Mbeya City ya sasa, ni Mwasapili

12Jun 2016
Lasteck Alfred
Lete Raha
Mbeya City ya sasa, ni Mwasapili

BAADA ya kuisha kwa Ligi Kuu Tanzania Bara 2015/16 huku Mbeya City ikimaliza kwenye nafasi ya nane kwa kuwa pointi 35, nahodha wa timu hiyo, beki Hassan Mwasapili ameandika rekodi ya kipekee kwenye kikosi hicho kwa kucheza kwa dakika nyingi zaidi kuliko wachezaji wengine.

Hassan Mwasapili

Pia takwimu mbalimbali ilizonazo gazeti hili zinaonesha kuwa beki huyo wa pembeni amewafunika mabeki wengi akiwamo beki kisiki wa Azam, Pascal Wawa, ambaye alikuwa akitaja kati ya mabeki waliocheza mechi nyingi zaidi msimu huu.

Mwasapili alivyocheza

Mwasapili aliyewahi kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars) wakati timu hiyo ilipokuwa chini ya kocha Mdernmark, Kim Paulsen, alifanikiwa kucheza kwa kiwango cha juu kwa dakika 2,520 hii ikiwa ni sawa na mechi 28 za timu yake katika msimu uliomalizika hivi karibuni huku akikosa mechi mbili tu.

Beki huyo alikosa mchezo dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga uliochezwa kwenye Uwanja wa Mwadui Complex kufuatia kufungiwa kutokana na kadi tatu za njano alizoonyeshwa.

Pia alikosa mechi ya mwisho dhidi ya Ndanda FC iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kutokana na kusumbuliwa na majeraha aliyopata wakati akiwa mazoezini.

Dakika 2,520

Kwa dakika 2,520 alizocheza beki huyo msimu huu ni wazi kuwa amemzidi kwa dakika 360 zaidi beki Muivory Coast wa Azam, Pascal Wawa, ambaye amekuwa akitajwa kuwa kati ya beki tishio kwenye Ligi Kuu kwa msimu huu.

Wawa alicheza dakika 2,160 huku akiisaidia Azam kumaliza kwenye nafasi ya pili ya ligi ikiwa na pointi 64. Kwa upande wa Azam, takwimu zinaonesha kuwa Wawa ni mchezaji wa pili kwa kucheza mechi nyingi zaidi kwenye kikosi hicho huku nafasi ya kwanza ikishikwa na kipa Aishi Manula aliyecheza dakika 2,640.

Rekodi ya Mwasapili inakuja baada ya kucheza mechi 28 na kukosa mbili huku akiifungia timu hiyo mabao mawili.

Kombe la Shirikisho

Beki huyo alicheza dakika nyingine 180 za Kombe la Shirikisho la Shirikisho la Soka nchini (TFF) ambayo City ilicheza dhidi ya Wenda FC na baadaye dhidi ya Tanzania Prisons.

Uongozi unasemaje?

Meneja wa City, Geoffrey Katepa alisema, "Mwasapili ni moja kati ya wachezaji wetu waliocheza vizuri msimu huu, alikosa mechi mbili tu katika msimu mzima huku mechi zote akicheza kwa kiwango bora, binafsi nampongeza na mambo yakienda vizuri kuna zawadi maalumu ambayo uongozi umepanga kumpatia kwa kufanya kazi vizuri.”

Kaseja aongoza kufungwa

Rekodi zinaonyesha kuwa, magolikipa watatu wa kikosi cha kwanza, Juma Kaseja, Haningtony Kalyesubula na Geoffrey Mwalyego, waliokuwa wakisimama langoni kwa kupishana kwenye michezo tofauti wamewajibika tofauti huku Kaseja akicheza mechi nyingi na kufungwa mabao mengi zaidi.

Katika rekodi hizo zinaonyesha, Juma Kaseja alicheza mechi 17 na kuruhusu kufungwa mabao 20, Haningtony Kalyesubula alicheza mechi 13 na kufungwa mabao 14 wakati Geoffrey Mwalyego yeye hakupata nafasi ya kucheza mechi hata moja.

Shamte afunika kwa kadi

Mlinzi wa kati wa timu hiyo, Haruna Shamte, alimaliza msimu akiwa na rekodi ya kupata kadi nyingi zaidi kuliko mchezaji yeyote wa kikosi hicho akiwa na jumla ya kadi nane ambapo kati ya hizo, sita ni za njano na mbili nyekundu.

Kiungo awa mfungaji bora

Kiungo Rafael Alpha ndiye aliyeibuka kinara wa mabao kwenye kikosi cha Mbeya City akimaliza msimu kwa kufunga mabao sita huku akiadhibiwa kwa kadi mbili za njano.

Kiungo miaka 17 aandika historia

Tangu City ilipopanda daraja msimu wa 2013/14, kiraka kinda wa timu hiyo, Aboubakary Shaaban amekuwa mchezaji wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi kuichezea timu hiyo kwenye mechi ya Ligi Kuu. Kinda huyo alicheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Coastal Union ya Tanga akiwa na umri wa miaka 17 na siku 129.