Mpango huo uliwasilishwa juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akisema serikali iatatumia Sh. trilioni 21.4 kila mwaka kukamilisha kutekeleza mpango huo.
Katika utekelezaji wa mpango huo, serikali itachangia Sh. trilioni 59 (sawa na Sh. trilioni 11.8 kila mwaka), huku Waziri Mpango akisema kutakuwa na ongezeko kubwa la fedha zinazohitajika kugharamia mpango huo ikilinganishwa na mpango wa kwanza.
Kwa mujibu wa Waziri Mpango, mpango huo umelenga kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu na kufikia malengo ya serikali ya kupunguza umaskini na kwamba watu milioni 10 nchini ni maskini, idadi ambayo ni kubwa kulinganishwa na nchi nyingi barani Afrika.
Sababu inayotajwa kuchangia hali hiyo ni kutoshiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, biashara na faida ndogo katika sekta ya kilimo ambayo ndiyo mhimili wa watu wengi wanaishi vijijni.
Pamoja na serikali kusema kuwa mpango huo utatumia fedha nyingi zaidi kuliko wa kwanza, lakini changamoto ya kuwapo idadi kubwa ya watu maskini wakiwamo vijana 800,000 inahitaji kutafutiwa ufumbuzi.
Kinashoshangaza ni kuwa serikali imekuwa ikipanga mipango, sera na mikakati kwa muda mrefu ya kupunguza umaskini, lakini takwimu zinazotolewa za kuongezeka kwa wananchi maskini zinaonyesha kuwa utekelezaji wa mipango hiyo, sera na mikakati una walakini, kwa sababu kama ingekuwa wa tija na ufanisi, idadi ya Watanzania maskini ingekuwa inazidi kupungua mwaka hadi mwaka.
Miongoni mwa mipango ambayo serikali imekuwa ikiitekeleza kwa lengo la kupunguza umaskini ni Mkukuta na Mkurabita, lakini tunaposikia taarifa za kuongezeka kwa idadi ya watu maskini nchini ni lazima tuhoji inakuwaje wakati serikali ikekuwa ikitumia fedha nyingi kutekeleza mipango ya kupinguza tatizo hilo.
Inawezekana kuwa tatizo hilo linatokana pengine na kutofanyia tathmini ya utekelezaji wa mipango na mikakati hiyo kama ulikuwa wa tija na ufanisi ili kubadilisha mbinu za utekelezaji.
Tunaishauri serikali kuhakikisha kwamba fedha zitakazotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa kupindi hicho zinasaidia kupunguze umaskini wa wananchi. Kwa maana hiyo, ni matumaini yetu kuwa maeneo muhimu yanayowagusa wananchi yatengewa na kupelekewa fedha za kutosha ili kuleta mabadiliko.
Baadhi ya sekta ambazo zikitengewa na kupelekewa fedha za kutosha zinaweza kuonyesha mabadiliko ni maji, elimu, afya, miundombimu pamoja na mifuko ya kuwezesha jamii kwa mikopo maka baadhi ya wabunge waliochangia mjadala huo walivyoshauri.
Jambo muhimu ni kufanyika kwa tathmini mara kwa mara kubaini kama utekelezaji wa mipango, sera na mikakati unafikia malengo. Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Nne ilianzisha Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), itakuwa vizuri kuendelea kuutumia kwa ajili ya kupima mafanikio katika sekta mbalimbali.










