Ustawi wa sekta ya michezo, siyo tu kujenga viwanja bora, kufungua vituo vya kukuza vipaji au kuweka bajeti kubwa katika sekta hiyo.
Kuna jambo moja zaidi ya hayo. Nidhamu ya wachezaji wetu. Sisi kama wanamichezo tunaamini kuwa, kipaji na nidhamu ya mchezaji huenda sambamba.
Ni jambo lililo wazi kuwa, mchezaji mwenye kipaji, ni lazima awe na nidhamu kwa sababu hali hiyo itampa nafasi ya kulinda kipaji chake.
Kutegemea kipaji bila nidhamu, hakuwezi kumfanya mchezaji afikie mafanikio. Nidhamu ndiyo itakayomwezesha kuzingatia mazoezi, kufuata maelekezo ya namna kulinda kipaji chake.
Nidhamu ya mchezaji pia ni sehemu ya kumjengea uhusiano mzuri na wachezaji wanzake, viongozi na walimu wake. Nidhamu nzuri ya mchezaji pia ni alama ya kupendwa na mashabiki.
Zaidi ya hayo, nidhamu ya mchezaji hapaswi kuwa na mipaka. Kwamba, anapaswa kuzingatia nidhamu anapokuwa uwanjani na anapokuwa mtaani anafanya mambo kinyume na maadili.
Mchezaji anapaswa kuwa mfano wa kuigwa mbele ya jamii ndani na nje ya uwanja. Ndiyo maana, nchi za wenzetu wanaojali ustawi wa maadili, huweza kumchukulia hatua mchezaji na hata kumfukuza kwa matendo yake mabaya siyo uwanjani, bali nje ya uwanja.
Leo hii Tanzania tuna tatizo la wachezaji wetu kupotea kwenye soka mapema kuliko kama ambavyo tumekuwa mashuhuda nchi nyingine.
Hakuna tena taswira ya wachezaji waliowahi kucheza muda mrefu. Hakuna tena wachezaji wa aina ya Omar Hussein, Madaraka Seleman, Edibily Lunyamila. Wachezaji wetu wa sasa wakifika miaka 30 wanakuwa tayari wameshapotea kwenye soka.
Upo mfano. Mchezaji wa timu ya PSG ya Ufaransa, Zlatan Ibrahimovic ana miaka 34 sasa na bado anaendelea kuwa keki Ulaya akiwindwa na klabu kubwa England kama Manchester United na Arsenal.
Lakini wachezaji wetu hawawzi kucheza kwa mafanikio baada ya 30, kwamba wakishafika umri huo au hata kabla wanakuwa tayari wameshachoka kisoka.
Kuna mambo kadhaa yanaweza kuinishwa kama sababu. Ukosefu wa uwekezaji wa maana katika soka la vijana nchini ni mojawapo. Tuna wachezaji wengi wana vipaji, lakini wanapotea mapema kwa vile hakuna njia bora za kuwatunza.
Ili kipaji kidumu muda mrefu, ni lazima kitunzwe. Kwa wachezaji wetu, hakuna anayeshughulika kuwatunza, siyo wao wenyewe tu bali hata mamlaka husika za usimamizi wa soka.
Hakuna bajeti ya maana kutoka serikalini katika kuwekeza soka la vijana kama ambavyo wenzetu wanafanya. Tunaangalia zaidi wachezaji wakubwa ambao hawana muda mrefu uwanjani.
Liko tatizo lingine, ambalo ni wachezaji wenyewe kushindwa kujitambua. Labda ni kutokana na ukosefu wa elimu, au kuathiriwa na mkumbo.
Kuwa elimu ndogo, kumewafanya kushindwa kujitambua au kutambua umuhimu wao.
Kushindwa kwao kujitambua, kumewafanya kujiingiza kwenye mambo mengi mabaya ambayo yanahatarisha uhai wa vipaji vyao. Matumizi ya dawa za kulevya, bangi, ulevi kupindukia ni hatari kwao.
Ukitaka kujua haya, nenda kushuhudia mechi za michangani ambao ndiko chimbuko la wachezaji wengi chipukizi wanaokuja kucheza timu kubwa za Ligi Kuu.
Wengi wa wachezaji wetu wanakosa misingi bora ya namna ya kutuza vipaji vyao. Viongozi wao ni moja ya sababu.
Leo hii ni jambo la kawaida kumkuta kiongozi wa klabu akiwa kwenye starehe usiku na wachezaji wake. Wanafanya kila linalowezekana kustarehe, hakuna anayejali.
Mchezaji anapotoka, anaona kwa kuwa yuko na kiongozi basi suala la kula raha kupindukia ni haki yake. Jiulize, mchezaji anayekesha kwenye majumba ya starehe atawezaje kuamka asubuhi kufanya mazoezi?
Ni mchezaji gani anayeweza kufanikiwa kwa kufikiria zaidi starehe kuliko kujituma kufanya mazoezi ili kulinda kipaji chake kitakachompa fursa ya kucheza muda mrefu?
Wachezaji wenyewe wamekosa uelewa, wamepotoshwa na kukubali kwenda njia isiyo sahihi. Sasa kwa hali kama hii kwanini wachezaji wetu tusiwaone wazee wakifika miaka 30?Nipashe, tunashauri, matunzo mazuri ya kipaji ni lazima yaanzie kwa mchezaji mwenyewe. Kama huonyeshi nia ya kutunza kipaji chake, nani atasaidia? Ni wakati wa kubadilika sasa.










