Ni mradi ulioanza kutekelezwa mwezi Januari mwaka huu na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Awamu ya kwanza ya utekelezaji mradi huo, ilianza kwa miundombinu ya barabara yenye urefu wa kilomita 1.8 pamoja na ujenzi wa kituo kipya cha mabasi ya mikoani cha Manispaa ya Singida.
Miji mingine iliyopo katika mradi huo Babati, Geita, Bariadi, Musoma, Bukoba,
Shinyanga, Tabora, Sumbawanga, Mpanda,Songea, Moshi, Lindi, Kibaha, Morogoro, Manispaa ya Singida, Korogwe, Iringa na Njombe.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Deus Luzige, anaeleza changamoto zinazoukabili mradi huo anaoutaja ni wa manufaa makubwa kwa wananchi wa Singida, kwa upatikanaji huduma mbalimbali.
Luzige anafafanua kwamba, katika kutekeleza mradi huo, wameanza kujenga barabara yenye urefu wa kilomita 1.8 na kituo kikuu kipya cha mabasi yaendayo mikoani na wilayani.
Anasema katika kutengeneza barabara hiyo, walikaa na wadau mbalimbali likiwemo Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco).
Pia, zimo kampuni za simu na vituo vya kuuza mafuta ambavyo miundombinu ya barabara inapita kwenye maeneo yake na makubaliano yaliyopo ni miundombinu hiyo ihamishwe.
Anabainisha kwamba, mkakati mwingine ni kuhakikisha miundombinu yote ya maji iwe imehamishwa, ili kumsaidia mkandarasi awe huru na barabara zitakazofanyiwa kazi,lakini changamoto iliyopo ni kwamba mkandarasi amekuwa akikutana na mfumo wa mabomba ya maji yanayokwaza kazi zake.
“Fedha tulizolipa zilikuwa Sh. milioni kumi kama tulivyokubaliana kuchangia kuhamisha miundombinu ya maji, kwa maana kwamba miundombinu yote ya maji iwe imehamishwa ili mkandarasi awe huru na barabara hiyo kuendelea kuitengeneza,” anasema Luzige, ambaye ni mchumi wa Manispaa ya Singida
Analalamika kwamba, mamlaka inayohusika na usimamizi wa mabomba hayo inachelewa kuhamisha miundombinu ya maji, jambo linalochelewesha malengo muhimu ya ujenzi huo wa barabara.
“Tunajua kuwa extension of time (muda uliosogezwa) maana yake kwa mkandarasi lazima kuna gharama zitaongezeka. Kwa hiyo, tunasihi SUWASA (Mamlaka ya Majisafi na Majitaka) ikamilishe haraka kuondoa miundombinu yote ya maji.
Mhandisi wa ujenzi wa Manispaa ya Singida, Lambert Bayona, anasema ujenzi wa barabara hiyo inayoanzia kwenye makutano ya Barabara za Karume na Mtaa wa Semali Baa na kisha kituo kikuu kipya cha mabasi yaendayo mikoani.
Mhandisi huyo anasema kituo hicho kitakapokamilika, kitakuwa na uwezo wa kuchukua mabasi ya kwenda mikoani yasiyopungua 72 na mabasi madogo ya kwenda wilayani yasiyopungua 48.
Ni kituo kinachoelezwa kitakuwa na fursa ya abiria kukaa, pia wasindikizaji.
Hata hivyo, anasema baada ya tukio hilo walikwenda kuonana na Mhandisi wa Ujenzi wa Manispaa ya Singida na kumpa ushauri, kwa sababu mitandao ya mabomba inafahamika, hivyo ni vyema wakamtahadharisha mkandarasi anayefanya kazi hiyo.
Mhandisi huyo anaeleza zaidi kuwa tangu ujenzi wa mradi ulipoanza miezi mitatu iliyopita, ofisi yake ilishapeleka maandishi ya kuifahamisha mamlaka hiyo inayohusika na maji, kuhusu hasara iliyofikwa.
Mmoja wa wakazi wa Mjini Singida, Saad Mangala, anaeleza kutoridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa miundombinu ya barabara na kituo kikuu kipya cha mabasi cha mjini Singida unavyoendelea.
“Mkandarasi asije akasingizia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Manzingira (SUWASA) kuwa ndiyo inayowachelewesha” anasisitiza Mangala.










