Samatta kuingoza Stars dhidi ya Misri leo

04Jun 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Samatta kuingoza Stars dhidi ya Misri leo
  • ***Ushindi pekee ndiyo utaifanya timu hiyo kuwa na matumaini ya kufuzu fainali za Afrika kabla ya mechi ya mwisho dhidi ya Nigeria itakayofanyika Septemba

TAIFA Stars, leo inaikabili Misri katika mechi muhimu ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Gabon, huku mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta akivaa kitambaa cha unahodha kwa mara ya kwanza tangu apewe nafasi hiyo.

SAMATTA

Samatta, anayecheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji, atawaongoza wachezaji wenzake dhidi ya Misri inayoundwa na wachezaji kadhaa wanaocheza soka Ulaya.

Mara ya mwisho kwa Taifa Stars kucheza michuano hiyo mikubwa Afrika ikiwa chini ya nahodha na Rais wa zamani wa TFF, Leodegar Tenga, ilikuwa mwaka 1980 nchini Nigeria na kuondolewa katika raundi ya kwanza.

Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, ina taswira ya kisasi hasa baada ya Stars kunyukwa mabao 3-0 na Wamisri hao katika mchezo wa kwanza mwaka mmoja uliopita.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Samatta alisema wamejipanga vizuri kushinda mchezo huo.
"Tupo tayari kuwakabili Misri, tunaamini tunaweza kupata matokeo mazuri kwenye uwanja wetu," alisema Samatta.

Ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele, Stars italazimika kushinda mechi ya leo kwa idadi kubwa ya mabao, kadhalika kuifunga Nigeria katika mechi ya marudiano ugenini, na kinyume na matakwa hayo, basi hesabu za safari ya Stars kwenda Gabon zitakuwa zimefika tamati.

Kocha wa Stars, Boniface Mkwasa alisema jana kuwa watalazimika kushinda mchezo huo na kisha kujipanga kwa mchezo wa marudiano.

"Kwanza tushinde kesho (leo) ndio tuangalie mengine. Tuna uwezo wa kushinda kwa sababu tumefanya maandalizi mazuri na wachezaji wapo kwenye hali nzuri," alisema Mkwasa.

Kama Misri watashinda mchezo wa leo, basi moja kwa moja watakuwa wamekata tiketi ya kucheza fainali hizo mwakani, kwani itakuwa imefikisha pointi 10 ambazo haziwezi kufikiwa na Nigeria na Tanzania.