Samatta ampa Mao dili la Ulaya

03Feb 2016
Lete Raha
Samatta ampa Mao dili la Ulaya

IMEFAHAMIKA kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta, amempa mchongo kiungo wa Azam, Himid Mao, ili akacheze Ulaya.

Samatta amemuunganisha na meneja wake Jamal Kisongo na meneja huyo akamuunganisha na wakala wa Ufaransa aitwaye Herve Faisal. Kisongo alisema, “Wakala ambaye ninashirikiana naye kumsimamia Samatta ameniambia kuwa Samatta alimpendekeza Himid Mao kwaajili ya kucheza Ulaya na hii imekuja baada ya wakala huyo kuwa na moja ya timu inayomuhitaji awaletee kiungo mkabaji. “Samatta amekuwa na moyo na alipoulizwa juu ya Mtanzania anayeweza kucheza vizuri kama kiungo mkabaji alimtaja Mao kutokana na jinsi anavyofanya vyema kwasasa akiwa na Azam pamoja na timu ya taifa. Naamini fursa hiyo itamfaa kwa kuwa ana uwezo mzuri na anaweza kupambana,” alisema. Hivi sasa Mao yuko na klabu yake nchini Zambia walikoenda kwa mwaliko wa kushiriki michuano maalumu ya klabu. Kumbe Samatta alimuiga Mgosi Pia imefahamika kuwa nahodha huyo mpya wa Stars, asingefika klabu ya Genk ya Ubelgiji kama si kuiga uhodari wa nahodha wa Simba, Musa Hassan ‘Mgosi’, katika miaka ya 2006 hadi 2010 wakati mkongwe huyo akitamba Simba. Kama si Samatta kuwa na ndoto za kuwa kama Mgosi au kuwa kama straika wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry, pengine leo asingefika alipofika sasa. Unajua kwanini? Kaka wa Mbwana, Mohammed Samatta, amefichua kuwa tangu enzi za utotoni walipokuwa wakicheza soka la mtaani maarufu kwa jina la ‘chandimu’, Samatta alikuwa akivutiwa sana na uwezo wa Mgosi ambaye kwa wakati huo alikuwa akiwika na Simba. Mohamed alisema, “ulikuwa humwambii kitu Samatta juu ya Mgosi. Alikuwa akimpenda sana na alikuwa akimfungia safari kwenda kumuona akicheza, wakati mwingine alitoroka bila kuaga, lakini hiyo yote ilitokana na jinsi alivyomkubali. “Wakati mwingine akiwa anacheza, akifunga bao hujidai amefunga kama Mgosi,” alisema Mohamed huku akisema ‘straika’ huyo mpya wa Genk, wakati mwingine alikuwa akimkubali straika wa zamani wa Arsenal, Henry. Licha ya kuwa nahodha wa Simba, Mgosi mbali na kujikusanyia umaarufu mkubwa kati ya mwaka 2006 hadi 2010, kwa sasa amepoteza ubora wake aliokuwa nao na kwa mtazamo wa kawaida ni vigumu leo hii kuamini kuwa Samatta alikuwa na ndoto za kuwa kama Mgosi.