taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zimesema mvua kubwa zaidi za kimbunga zinatarajiwa kuanza leo hadi mwisho wa mwezi huu.
TMA imesema mvua hizo zitasababishwa na kimbunga kiitwacho Fantala ambacho kwa sasa kimeonekana katika bahari ya Hindi kikienda kwa mwendo wa pole pole.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi alithibitisha kuwa kuanzia leo hali ya mvua itaendelea kuongezeka katika maeneo mengi nchini hususan maeneo ya Ziwa Viktoria a maeneo ya Magharibi.
Huu ni msimu wa mvua za masika, na kwa ujio wa mvua ya kimbunga cha upepo wa Fantala, ni dhahiri kuwa madhara yatakayosababishwa na mvua hizo yanaweza kuwa makubwa kuliko hata athari ambazo tayari zimewakumba wananchi wengi katika mikoa mingi.
Dk. Kijazi alifafanua kuwa tatizo kubwa la kimbunga hicho ni mgandamizo mdogo wa hewa unaoweza kuvuta upepo kutoka maeneo mbalimbali kwenda sehemu ambazo kimbunga kipo.
Tunaamini kuwa wananchi wengi sasa wanaelewa athari za mvua kubwa katika maeneo ya makazi, na kwa bahati nzuri Serikali pia imekuwa ikichukua hatua kila wakati za kuwakumbusha kuhama maeneo hatarishi yanayoweza kusababisha mafuriko.
Wapo wananchi wengi katika maeneo mbalimbali nchini ambao hadi sasa wanaishi katika makazi ya muda ikiwa ni pamoja na ndani ya mahema, maeneo mengine ya wazi, katika majengo ya shule na hata katika hifadhi za majengo yasiyotumika rasmi, wananchi waliookolewa kutoka maeneo yaliyoathiriwa na mvua kubwa.
Mafuriko yanayosababishwa na mvua za upepo mkali huwa na athari kubwa na mbaya kwa maisha ya watu, ni wakati muafaka sasa wa kufanya maandalizi mazuri ya kujihami kwa mvua hizo zijazo, maandalizi yatakayohitaji pia kuhifadhi chakula cha kutosha majumbani.
Tumekuwa mashahidi wa kuona namna mvua kubwa zinavyoathiri uchumi wa mtu mmoja mmoja na hata kwa taifa pia, mazao ya chakula yanategemea kwa asilimia kubwa kilimo kinachotegemea mvua, ingawa mvua za masika hii, zinaweza kuwa kubwa kupita kiasi na kusababisha mazao yasikomae na ikawa njaa kwa msimu ujao.
Tunaamini taarifa za TMA zinaweza kunusuru wananchi wengi na mvua hizo za kimbunga, na hili litategemea namna wananchi watakavyozingatia na kuchukua tahadhari muhimu ili kuepuka madhara yaliyokwisha tolewa awali.
Ni imani yetu kuwa kila wakati TMA itakuwa ikitoa tahadhari kwa maeneo yatakayoathirika zaidi, ni wajibu wa wananchi kuzingatia tahadhari za aina hiyo ili kujinusuru na madhara ya mvua zijazo.










