Hiyo inafuatia Yanga kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrikana Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 3-2,baada ya kufungwa 2-1 Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora, ikitoka kulazimishwa sare ya 1-1 Uwanja wa Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.
Hii inakuwa mara ya pili kwa Yanga kuangukia kwenye nafasi hii na kwa ujumla hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kuingia kwenye mchujo huo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo midogo ya klabu Afrika.
Mwaka 2007 Yanga ilifungwa 3-0 na Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutoa sare ya 0-0 mjini Mwanza, hivyo kucheza na El Merreikh ya Sudan na kutoa sare ya 0-0 pia Mwanza kabla ya kufungwa 2-0 Khartoum na kutolewa.
Mwaka 2011 Simba ilitolewa na DC Motema Pembe ya DRC kwa jumla ya mabao 2-1, ikifungwa 2-0 ugenini na kushinda 1-0 nyumbani.
Na Simba iliangukia huko baada ya kufungwa 3-0 na Wydad Casablanca ya Morocco mjini Cairo, Misri katika mechi maalum ya mkondo mmoja.
Hiyo ilifuatia TP Mazembe iliyoitoa Simba katika Raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 6-3, ikiifunga 3-1 Lubumbashi na 3-2 Dar es Salaam katika Raundi ya Kwanza na baadaye kuitoa Wydad katika Raundi ya Pili kuondolewa mashindanoni na CAF kwa kosa la kumtumia beki Janvier Besala Bokungu, aliyevunja mkataba kinyume cha taratibu na klabu ya Esperance ya Tunisia.
Kwa kuwa Simba ndiyo waliyoikatia rufaa Mazembe baada ya kutolewa tu, CAF ikaamua timuhiyo zicheza na Wydad iliyotolewa pia na Mazembe katika hatua iliyofuata.
Baada ya Yanga kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho, inaonekana kama wanajiona tayari wamekwishafuzu hatua ya makundi, wakati ukweli ni kwamba ni wanaingia kwenye kuwania hatua hiyo.
Yanga wanaonekana kuidharau timu ya Angola na hesabu zao zimeanza kufikiria hatua ya makundi, jambo ambalo ni kosa. Hadi kufikia kwenye hatua hii, maana yake Sagrada Esperanca imewatoa wapinzani wake wote katika hatua za mwanzoni.
Na timu hiyo ilianzia kwenye Raundi ya Awali, ambako Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani, kabla ya kuitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 2-1 ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na kwenda hatua ya 16 Bora, ambako imeitoaV.Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 ikishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.
Kwa rekodi hizi, hii si timu ya kubeza, ikitoka kushinda nyumbani na ugenini katika hatua ya 16 Bora, maana yake Yanga wanakutana na wapinzani wagumu.
Ndiyo maana leo Lete Raha tunawaambia Yanga kabla ya kuanza kufikiria hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, wajipange kwa mchezo wa mtoano wa kuwania nafasi hiyo dhidi ya Sagrada Esperanca.










