa ambayo bado inasuasua katika chanjo, inajifunza kutoka zile ambazo zimepiga hatua katika utoaji chanjo hiyo.
Ikumbukwe, ili kuwa mshindi ni muhimu kujifunza kutokana na makosa, kwani bila ya kufanya hivyo, mtu anaweza kujikuta akiendelea kukosea tu au kushindwa kupiga hatua kwenda mbele.
Mikoa kusuasua katika utoaji chanjo, ni wazi kuna sababu mbalimbali zinazochangia kusaidia kujirekebisha, hasa kujifunza kwa mikoa, ambayo imepiga hatua ili kujua mbinu zilizotumika.
Kama kuna jambo watu hawalipendi, jamii kuambiwa wamekosea. Wengi wanatamani waishi bila ya kufanya makosa, lakini hilo haliwezekani. Ndiyo maana, kuna suala la kujifunza kutokana na makosa.
Ndani ya mazingira ya duniani, hakuna namna ambayo mtu anaweza kuishi bila ya kufanya makosa. Watu wanakosea kila siku inayoenda kwa Mungu, wakijua hata wakati mwingine kwa kutojua wamekosea.
Hivyo, umuhimu wa kujifunza kutokana na makosa una uzito wake, hata kwenye suala la chanjo, inamaanisha kwamba mikoa iliyoko nyuma katika utoaji chanjo, ijifunze mahali ilikokosea, ili zichukue hatua za kujirekebisha.
Taarifa za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, zinaonyesha tangu chanjo ya UVIKO-19 ilipozinduliwa mwishoni mwa Julai hadi kufikia Desemba 18, mwaka jana, kuna watu milioni 1.27 waliokwishapata chanjo hiyo.
Wizara pia imesema, kuwa taarifa potofu kuhusu chanjo hiyo inachangia baadhi ya watu kukana kuchanjwa. Hivyo, ni vyema viongozi wa mikoa wakaliona hilo linakwamisha chanjo katika maeneo yao, walifanyie kazi.
Hatua hiyo ya kuangalia vikwazo vya chanjo, ingeenda sambamba na kuhimiza watu kuzingatia mwongozo wa kudhibiti ugonjwa huo, kwani wengine wanaonekana kutochukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa Uviko - 19.
Mwongozo wa sasa unataka watu waepuke hali ya mikusanyiko isiyo ya lazima, pia kunahitajika watu wavae barakoa, kunawa maji tiririka na kutumia vitakasa mikono na penye usafiri abiria wa umma, idadi ya abiria ifanane na viti kwenye basi.
Ukweli ni kwamba, penye baadhi ya maeneo, ni kama watu hawana habari na ugonjwa huo hawachukui hatua za kujikinga, hali inayokaribisha ujio wa UVIKO -19 kuendelea kuwapo nchini.
Iwapo watu hawatazingatia mwongozo huo, ni wazi watashindwa kujitokeza kupata chanjo. Hivyo, si vibaya viongozi wa mikoa iliyo nyuma katika chanjo, wakaenda kujifunza kwa wenzao ambao mikoa yao iinaoongoza.
Wizara yenye dhamana na afya inatukumbusha kuwa, hali ya maambukizi ya UVIKO imeongezeka, jambo ambalo si ishara nzuri kijamii. Watanzania wanatakiwa kuchukua tahadhari zinazoelekezwa na wataalamu wa afya, ili wabaki salama dhidi ya ugonjwa huo.
Ni katika uthibitisho sasa, wizara hiyo inasema idadi ya sampuli nyingi zinazopokewa katika Maabara Kuu ya Taifa, zimekuwa zikiongezeka kutoka siku 14 hadi kufikia 47, hali inayoashiria ongezeko la maambukizi hayo.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







